Walimu, Ninyi ndio Mnaojifunza, Wanafunzi wenu ni Wapokea Taarifa tu
Picha kwa hisani ya www.jiandae.wordpress.com
Kuna msemo usemao, kati ya anayefundisha na anayefundishwa, anayejifunza zaidi ni yule anayefundisha/ elekeza. Msemo huu una ukweli kwa kuwa, anayefundisha hujiandaa kwa kila hali na pia kupata fursa ya kutumia kile alichojifunza kwa kuelekeza wenzake.
Msemo huu bila shaka, chanzo chake ni aina ya ufundishaji wa
muda mrefu uliozoeleka mashuleni. Kwamba, mwalimu ndiye anayepaswa kusoma kwa
kina na kisha kuwaeleza wanafunzi dhana ya yale aliyoyasoma. Kimsingi, mwalimu
anatoa taarifa ya alichojifunza kile wanafunzi wanachopaswa kukijifunza.
Bila shaka unaweza ukashangazwa au kupata mshtuko, lakini
hali halisi ndio hii.
Kabla ya kufundisha, mwalimu anapaswa kujiandaa na somo. Kwa
mtazamo wa ufundishaji wa walimu wengi, jukumu lao kubwa ni kujisomea ili
wapate uelewa wa kutosha kuhusu kile wanachopaswa kukifundisha. Utaratibu huu
unaenda sambamba na uandaaji wa nukuu za somo. Mara chache sana walimu
watajibidisha kuandaa zana za kufundishia. Labda pale panapokuwa na ukaguzi
maalum.
Hata hivyo, ieleweke vizuri kwamba, mwalimu kuwa na uelewa
wa kutosha kuhusu kile anachopaswa kukisimia wakati wa ujifunzaji darasani ni
jambo la msingi sana. Ni muhimu msimamizi wa jambo akawa na uelewa mpana wa
jambo analolisimamia.
Hata hivyo, suala la msingi la kujiuliza ni kuwa, mwalimu
anajifunza ili akawaelekeze wanafunzi kile alichojifunza au wanafunzi nao kama
mwalimu wao, wanapaswa kupatiwa muda wa kujijengea uelewa wao wa yale wanayopaswa
kujifunza?
Walimu wanatumia vyanzo vipi kujifunzia ambavyo wanafunzi
hawawezi nao kujisomea na wakajenga uelewa wao?
walimu wanapojiuliza maswali haya, hawana budi kutafakari na
kukubaliana nami kuwa, wao ndio wajifunzaji wakuu na wanafunzi wanabaki kuwa
wasikilizaji wakuu wa yale mwalimu aliyojifunza kwa ajili ya kile kinachoitwa
kufundisha.
Wakati hali ikiwa hivi kwenye madarasa yetu, nini kifanyike?
Kwanza, walimu watambue wajibu wao mkuu. Katika Makala hii
iliyotangulia, nilijaribu kufafanua yale mwalimu anayopaswa kufanya wakati wa
uwezeshaji wake chini ya ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi.
Kwa kuwekea mkazo, mwalimu anapaswa kutambua, kujiandaa kwa
kujifunza kile anachopaswa kukisimamia wakati wa ujifunzaji wa wanafunzi ni
muhimu. Pia, mwalimu anapaswa kufahamu kuwa, kwenye ufundishaji wa kiudadisi/
unaomzingatia mwanafunzi, mwanafunzi ana wajibu wa kujijengea uelewa wake
mwenyewe. Hii ni kusema kuwa, darasa linapaswa kuwa karakana ya kujifunzia
kuliko kuwa ukumbi wa kutolea taarifa za ujifunzaji wa mwalimu.
Wajibu mwingine na wa muhimu sana wa mwalimu ni kufikiria
aina ya nyenzo atakazozipeleka darasani kwa ajili ya mwanafunzi kujifunzia. Hapa
mwalimu anapaswa atumie muda wake mwingi kutafuta vyanzo vya nyenzo za
kujifunzia zikiwemo nyenzo alizozitumia yeye wakati akijijengea uelwa wake wa
kile anachokusudia kukipeleka darasani wanafunzi wakajifunze.
Aina na namna ya kuwasilisha nyenzo za ujifunzaji darasani
huweza kutegemea na namna mwalimu
alivyopanga wanafunzi wajifunze.
Kwa mazingira ya Tanzania ambayo nyenzo za kufundishia
zinapatikana kwa uchache, walimu hawana budi kujiuliza namna wanavyoweza
kutumia nyenzo hizo chache. Uchache wa nyenzo unaweza kuamua aina ya ujifunzaji
na namna ya kuwasilisha nyenzo hizo darasanni.
Ifahamike kuwa, zipo mbinu/ namna nyingi sana za namna
ambavyo mwalimu anavyoweza kusimamia ujifunzaji wa wanafunzi. Namna hizo ni
kama vile kufanya majadiliano darasani, kufanya shughuli za mradi, kutembelea
mahali, changanya kete, onesho mbinu, bungua bongo na namna nyingi.
Changamoto kubwa ni kuwa, kwa kila mbinu ya ujifunzaji,
walimu wengi huwa hawawapatii wanafunzi nyenzo za kujifunzia. Wanafunzi
wanawekwa kwenye makundi na kupewa kazi ya kufanya bila kuwa na nyenzo za
kuwasadia kufanya kazi hiyo. Wanafunzi wanatumia uzoefu wao (ambalo ni jambo
jema) na kisha wanakosa fursa ya kufanya utafiti zaidi kuona wengine wamefanya
nini au wanasema nini kuhusu wanachopaswa kujifunza na kisha kujenga uelewa
wao.
Kwa kuhitimisha, niwakumbushe walimu kuwa, mfumo wa
ujifunzaji wanaoutumia kwa sasa, walimu ndio wanajifunza zaidi kuliko wanafunzi
ambao ndio walengwa wa ujifunzaji. Tutafakari kwa pamoja na kisha tuchukue
hatua stahiki. Wapeni wanafunzi fursa ya kujifunza bila kujali upungufu wa
nyenzo wala muda. Muda upo pamoja na kuwa hautoshi. Nyezo zipo, pamoja na kuwa
hazitoshi.
Ni bora kuanza kufanya jambo sahihi kwa kutumia rasilimali
chache zilizopo kuliko kutokufanya jambo sahihi na kuendelea kulalamika kuhusu
upungufu wa nyenzo za kufundishia na uchache wa muda. Tutekeleze ufundishaji
unaomzingatia mwanafunzi kwa kuzingatia mazingira yetu. Ni rahisi kumweleza mtu
changamoto zinazotokana na jambo unalolitekeleza kwa wakati huo kuliko
kumwambia changamoto za jambo ambalo halijaanza kutekelezwa.
Comments
An Thái Sơn chia sẻ trẻ sơ sinh nằm nôi điện có tốt không hay võng điện có tốt không và giải đáp cục điện đưa võng giá bao nhiêu cũng như mua máy đưa võng ở tphcm địa chỉ ở đâu uy tín.