Namna ya Ujifunzaji ni Moja ya Changamoto kuu ya Elimu Yetu.


Image result for shule ya mwalimu aliyechora window ubaoni yazawadiwa komputa
Mwalimu Hottish wa Shule moja huko Ghana Akichora Kitumizi cha Microsoft Word kama namna ya kuwasaidia wanafunzi wake kujifunza. Picha kwa hisani ya www.MillardAyo.com
Mjadala wa kujadili mustakabali wa Elimu yetu umeitishwa. Bila shaka ni kutokana na mwenendo usioridhisha wa elimu yetu. 

Elimu yetu inaonekana kutokukidhi mahitaji ya watanzania na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, kabla ya kufika mbali, wadau wa elimu-walimu, wanafunzi, wazazi, raia, viongozi, n.k wanafahamu bayana kuhusu matarajio ya elimu inayotolewa?

Kwa mini tunasema  elimu yetu imezorota? Wanafunzi kufeli sana? Mazingira ya kufundishia na kujifunzia kuwa magumu (sana)? Tunahitaji elimu itusaidie kufika wapi kama watanzania na kama Taifa?Pengine maswali haya yabaki kama sehemu ya kuchochea mjadala wa wa kitaifa kuhusu elimu nchini kwetu. 

Makala haya yanalenga kushirikisha uzoefu wangu wa darasani na kuonesha angalao moja ya maeneo ambayo, yakifanyiwa kazi vizuri, yanaweza kuifanya elimu yetu ikapigiwa mfano. Eneo hili ni namna ya kujifunza.Ndio, namna ambavyo wanafunzi wanajifunza. Achilia mbali maudhui wanayojifunza.  Katika blogu hii, nimewahi kujadili kuhusu dhana hii mara kadhaa. Unaweza kufuatilia Makala zinazohusu dhana ya namna ya ujifunzaji kwa kusoma kamala hii hapa. 

Kisa cha Darasani

Kwanza, ni vyema ikatambulika kuwa mimi ni "Champion" wa ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi. Kwa kimombo, ufundishaji huu unaitwa Learner Centred Pedagogy. Katika mfumo huu, mwalimu ana wajibu wa kumsaidia mwanafunzi kujifunza kwa maana ya kujenga uelewa wake kuhusiana na mada husika.

Hajilalishi ni kwa kiasi ninaweza kumshirikisha mwanafunzi. Lakini, kwa kuwa ninafahamu umuhimu wa kufanya hivi, huwa ninajitahidi sana kuhakikisha mwanafunzi ndiye mchapa kazi mkuu huko darasani. Ninaamini darasa ndio karakana yake ya kujidai. Hivyo, hadi mwisho wa kipindi, yeye ndiye anapaswa kufuta jasho la mihangaiko ya kujitafutia ‘rizki’ yake ya kila siku.

Kwa hiyo, ninapojiandaa na ufundishaji, ninajiandaa huku ninawaza wanafunzi watafanya nini ili wafikie malengo ya ujifunzaji yanayokusudiwa kwao na ni kwa namna gani watafanya shughuli husika. 

Katika tafakari hii, nikapata wazo la kufundisha kwa Senario(Scenario). Ufundishaji wa namna hii, katika hatua za mwanzo kabisa, mwanafunzi anakutana na changamoto anayopaswa kuitatua. Inategemewa katika ufundishaji wa namna hii, wanafunzi wahitaji kwanza maarifa ama ujuzi fulani ili watatue changamoto hii. 

Hatua hii, kutegemea na aina ya wanafunzi, inawapa fursa ya kutengeneza mabunio yao (hypotheses), kujiuliza maswali ambayo watapaswa kujitafutia majibu kwa kutafiti maandiko mbalimbali, mijadala n.k. Kama umepitia mitaala ya NACTE, bila shaka, Scenario unaweza kufananisha na "complex integrated Challenge". Wanafunzi wanapaswa kutatua changamoto inayoakisi mazingira halisi ya kazi.

Nilikuwa ninafundisha Probability, mada ndogo ya Permutations and Combinations. Nilihitaji wanafunzi waweze kueleza maana ya permutation na combination. Pia, waweze kutofautisha dhana hizi mbili. Na mwisho waweze kufanya maswali yanayohusu combination na permutation. 

