Walimu, Ninyi ndio Mnaojifunza, Wanafunzi wenu ni Wapokea Taarifa tu



                                            Picha kwa hisani ya www.jiandae.wordpress.com
                                                                             
Kuna msemo usemao, kati ya anayefundisha na anayefundishwa, anayejifunza zaidi ni yule anayefundisha/ elekeza. Msemo huu una ukweli kwa kuwa, anayefundisha hujiandaa kwa kila hali na pia kupata fursa ya kutumia kile alichojifunza kwa kuelekeza wenzake.

Msemo huu bila shaka, chanzo chake ni aina ya ufundishaji wa muda mrefu uliozoeleka mashuleni. Kwamba, mwalimu ndiye anayepaswa kusoma kwa kina na kisha kuwaeleza wanafunzi dhana ya yale aliyoyasoma. Kimsingi, mwalimu anatoa taarifa ya alichojifunza kile wanafunzi wanachopaswa kukijifunza.  

Bila shaka unaweza ukashangazwa au kupata mshtuko, lakini hali halisi ndio hii.
Kabla ya kufundisha, mwalimu anapaswa kujiandaa na somo. Kwa mtazamo wa ufundishaji wa walimu wengi, jukumu lao kubwa ni kujisomea ili wapate uelewa wa kutosha kuhusu kile wanachopaswa kukifundisha. Utaratibu huu unaenda sambamba na uandaaji wa nukuu za somo. Mara chache sana walimu watajibidisha kuandaa zana za kufundishia. Labda pale panapokuwa na ukaguzi maalum. 

Hata hivyo, ieleweke vizuri kwamba, mwalimu kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kile anachopaswa kukisimia wakati wa ujifunzaji darasani ni jambo la msingi sana. Ni muhimu msimamizi wa jambo akawa na uelewa mpana wa jambo analolisimamia. 

Hata hivyo, suala la msingi la kujiuliza ni kuwa, mwalimu anajifunza ili akawaelekeze wanafunzi kile alichojifunza au wanafunzi nao kama mwalimu wao, wanapaswa kupatiwa muda wa kujijengea uelewa wao wa yale wanayopaswa kujifunza?

Walimu wanatumia vyanzo vipi kujifunzia ambavyo wanafunzi hawawezi nao kujisomea na wakajenga uelewa wao? 

walimu wanapojiuliza maswali haya, hawana budi kutafakari na kukubaliana nami kuwa, wao ndio wajifunzaji wakuu na wanafunzi wanabaki kuwa wasikilizaji wakuu wa yale mwalimu aliyojifunza kwa ajili ya kile kinachoitwa kufundisha. 

Wakati hali ikiwa hivi kwenye madarasa yetu, nini kifanyike? 

Kwanza, walimu watambue wajibu wao mkuu. Katika Makala hii iliyotangulia, nilijaribu kufafanua yale mwalimu anayopaswa kufanya wakati wa uwezeshaji wake chini ya ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi. 

Kwa kuwekea mkazo, mwalimu anapaswa kutambua, kujiandaa kwa kujifunza kile anachopaswa kukisimamia wakati wa ujifunzaji wa wanafunzi ni muhimu. Pia, mwalimu anapaswa kufahamu kuwa, kwenye ufundishaji wa kiudadisi/ unaomzingatia mwanafunzi, mwanafunzi ana wajibu wa kujijengea uelewa wake mwenyewe. Hii ni kusema kuwa, darasa linapaswa kuwa karakana ya kujifunzia kuliko kuwa ukumbi wa kutolea taarifa za ujifunzaji wa mwalimu. 

Wajibu mwingine na wa muhimu sana wa mwalimu ni kufikiria aina ya nyenzo atakazozipeleka darasani kwa ajili ya mwanafunzi kujifunzia. Hapa mwalimu anapaswa atumie muda wake mwingi kutafuta vyanzo vya nyenzo za kujifunzia zikiwemo nyenzo alizozitumia yeye wakati akijijengea uelwa wake wa kile anachokusudia kukipeleka darasani wanafunzi wakajifunze. 

Aina na namna ya kuwasilisha nyenzo za ujifunzaji darasani huweza kutegemea na  namna mwalimu alivyopanga wanafunzi wajifunze. 

Kwa mazingira ya Tanzania ambayo nyenzo za kufundishia zinapatikana kwa uchache, walimu hawana budi kujiuliza namna wanavyoweza kutumia nyenzo hizo chache. Uchache wa nyenzo unaweza kuamua aina ya ujifunzaji na namna ya kuwasilisha nyenzo hizo darasanni. 

Ifahamike kuwa, zipo mbinu/ namna nyingi sana za namna ambavyo mwalimu anavyoweza kusimamia ujifunzaji wa wanafunzi. Namna hizo ni kama vile kufanya majadiliano darasani, kufanya shughuli za mradi, kutembelea mahali, changanya kete, onesho mbinu, bungua bongo na namna nyingi.

Changamoto kubwa ni kuwa, kwa kila mbinu ya ujifunzaji, walimu wengi huwa hawawapatii wanafunzi nyenzo za kujifunzia. Wanafunzi wanawekwa kwenye makundi na kupewa kazi ya kufanya bila kuwa na nyenzo za kuwasadia kufanya kazi hiyo. Wanafunzi wanatumia uzoefu wao (ambalo ni jambo jema) na kisha wanakosa fursa ya kufanya utafiti zaidi kuona wengine wamefanya nini au wanasema nini kuhusu wanachopaswa kujifunza na kisha kujenga uelewa wao. 

Kwa kuhitimisha, niwakumbushe walimu kuwa, mfumo wa ujifunzaji wanaoutumia kwa sasa, walimu ndio wanajifunza zaidi kuliko wanafunzi ambao ndio walengwa wa ujifunzaji. Tutafakari kwa pamoja na kisha tuchukue hatua stahiki. Wapeni wanafunzi fursa ya kujifunza bila kujali upungufu wa nyenzo wala muda. Muda upo pamoja na kuwa hautoshi. Nyezo zipo, pamoja na kuwa hazitoshi. 

Ni bora kuanza kufanya jambo sahihi kwa kutumia rasilimali chache zilizopo kuliko kutokufanya jambo sahihi na kuendelea kulalamika kuhusu upungufu wa nyenzo za kufundishia na uchache wa muda. Tutekeleze ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi kwa kuzingatia mazingira yetu. Ni rahisi kumweleza mtu changamoto zinazotokana na jambo unalolitekeleza kwa wakati huo kuliko kumwambia changamoto za jambo ambalo halijaanza kutekelezwa.


Comments

ngoclan said…
Thanks for sharing, nice post! Post really provice useful information!

An Thái Sơn chia sẻ trẻ sơ sinh nằm nôi điện có tốt không hay võng điện có tốt không và giải đáp cục điện đưa võng giá bao nhiêu cũng như mua máy đưa võng ở tphcm địa chỉ ở đâu uy tín.

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?