Elimu inayozingatia uwezo(Competence Based Education): Maana na Misingi yake Mikuu
Matumizi ya TEHAMA ni moja ya njenzo muhimu ya kufanikisha Elimu inayozingatia uwezo mashuleni. Kupitia TEHAMA, wanafunzi wanaweza kujisomea popote na kwa wakati wao huku wakishirikiana na wenzao popote pale walipo. Picha kutoka HakiElimu Kama nilivyotangulia kuandika katika makala iliyotangualia, ni takribani miaka kumi na ushei tangu elimu inayozingatia uwezo ilipoanza kutumika rasmi nchini Tanzania. Katika kipindi hiki, hakujakuwa na mafanikio ya kuridhisha sana katika ngazi zote za elimu. Wanafunzi wengi wanamaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wala kuandika, wanafunzi wengi wanamaliza shule za sekondari wakiwa wamepata madara yasiyoridhisha. Vile vile, vijana wa vyuo vikuu wanamaliza vyuo bila kuwa na stadi stahiki za kukabiliana na changamoto za kukosekana kwa ajira n.k. Elimu inayozingatia uwezo ilitazamiwa kuwa ingeweza kukabiliana vyema na changamoto hizi za kufeli kwa wanafunzi pamoja na suala la ajira hususani kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu. ...