Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija
Upimaji
endelevu wa mwanafunzi ndio namna pekee ya kutoa taarifa za maendeleo ya
ujifunzaji wa mwanafunzi katika kufikia malengo ya ujifunzaji yaliyokusudiwa kwake. Kwa
hiyo, upimaji endelevu ni shuhguli ya msingi mno ya kuzingatiwa na mwalimu na
wanafunzi.
Upimaji
endelevu siyo shughuli ya mwalimu peke yake. Ni mchakato wa pamoja kati ya
mwalimu na manafunzi. Hii ni kusema kuwa, upimaji endelevu ni sehemu ya
ujifunzaji wa mwanafunzi na ufundishaji wa mwalimu. Ikiwa tunahitaji kuona upimaji wenye tija, basi kila mmoja ni lazima atimize wajibu wake kwa kushirikiana.
NWEA katika
chapisho lao la mwaka 2016 linaloelezea mambo makuu manne ya kuzingatia ili kuleta ufanisi kwenye upimaji endelevu, wanaeleza kuwa upimaji endelevu ni mchakato wa pamoja kati ya mwalimu na wanafunzi
wa kukusanya ushahidi wa ujifunzaji wa wanafunzi kwa lengo la kuboresha kile
kinachoendelea darasani, kwa maana ya mchakato wa ujifunzaji wa wanafunzi.
Ili kufanya mchakato
wa upimaji endelevu kuwa wa mafanikio, wanafunzi wanapaswa kusaidiwa na
mwalimju wao kuwa na majibu ya maswali matatu makuu. Kwanza, hadi mwisho wa
kipindi, mada au kozi, wanafunzi wanapaswa kuwa wamejifunza nini, wanafunzi
wamefikia wapi katika ujifunzaji wao na ni kwa namna gani watakamilisha kile
ambacho hawajajifunza ili wafikie malengo yao ya ujifunzaji.
Maswali hapo
juu ni muhimu sana yakaweza kujibiwa na wanafunzi wenyewe kwa kushirikiana na
mwalimu wao. Mchakato huu ili uwezekane unahitaji utamaduni mzuri wa kuwajumuisha
na kuwashirikisha wanafunzi kwenye upimaji endelevu.
Hata hivyo,
tafiti anuai zinaonesha kuwa kuna ugumu mkubwa wa kuelezea kwa ufasaha namna
nzuri zaidi ya kutekeleza upimaji
endelevu wa mwanafunzi (Havover Research, 2014) kutokana na sababu mbalimbali
zikiwemo za upimaji endelevu kuwa na tafsiri tofauti (kulingana na mazingira),
aina ya walimu, upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na mambo mengine.
Pamoja na
ugumu huu, taasisi ya NWEA inayojihusisha na utafiti wa namna bora za
kutekeleza upimaji wa wanafunzi, imebaini mambo makuu manne ya kuzingatia ilikuhakikisha upimaji endelevu unaleta tija kwenye ujifunzaji wa wanafunzi.
Makala haya yanalenga kujadili mambo hayo makuu
manne ambayo ni; ufafanuzi wa kina wa mambo makuu yanayopaswa kujifunzwa na
wanafunzi (clarifying learning), kuwajengea wanafunzi ari ya kujifunza
(activating learners), kutoa mrejesho wa maendeleo yao (providing feedback) na
kutafuta ushahidi wa ujifunzaji (eliciting evidence of learning).
Ufafanuzi wa Kina wa Mambo Mahususi
ya Kujifunza
Ni muhimu
sana kwa mwalimu kueleza kinagaubaga mambo mahususi wanayopaswa kujifunza
wanafunzi kabla ya kipindi au kabla ya kuanza kufundisha mada. Kwa mujibu wa
Hanover Research(2014), kulinganisha kwa ufasaha shughuli za ufundishaji na
malengo mahususi ya ujifunzaji yanasaidia kuwafanya wanafunzi wafahamu vizuri
umuhimu wa kile wanachojifunza na hivyo kuongeza ari ya ushiriki wao.
Mitaala
inayoandaliwa na kusimawiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni moja ya mifano hai ya kuigwa sana katika mfumo wetu wa elimu. Ikiwa unapenda
kufahamu vizuri zaidi dhana ya umuhimu wa ufafanuzi wa kina wa mambo
wanayopaswa kujifunza wanafunzi, basi rejea mitaala ya NACTE.
Pamoja na
ufafanuzi wa kina wa malengo ya ujifunzaji, walimu wanashauriwa pia kuandaa
vizuri vigezo vya upimaji ambavyo ni kiongozi cha mwanafunzi kufahamu alipotoka kitaaluma, alipo na anapotakiwa kwenda.
