Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.
Umbali kati ya shule na waishipo wanafunzi, hususani kwa shule za kutwa, umebainishwa na watafiti wa elimu kuwa unaathiri masomo ya mwanafunzi. Picha kutoka Fullshangwe Blog. Imetumiwa bila ruhusa.
Kama nilivyodokeza katika makala iliyotangulia, makala hii inajadili mambo kadhaa ya msingi ya kuzingatia ili kuboresha na kuongeza ufanisi wa shule, hususani za msingi na sekondari. Mambo haya ni matokeo ya tafiti mbalimbali za masuala ya uboreshaji na ufanisi wa shule. Ubora wa elimu Tanzania umeendelea kushuka siku hadi siku, na mikakati kadhaa ikiwamo ya matokeo makubwa sasa imeanzishwa katika kukabiliana na changamoto hii.. Harakati yoyote ya kuboresha ufanisi na ubora wa shule hauna budi kuzingatia mambo kadhaa yakiwemo haya takayoyajadili hivi punde kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kielimu.
Uongozi bora
Tafiti za masuala ya ufanisi wa shule zinaonesha kuwa, wakuu
wa shule wamekuwa kiini cha mafanikio ya shule.
Tafiti hizi zinaonesha kuwa, ubora wao hufikiwa pale wanapotimiza
majukumu yao ya kuhakikisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana
kwa wakati na vya kutosha, kueleza kwa uwazi dira na mikakati ya shule,
kuelezea kwa uwazi na usahihi kile wanafunzi wanachotegemea kukipata wakati wa
mafunzo yao, kuwa na mawasiliano rafiki,
ya mara kwa mara kati yake na walimu, wanafunzi, wafanyakazi wasio
walimu, wazazi na jamii inayoizunguka shule. Pia, mkuu wa shule hana budi
kutengeneza mazingira rafiki ya kufikiwa kwa urahisi na bila ya vikwanzo pale,
mwalimu, mwanafunzi, mzazi au mwanajamii anapolazimika kuwasiliana naye ana kwa
ana.
Mchango wa Wazazi na Jamii
Ogula na Asia(2013) katika kuchambua tafiti mbalimbali za
masuala ya ufanisi wa shule, wamebaini kuwa, wazazi na jamii inayozunguka shule
husika wana mchango mkubwa katika kuipatia shule mafanikio.
Katika uchambuzi wao, wameonesha kuwa wajibu wa wazazi na
jamii ni kuisaidia shule kifedha na kwa vifaa katika kuhakikisha shule
inatimiza majuku yake ipasavyo, kushiriki kikamilifu kwenye safu za uongozi wa
shule, kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya uongozi na wafanyakazi
wengine wa shule, kushiriki katika ufundishaji wa wanafunzi na shughuli
nyingine za shule. Ikumbukwe kuwa, wazazi na wanajamii wanaweza kushiriki
katika ufundishaji pale wanapokuwa likizo au baada ya kustaafu. Hili
linawezekana, siyo tu kwa walimu, bali hata kwa kada nyingine kama vile
madaktari wanaoweza kufundisha masuala mbalimbali ya afya ikiwemo na masomo ya
sayansi kama vile bayolojia, kemia na fizikia.
Mbali na mambo hayo, jamii pia ina wajibu wa kuhakikisha
inawaandaa vyema watoto wao ili waweze kupokea vyema yale wanayofundishwa
shuleni. Katika kufaninikisha hili, wazazi, walezi na jamii hawanabudi
kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe ya kutosha, malazi bora, mavazi bora
zikiwamo sare za shule, vifaa muhimu vya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi
wanakuwa na afya njema wakati wote.
Uwezo wa Mwanafunzi wa Kujifunza.
Kama nilivyotanguliakusema katika makala iliyopita, mwanafunzi mwenyewe ni
sehemu muhimu ya kboresha au kushusha ufanisi wa shule. Tafiti za uboreshaji na
ufanisi wa shule zimeweka bayana mambo kadhaa yamhusuyo mototo ambayo huweza
kuathiri ufanisi wa shule husika. Mambo hayo ni pamoja na utayari wa mwanafunzi
mwenyewe katika kujifunza maarifa na stadi mpya. Uongozi wa shule, walimu,
wazazi na jamii hawana budi kujua namna bora za kuwaandaa watoto wao
kisaikolojia ili wawe tayari kujifunza maarifa na stadi mpya, shuleni na
majumbani.