Scenario zilikuwa kadhaa. Mojawapo ilihusu kofuli zinazotumia nywila na haswa zile za namba. Niliwauliza ikiwa walihawi kuzitumia ama wanazitumia. Wanafunzi wengi walionekana kuzifahamu. Haswa mfumo unaotumika kwenye baadhi ya mabegi ya kusafiria.
Niliwaomba wapendekeze nywila ambayo wangependa kuitumia kama mfano. 


Mwanafunzi mmoja alipendekeza 0,9,0,9. Kisha niliwauliza, wanapohitaji kufungua begi, wanaweza kuweka namba hizi kwa mpangilio wowote au ni lazima waweke kama namna zolivyopangwa? Niliwauliza pia  wanafikiri utumiaji wa nywila wa namna hiyo (kulingana na majibu yao) ni permutation au combination? Swali kuu ni mfumo wa uwekaji nywila unaelezea vyema permutation au combination kwa namna gani?

Matarajio yangu ni kuwa, wanafunzi watakosa majibu katika hatua ya awali kabisa. Kwa maana kuwa nimewajengea changamoto wanayopaswa kuitatua. Matarajio ya ujifunzaji ni kuwa wanafunzi wafahamu kuwa hawana maarifa ya kutosha kupata majibu sahihi (tatizo). Wakishagundua hili, waende hatua nyingine ya kutafuta suluhisho la tatizo. 

Unaweza kubashiri ni mambo gani yaliendelea darasani? 

Ulitokea mjadala wa haja. Kwanza niseme, nilifurahishwa mno na hali ile. Nitaeleza baadae ni kwa nini.Baadhi ya wanafunzi waliohoji kuwa maswali haya ninawataka wajibu ilihali "sijawafundisha" dhana za permutation na combination. Kwamba, wao watapa wapi majibu? Kama vile niliwaonea. Baadhi ya wanafunzi walihitaji ufafanuzi kutoka kwa mwalimu. Hawakutaka kuendelea kujihoji wangaliweza kufanya nini ili kujifunza dhana hizi.  

Ilibidi niruhusu mjadala wa namna wanafunzi wanavyoweza kupata majibu ya changamoto inayowakabili. Kwanza, niliwapongeza kwa kuhoji. Angalao ninawezaje kuwauliza maswali na kuhitaji majibu ya mambo ambayo hawajajifunza. Ni namna ya uwajibikaji. 

Niliongoza mjadala kwa kuwaonesha namna walivyo na wajibu wa kutafakari ni kwa namna gani wanaweza kutatua changamoto yao. Wanafunzi walilalamika kutokuwepo kwa vitabu. Bahati nzuri, wakati wengine wanalalamika kuhusu ukosefu wa zana za kujifunzia, mwanafunzi mmoja alileta mrejesho kuwa ameshapata angalao maana ya dhana za combination na permutation. 
Labda msomaji nikufafanulie kidogo kuhusu hali ya darasa hili. Kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaomiliki simu janja. Mara kadhaa nimekuwa nikiwaongoza kuzitumia kwenye ujifunzaji. Hawa na wanafunzi wanaojiandaa kuwa walimu. Tulijadili namna wanavyoweza kutumia simu zao, umuhimu wa kuja na vitabu darasani na vitabu vya masomo husika. Kimsingi, niliwakumbusha umuhimu wa kuona wajibu wao kwenye ujifunzaji wao wenyewe.

Angalao, mwanafunzi huyu, alibadili hali ya mambo. Alikuwa mfano mzuri wa kuigwa. Aliingia mtandaoni kwa kutumia simu yake. Alitafuta majibu. Mwanfunzi huyu anatoa funzo kwa wanafunzi wenzake. Ni muhimu kutafuta namna ya kutatua changamoto kuliko kukwamishwa na vikwanzo ambavyo, katika mazingira yao havipo. Kwa kutumia simu janja zao, wanaweza kupakua vitabu lukuki na wakavitumia.

Ndugu msomaji, dhana kubwa hapa ni uwezo wa mwanafunzi wa kujiuliza maswali  na kisha kufikiri namna ya kutafuta majibu ya maswali yake. Tabia hii inakaribisha na kujenga uwezo wa mwanafunzi kufikiri, kutatua changamoto, kushirikiana na kadhalika.

Elimu yetu inapungukiwa na nini ukiachilia mbali maudhui yanayofundishwa?

