Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?


Kila mwanafunzi anajituma wakati wa kujifunza katika harakati za kufikia malengo yao ya ujifunzaji.


Picha: Mwandishi wa makala

Kama mnakumbuka, kati ya mwaka 2005 na  2007 yalitokea mabadiliko ya mitaala, hususani kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya Ualimu. Kulikuwa na msemo uliovuma sana wa "muhamo wa ruwaza" au "paradigm shift" kwa kiingereza.

Ruwaza ni mfumo au imani inayomuwezesha mtu kutekeleza jambo fulani kulingana na matakwa na taratibu fulani zinazofahamika. Kwenye ufundishaji, iliaminika kuwa mitaala yetu ilikuwa ya mfumo unaomuona mwalimu kama chanzo cha maarifa na mwanafunzi kama pipa linalosubiri kujazwa tu maarifa.

Mitaala mipya inaaminika kuwa ya ruwaza tofauti, ndio maana mabadiliko haya yakaitwa ya kuhama kwa ruwaza. Namna mitaala ilivyoandikwa na namna ya kuitekeleza ni miongoni mwa mabadiliko haya. Kwa mfano, mabadiliko haya yalipelekea maandalio ya masomo yawe na kipengele cha upimaji kwa kila hatua ya somo. Pia, zimependekezwa njia na mbinu anuai za kufundishia na kujifunzia zinazoakisi mabadiliko haya.

Hata hivyo, tafiti nyingi zinazoangalia kiwango cha utekelezaji wa mitaala hii mashuleni zinaonesha kuwa kumekuwa na changamoto kadhaa zinazokwamisha utekelezaji wake. Miongoni mwa changamoto hizo ni uelewa usioridhisha wa walimu kuhusu misingi ya mitaala yenyewe na namna inavyoweza kutekelezwa.

Makala haya yanalenga kujadili namna anuai walimu na wanafunzi wanavyoweza kubadilika ili kuendana na mabadiliko ya mitaala yaliyoruhusu ufundishaji na ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi.

Majukumu ya Mwalimu na Mwanafunzi

Kwanza, ni muhimu kufahamu kuwa, shughuli nyingi za ujifunzaji zinapaswa kuachwa kwa wanafunzi. Mwalimu ana wajibu wa kumsaidia mwanafunzi kufahamu vizuri mambo anayopaswa kuyajifunza. Mchakato huu huwa mrahisi sana ikiwa mtaala husika utaandaliwa vizuri. 

Kwa ufafanuzi wa kina wa mitaala, siwezi kuchoka kupigia mfano mitaala ya NACTE. Kwa maoni yangu, hii ni moja ya mitaala bora kabisa ambayo anayeitekeleza hutumia nguvu kidogo mno kumsaidia mwanafunzi kuelewa kile anachopaswa kujifunza. Unaweza kurejea makala haya hapa ili kufahamu kwa kuchache kuhusu uzuri wa mitaala ya NACTE. 

Pili, mwalimu ana wajibu wa kuwaza ni kazi gani mwanafunzi anapaswa kuzifanya ili afikie malengo ya ujifunzaji yaliyokusudiwa. Hali ilivyo sasa ni tofauti kabisa. Mwalimu anapojiandaa na somo, anafikiria yeye atafanya nini, pengine kutoa ufafanuzi wa maudhui au kufanya mifano kadhaa huku akiongozwa na muda wa kipindi. 

Kwa mfano, mwalimu anajiandaa na maudhui fulani au ameejiandaa kufanya mifano kadhaa, akiamini kuwa, hadi atakapomaliza kuyaelezea au kufanya mifano, kipindi kitakuwa kimeisha. Hali inapaswa kuwa tofauti kabisa ikiwa tuna nia ya dhati ya kuwafanya wanafunzi wajifunze.

Mwalimu anapaswa kuwaza ni kwa namna gani wanafunzi watumia "resources" kujifunza maudhui fulani wao wenyewe lakini kwa usimamizi wa karibu mno wa mwalimu. Kulingana na upatikanaji wa "resources", hapa mwalimu anapaswa pia kuwaza ni kwa  namna gani wanafunzi watajifunza. Ama kujifunza kwa makundi, kufanya kazi mradi, vikundi vidogo vidogo vya majadiliano au mmoja mmoja. 

Utekelezaji wa mtazamo huu unaweza kuonekana kwenye jambo dogo ambalo halihitaji sana uwekezaji. Mwalimu anaweza kuongoza mjadala  na wanafunzi kuhusu mada fulani ili kujenga uelewa. Kisha,  mwalimu anakuwa ameandaa changamoto kadhaa ambazo wanafunzi wanaweza kushughulika nazo kuzitatua kwa kutumia maarifa waliyoyapata.

 Jambo la muhimu ni uwepo wa mwalimu wakati wote ili aendelee kujadiliana na wanafunzi pale wanapomuhitaji, kupitia kuona wanafunzi wanavyofanya kazi zao na kufanya tathmini ya maendeleo yao. Hapa mwalimu anaweza kubaini ubora na udhaifu wa kama si mwanafunzi mmoja mmoja, basi wanafunzi wote. Kwa namna hii, taratibu ufundishaji unaweza kuanza kuwa na maana na wenye tija.