Mambo mengine yanayomhusu mwnafunzi ni pamoja na mtazamo
wake kuhusu shule, walimu na uongozi, hali ya uchumi wa nyumbani, maudhurio ya
mwanafunzi shuleni na darasani, kiwango cha matarajio ya mwanafunzi kuhusiana
na mustakabali wa elimu yake, umbali uliopo kati ya shule na aishipo
mwnafunzi(husuani kwa shule za kutwa), nidhamu ya mwanafunzi husika ikiwa ni
pamoja na historia yake ya matukio ya kinidhamu, shuleni na nyumbani.
Nidhamu kwa mwanafunzi ni moja ya nyenzo za muhimu sana
katika kuhakikisha mwanafunzi husika na shule husika inafikia ,alengo
yaliyokusudiwa. Kuna baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikidahili wanafunzi
walioshindikana kimaadili katika shule nyingine. Bahati mbaya sana kama uongozi wa shule na
walimu hawatakuwa na historia sahihi ya wanafunzi hawa, wanaweza kupoteza muda
mwingi kukabiliana na matatizo ya kinidhamu. Upotezaji wa vipindi kwa ajili ya
kukaa vikao vya nidhamu unaweza kuathiri ufanisi wa shule kwa kiasi kikubwa, na
hivyo kuzuia kufikiwa kwa malengo ya shule.
Sio lengo langu kusema kuwa wanafunzi wenye historia mbaya
ya nidhamu wasipokelewe mashuleni, la hasha. Lengo hapa ni kuukumbusha uongozi
pamoja na walimu kufuatilia vyema historia za wanafunzi, hususani kwa shule
zenye mazoea ya kuchukua wanafunzi wanaoendelea na masomo kutoka katika shule
nyingine. Utaratibu huu utawawezesha walimu na uongozi kutumia mbinu sahihi
katika kuwakuza vijana hawa kimasomo, kimaadili na kijamii.
Kufuatilia uwezo wa mwanafunzi mmoja mmoja husaidia pia kufahamu
wanafunzi wanaohitaji uangalizi maalum. Kwa mfano, wapo watoto wanaohitaji
matunzo maalum kama vile wenye usikivu hafifu, wasioongea n.k. Pia, kufahamu
historia ya maisha ya mwanfaunzi akiwa nyumbani na utamaduni wake huweza
kusaidia katika kuelewa namna bora ya kumkuza kitaaluma na kijamii.
Muda ambao Mwanafunzi anaoutumia Kujifunza awapo shuleni na
Nyumbani.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika za ufanisi na ubora wa
shule katika nchi za ulimwengu wa tatu na zinazondelea, imeonekana kuwa, ,kuna
uhusiano mkubwa kati ya mafanikio ya mwanafunzi kielimu pamoja na muda
anaoutumia katika kujifunza. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa, wanafunzi wanapotumia
siku nyingi za mwaka wakiwa shuleni na
wakijibidisha na kazi zilizoandaliwa na kuratibiwa vizuri na walimu hao,
hufanya vizuri zaidi katika masomo yao. Imefahamika pia kuwa, utoaji wa kazi
nyingi za nyumbani kunakomfanya mwanafunzi awapo nyumabani atumie muda wake
vizuri katika masomo, kuwemekuwa na matokeo chanya katika ufaulu wa wanafunzi.
Pia, muda mwingi wa ufundishaji madarasani umeonekana kuongeza kiwango cha
ufaulu wa wanafunzi.