Ukirejea kisa hiki, moja ya vitu ambavyo elimu yetu iinapungukiwa ni namna wanafunzi wanavyojifunza. Elimu yetu haiwezi kutukomboa ikiwa wanafunzi wanakaa tu darasani bila kuwa sehemu ya kutatua changamoto. Kazi za ujifunzaji zinazomshirikisha mwanfunzi zinampa uwezo wa kukuza uwezo wa kufikiri, kutatua changamoto, kuwasiliana na kushirikiana. Hizi ndizo tabia za mtu anayeweza kujiajiri na kuajirika.

Kwa hiyo, namna wanafunzi wanavyojifunza ni eneo linalohitaji makazo wa hali ya juu kabisa. Kuna wakati maudhui yanaweza kuwa hayatoshelezi lakini namna wanafunzi wanavyojifunza ikwa na maana kubwa sana kwenye maisha ya mwanafunzi husika. Watoto wanaokulia jijini Dar es Salaam kwa mfano, wanaonekana kuwa wajanja sana katika maisha. Hakuna shule rasmi wanayokwenda au mtaala rasmi unaowajenga hivyo. Ni namna ya maisha wanayokutana nayo. Yanawajengea hali ya kuwa na ujanja anaoukosa mtoto aliyekulia shamba.

Je, unakumbuka kisa cha kweli cha mwalimu Owura Kwadwo Hottish wa nchini Ghana aliyekuwa anafundisha somo la Kompyuta? 


Alichora kitumizi cha Microsoft Word ubaoni ili kuwafundisha wanafunzi namna kitumizi hiki kinavyofanya kazi. Kwa sisi walimu wa Tanzania, hatungeishia kuacha kufundisha kwa sababu hakuna kompyuta? Je changamoto za ufundishaji na ujifunzaji siyo fursa kwa walimu na wanafunzi?

Mwalimu Hottish alipata wapi nguvu ya kuchora kitumizi cha Microsoft Word ubaoni? Hii ni nguvu ya kuamua na kutenda. Mambo ambayo kwa mfumo  wetu wa elimu, wanafunzi wetu hawapati fursa ya kuyafanya pamoja na kuwa mazingira ya kazi yanaweza kuwa magumu kuliko hata hayo ya Hottish. 
Ujumbe wa Twitter wa @MicrosoftAfrica: BREAKING NEWS We're excited to see Owura Kwadwo Hottish in Singapore attending the Microsoft Global Education Exchange Summit!
Picha kwa hisani ya BBC

Mwanafunzi anayekaa tu darasani mwanzo wa kipindi ha di mwisho, amekunja mikono, amekunja nne, anamsikiliza mwalimu anayeongea hadi koo linakauka na kufuta majasho, mwanafunzi huyu anasema yupo darasani anasoma. Tunajidanganya. Mwalimu anaonesha maaarifa ama ujuzi alioupata kwa kusoma. Mwanfunzi anabaki kuwa shuhuda.

Ninakuacha na tafakari ya Mwalimu Hottish. Jaribio lake la angalao kufanya linalowezekana ili wanafunzi wajifunze kompyuta, kulipelekea shule yake kuzawadiwa kompyuta na yeye kupata fursa ya kuhudhuria mkutano wa Waelimishaji wa Microsoft huko Singapore.

Tusikwamishwe na mazingira. Jambo la msingi ni kufanya jambo ambalo ni sahihi, hata kama ni kwa upungufu wa namna gani. Huo ndio mwanzo. Hakuna sababu ya kusema muda hautoshi kwenye ufundishji na ujifunzaji unamzingatia mwanafunzi wakati hata kutumia muda mchache ulipo hatujaweza. Tusiseme hakuna vitabu wakati simu janja moja ya mwalimu au mwanafunzi inaweza kubadili hali ya mambo.

Ni bora hata kama kuna kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja akasoma kwa sauti kisha wanafunzi wakajadili kile walichosikia. Namna wanafunzi wanavyojifunza ni changamoto kubwa sana inayokwamisha elimu yetu. Wanafunzi hawapati fursa ya kuonesha ubunifu, kutatua changamoto, kushirikiana, kuwasiliana kwa sababu, katika kujifunza, wao ni wasilikizaji wakuu. Mwalimu anatumia muda mwingi kuonesha kile alichojifunza yeye badala ya kuwasaidia wanafunzi kujifunza.

Hadi, tutakapoweza kubadili hali hii, ndipo tutakapoanza safari mpya ya kusubiri amtunda chanya ya elimu yetu. Kubadili maudhui yanayojifunzwa bila ya kubadili namna ya kujifunza maudhui hayo, elimu yetu bado itakuwa kichwa cha mwendawazimu.

Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?