Video hapa chini ni darasa langu. Waalimu wanafunzi wanajifunza Calculus. Ukiwaangalia vyema, utaona kila mmoja anafanya kazi lakini kwa kujadiliana na mwenzake. Hapa wanatatua changamoto za kukadiria majibu ya milinganyo sahili kwa kutumia fomula ya Newton-Raphson.

Nilipendezwa na ubunifu wa mwanafunzi mmoja aliyekuwa akitafuta namba ya kianzio ili aweze kuitumia sambamba na kanuni ya Newton-Raphson ili kutafuta kipeuo cha pili cha 10. Aliona kujaribu namba nyingi kuanzia 1 na kuendelea kungemchukulia muda. Badala yake, alijiuliza ikiwa kuna namba zinazokaribia kumi na mbazo kipeuo chake cha pili kinafahamika kwa urahisi. Alipata kuwa ni 9 na 16, kisha akatafuta kipeuo cha pili cha namba hizi, ambazo ni 3 na 4. akagundua kuwa, namba ya kianzio lazima itakuwa kati ya tatu na nne. Mambo yalikuwa marahisi kwake. 

Nilimpongeza mwanafunzi huyu. Nilimueleza, ubunifu wa namna hii siyo tu utamfaa wakati akisoma, bali hata atakapokwenda kwenye soko la ajira.  Anaweza akawa siyo miongoni mwa wale wanaolalamika kuwa wamekosa ajira na hawana la kufanya. Ubunifu na utayari wa kutatua changamoto za darasani ni maandalizi kabambe ya kuwa na uwezo wa kujiajiri na kukabiliana na hali ya ukosefu wa ajira.

Dhana kubwa hapa ni kuwa, walimu wanapaswa kuyaona madarasa kama "karakana" za kujifunzia. Wanafunzi ndio wanaopaswa kushughulika muda mwingi na muda wa nje ya darasa uwe ni wa kufanya shughuli nyingine za ziada. 

Hebu mtazame mwanafunzi kama fundi Seremala kwenye karakana yake (darasa). Itakuwa jambo la kushangaza ikiwa fundi huyu atakaa siku nzima, au lisaa limoja bila ya kuwa na chochote alichokifanya, Hali hii inashangaza vilevile hata kwa wanafunzi. Mwanafunzi masaa mawili au limoja, amekaa tu anamsikiliza mwalimu.

Ufundishaji wa namna hii, walimu wanabaki kuwa ndio wajifunzaji wakuu kwani wao ndio watendaji wakuu na wanafunzi wanabaki kuwa watazamaji wa ujifunzaji wa mwalimu, au wajifunze kwa uchache sana au wasijifunze kabisa. 

Malengo ya Maudhui Yanayofundishwa

Ili kubaini umuhimu wa mabadiliko ya mitaala, ni muhimu sana kufahamu wanafunzi wanajifunza maudhui fulani kwa malengo yapi. Hali ilivyo sasa, lengo la maudhui yanayofundishwa ni kufanya mwanafunzi ayafahamu maarifa hayo ili akayatumie mbele ya safari. Lengo ambalo halijitoshelezi kabisa. Ndio maana imekuwa vigumu sana kujibu swali hili maarufu, "mwalimu logarithm nitaitumia wapi kwenye maisha?"

Kwenye ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi, maudhui wanayojifunza wanafunzi yanapaswa kuonwa kama namna ya kuwajengea msingi wa kujenga maarifa, kukuza stadi za ujifunzaji na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitawala na kujitambua. 

Sina hakika kama unafahamu kuwa, katika karne hii, kuna stadi muhimu ambazo zinategemewa kwa kila mhitimu. Stadi zinazoaminika kuwa mtu akiwa nazo, zitamsaidia kujiajiri, kuajirika na hata kuweza kumudu maisha yake vyema.

Stadi hizi ni ubunifu, fikra tunduizi, Uwezo wa kutatua changamoto, ushirikiano na mawasiliano. Tunaweza kukubalina kuwa, stadi hizi hakuna somo maalum za kuzifundisha. Hata lingekuwepo, ufanisi wa ujifunzaji wake usingeonekana. Huu ndio ukweli. Ni kama Kiingereza kinavyotupiga chenga pamoja na kukitumia karibu maisha yetu yote ya kusoma. 

Namna tunavyojifunza maudhui haya ina mchango mkubwa sana kwenye kujijengea uwezo katika stadi hizi. Mfumo wa elimu nao una nafsi kubwa sana. Tujiulize elimu ya msingi lengo lake ni nini haswa? Kumbuka kwa Tanzania, elimu ya msingi kwa sasa ni hadi kidato cha nne.

Hivi kwenye elimu ya msingi ni kujifunza stadi muhimu za kusoma, kuandika na kuhesabu tu?. Hadi mtoto anamaliza kidato cha nne, anapswa kuwa na stadi zipi? Stadi nilizozitaja zinapaswa kuwa zimeshajipambanua vya kutosha sana nikijazia na stadi ya kujua namna bora ya kujifunza. Kuanzia kidato cha tano na kuendelea, pamoja na kuwa mwanafunzi atakuwa anaendelea kukuza stadi hizi, anatarajiwa kuzitumia zaidi kwenye kujenga msingi imara wa maarifa, ujuzi na mielekeo sambamba na kujitambua zaidi. 

Itaendelea...
















Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.