Kwa bahati mbaya, katika shule zetu za msingi na sekondari,
kumekuwa na uvunjwaji wa vipindi mara kwa mara na hivyo kumega siku nyingi
ambazo mwanafunzi alipaswa kujifunza. Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakimega
muda wa wanafunzi wa kujifunza darasani na walimu kufundisha ni vikao
visivyokuwa na muda maalum na vinavyofanyika wakati wa masomo, shughuli
zisizokuwa na ulazima kwa wanafunzi kama vile kufanya kazi kwa walimu n.k
Mambo mengine ya kuzingatia katika kuleta ufanisi wa shule
ni pamoja na kuangalia uwezo wa walimu. Uwezo wa mwalimu hujumuisha mambo
kadhaa kama vile uzoefu wake, kiwango cha elimu, kuangalia kama mwalimu
ametimiza matakwa ya kuwa katika taaluma yake, utayari wa mwalimu katika
kufundisha, ujuzi wa kutahini na kutathmini wanafunzi, tabia ya uhamaji wa
mwalimu kutoka shule moja hadi nyingine,
uwiano wa mwalimu na wanafunzi katika darasa n.k
Pia, tafiti hizi zinaonesha kuwa ubora wa ufundishaji
unachangia kupata matokeo chanya ya wanafunzi na hivyo kuboresha ufanisi wa
shule. Ubora wa ufundishaji katika tafiti za kielimu zilizokwisha fanyika
zimezingatia mambo kama vile ubora wa mbinu na njia za ufundishaji, uwezo wa
mwalimu katika somo analofundisha, mtazamo wa mwalimu kuhusu wanafunzi na shule,
ikiwa ni pamoja na kuwa na utayari wa kufanya kazi kwa moyo na kuitumikia shule
kwa kuzingatia mikakati na dira ya shule, utoaji wa mazoezi na kazi za nyumbani
mara kwa mara na urudishaji wa haraka wa matokeo.
Uungwaji Mkono Kutoka Mamlaka za Elimu
Tafiti nyingi za kielimu zinaonesha kuwa, mamlaka za elimu
zina mchango mkubwa katika kuhakikisha
ubora na ufanisi wa shule unafikiwa. Mamlaka hizi ndizo zinazopaswa
kuhakikisha walimu wanapata maslahi yao ya kutosha na kwa wakati, wanapata mazingira rafiki ya
kufundishia na wanafunzi wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia na kuhakikisha
kuna zana bora na za kutosha za kufundishia na kujifunzia.
Kwa kawaida wakaguzi
wa shule wamekuwa ndio kiungo kikuu kati ya shule na mamlaka za juu za elimu.
Wakaguzi wa shule wana majukumu ya kufuatilia mchakato wa ufundishaji na
ufundishaji mashuleni na kuwashauri walimu na wakuu wa shule katika mambo
kadhaa yanayolenga kuongeza ufanisi na ubora wa shule. wanajukumu pia la kuleta
mrejesho wa changamoto wanazoziwasilisha katika mamlaka za juu za elimu. Kwa
Tanzania, wakaguzi wa shule hawajapewa msisitizo wa kutosha. Upitiaji wa shule umekuwa wa mara chache
sana. Pia, mrejesho wa mambo kadha wa kadha umekuwa haufanyiki na hivyo, kitengo
hiki muhimu kuonekana kutotimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande mwingine, walimu wengi wamekuwa wakiwaogopa
wakaguzi wa shule kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ya kujengeka kwa dhana
miongoni mwa walimu wengi kuwa, wakaguzi huja kuhukumu badala ya kushauri na
kuelekeza yapi yafanyike. Bila shaka, kukosekana pia kw maadili ya kazi
miongoni mwa walimu mara kw mara, kunaweza kuchangia wakaguzi hawa, pindi
wafikapo mashuleni kuchukua hatua kali zaidi kutokana na ukiukwaji wa taratibu
za kazini kujirudia siku hadi siku.
Mambo haya niliyoyajadili ni ya muhimu kuzingatiwa katika
kuhakikisha ubora na ufanisi unaotakiwa katika shule yetu yanafikiwa. Ikumbukwe
pia kuwa, haya ni baadhi, yapo mengi kwa kuzingatia pia kuwa, tafiti za kielimu
zinaendelea kufanyika na mambo mengine mengi yanaweza kuibuliwa mbali na hay
machache niliyoyajadili. Kama nilivyotangulia kusema, mambo haya yataweza
kuleta ufanisi mkubwa kama tu kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake. Hivyo
basi, makala inayofuata, itaangalia kwa ufupi, suala hili la uwajibikaji katika
kuhakikisha ubora na ufanisi unaotakiwa wa shule unafikiwa.
Shukrani kwa Ogula na Rubeba (2013) walioandaa makala ya Mapitio ya Tafiti za Kielimu za Uboreshaji na Ubora wa Shule iliyochapishwa katika Jarida
la Tafiti za Kielimu, toleo la kwanza, la Chuo Kikuu cha Kikatoliki Cha Mwenge.
Comments
Maoni na mtazamo wako katika kuboresha kiwango cha ufaulu katika elimu nchini ni mzuri na uliotazama umuhimu wa kila mdau katika kuufikia ufanisi. hongera sana