Katika mitaala
yake, NACTE imejitahidi sana kutoa ufafanuzi wa kile mwanafunzi anachopaswa
kukijifunza kupitia mfumo wa malengo ya ufundishaji yaliyogawanywa katika
sehemu kuu tatu ambazo ni Malengo Makuu (principle learning Outcome(s)), Malengo Wezeshi (Enabling Outcome(s)) na Malengo Wezeshi
mahususi(Sub-enabling Outcomes(s)).
Pia, uzuri
wa mitaala ya NACTE ni kuwa, malengo wezeshi mahususi yamegawanywa katika
shughuli mahususi anazopaswa kuzifanya mwanafunzi ili kuhakikisha anajifunza
mambo mahususi yaliyokusudiwa. Sambamba na hilo, kila malengo makuu yana vigezo
mahususi vya upimaji kwa ajili ya kusaidia kuonesha viwango vya mafanikio
yanayotarajiwa kwa mwanafunzi.
Hii ni
kusema kuwa, mitaala inayoandaliwa vizuri hutoa nafuu na kumrahisishia mwalimu
katika kutoa ufafanuzi wa mambo makuu wanayopaswa kujifunza wanafunzi kabla ya
ufundishaji. Ni rai yangu kwa wadau wa mitaala kujifunza mfumo wa kuigwa wa
mitaala ya NACTE ili kujihakikishia hitaji la kwanza la
kutekeleza kwa ufasaha upimaji endelevu wa wanafunzi.
Kuwajengea Wanafunzi Ari ya Kujifunza
Kama nilivyotangulia
kusema, upimaji endelevu ni matokeo ya juhudi za mwalimu na wanafunzi wake. Ni
vizuri walimu wakaondoa dhana kuwa, upimaji endelevu ni kutoa jaribio, testi au
kazi ya nyumbani tu. Haya ni mambo machache miongoni mwa mambo mengi na muhimu yanayojenga
upimaji endelevu wa mwanafunzi.
Upimaji endelevu
ni sehemu ya mchakato wa ujifunzaji wa mwanafunzi. Mwanfunzi anapaswa kujiona
kuwa anawajibika kwenye ujifunzaji wake na ni sehemu ya chanzo cha maarifa kwa
wanafunzi wenzake. Kufanikiwa kumshawishi mwanafunzi kushiriki kikamilifu kwenye ujfunzaji wake hufanya hata shughuli kama vile testi, majaribio, kazi za nyumbani, majadiliano n.k kuwa na maana kwake na kushiriki kwa lengo la kujifunza.
Zipo tafiti
nyingi zinazothitibisha kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi kunakotokana na
kuongezeka kwa ushiriki wao wakati wa ujifunzaji. Moja ya tafiti hizi ni ule
uliofanywa mwaka 2014 na Profesa Msaidizi, Daktari Gunuc Selim wa Chuo Kikuu
cha Yuzuncu Yil
cha nchini Uturuki. Katika utafiti wake uliolenga kutafuta uhusiano ulipo kati
ya kiwango cha ushiriki wa wanafunzi kwenye ujifunzaji na kiwango chao cha
ufaulu aligundua kuwa ushiriki wa wanafunzi kiakili, kitabia na kihisia kunabashiri
ongezeko la ufaulu kwa kiwango cha asilimia 10.
Utafiti
kama huu uliofanywa nchini Kenya na
watafiti Ndiewo, Aloka na Raburu ulenga kufahamu ikiwa mafanikio ya kitaaluma ya wanafunzi wa sekondari nchini humo yalikuwa na mahusiano na kiwango chao cha ushiriki kwenye ujifunzaji. Matokeo ya utafiti yalionesha uhusiano sawia wa
ushiriki wa wanafunzi na mafanikio yao kitaaluma.
Ushiriki wa wanafunzi kikamilifu kwenye ujifunzaji kunaongeza uwezekano wa kupata mafanikio kilelimu kutokana na mambo kadhaa. Wanafunzi hupata
nafasi ya kujitathmini-pale walipo, walipotoka na wanapohitaji kwenda-jambo
linalowapa hamasa ya kujirekebisha na kuchukua jukumu la kujisimamia kuelekea
malengo ya ujifunzaji wao.
Sambamba na
hili, ushiriki wa wanafunzi hutoa fursa ya wanafunzi kufanyiana tathmini,
kukosoana na kufundishana. Hii ni kama kusema, kila mwanafunzi anakuwa mwalimu
wa mwenzake.Ushiriki wa namna hii unawafanya wanafunzi kuwa wabunifu, kuwa na utayari wa kutatua changamoto wakijua wao ni vyanzo muhimu vya maarifa kwa wanafunzi wenzao na wasingalipenda kuwaangusha.
Itaendelea…..
Comments