Elimu inayozingatia uwezo(Competence Based Education): Maana na Misingi yake Mikuu
Matumizi ya TEHAMA ni moja ya njenzo muhimu ya kufanikisha Elimu inayozingatia uwezo mashuleni. Kupitia TEHAMA, wanafunzi wanaweza kujisomea popote na kwa wakati wao huku wakishirikiana na wenzao popote pale walipo. Picha kutoka HakiElimu
Kama nilivyotangulia kuandika katika makala
iliyotangualia, ni takribani miaka kumi na ushei tangu elimu inayozingatia
uwezo ilipoanza kutumika rasmi nchini Tanzania. Katika kipindi hiki, hakujakuwa
na mafanikio ya kuridhisha sana katika ngazi zote za elimu.
Wanafunzi wengi wanamaliza elimu ya msingi bila kujua
kusoma wala kuandika, wanafunzi wengi wanamaliza shule za sekondari wakiwa
wamepata madara yasiyoridhisha. Vile vile, vijana wa vyuo vikuu wanamaliza vyuo
bila kuwa na stadi stahiki za kukabiliana na changamoto za kukosekana kwa ajira
n.k.
Elimu
inayozingatia uwezo ilitazamiwa kuwa ingeweza kukabiliana vyema na changamoto
hizi za kufeli kwa wanafunzi pamoja na suala la ajira hususani kwa vijana wanaomaliza
vyuo vikuu. Lakini, swali la kujiuliza ni kuwa, mfumo huu wa elimu kwa takribani
miaka kumi ya uwepo wake, umetendewa haki au tuishie kusema kuwa siyo muafaka
kwa mazingira yetu? Walimu wanaufahamu wa kutosha wa elimu hii? Je, ni kweli
fikra za walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji zinaongozwa na misingi
ya mfumo huu?
Tafiti mbalimbali zilizoangalia matumizi sahihi ya
elimu inayozingatia uwezo zinaonesha kuwa mfumo huu bado haujatumika ipasavyo
mashuleni na hata vyuoni. Mambo kadhaa yameoneshwa kuwa yanahitajika kufanyiwa
kazi. Suala la kwanza ni elimu kuhusu mfumo huu wa ufundishaji na ujifunzaji.
Suala la pili ni uboreshaji wa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Lengo la
Makala haya ni kujaribu kutatua changamoto ya kwanza, hii ya ufahamu kuhusu
elimu inayozingatia uwezo. Nitajadili kuhusu maana pana ya elimu hii na misingi
yake mikuu mitatu.
Elimu inayozingatia Uwezo (Competency Based Education)
ni nini?
Elimu Inayozingatia Uwezo ni mfumo wa elimu
usiozingatia muda ambao mwanafunzi anapaswa kuutumia kujifunza kama kigezo cha
kuwa amehitimu masomo bali hujikita kwenye maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma
kwa kuangalia kama mwanafunzi husika amefikia malengo ya ujifunzaji
yaliyokusudiwa au bado hajayafikia.
Hii ina maana kwamba, muda siyo kigezo cha kumfanya
mwanafunzi ahame ngazi moja ya elimu kwenda nyingine au kuhama mada moja kwenda
nyingine. Kigezo kikubwa ni kama mwanafunzi amefikia lengo la kujifunza
lililokusudiwa. Kama bado, ataendelea kujifunza hadi atakapofanikiwa.
Kwa mfano, wanafunzi wanaojifunza kusoma na kuandika
darasa la kwanza, hawataondoka darasa hilo hadi watakapoweza kusoma na
kuandika, hata wakijifunza kwa zaidi ya mwaka mmoja. Wale wanaoweza kusoma na
kuandika, wataendelea na ngazi nyingine, hata kama mwaka haujaisha. Huu ndio
mfumo wa elimu inayozingatia uwezo kuliko umri au muda alioutumia mwanafunzi
kujifunza.
Bahati mbaya, walimu wengi mbali na kuwa dhana hii
bado ni ngeni kwao, lakini pia, ni dhahiri kuwa, kwa mfumo maarufu wa kusoma
kwa kuzingatia muda, utekelezaji wa mfumo huu bado una changamoto kubwa ya
kuweza kutekelezwa ipasavyo hapa Tanzania.
Mfumo huu wa elimu una misingi mikuu mitatu. Msingi wa
kwanza ni kuwa, mwanafunzi ndiye kiini cha ujifunzaji (Learner-Centric)
Katika msingi huu, ujifunzaji unamlenga mwanafunzi
mmoja mmoja (learner-centric). Mwanafunzi anapewa fursa ya kujifunza kwa wakati
wake, popote alipo na wakati huo akishirikiana na wenzake kwenye kufikia
malengo yake ya ujifunzaji. Mwanafunzi mmoja akifikia malengo yake ya
ujifunzaji, haimaanishi kuwa ni lazima kwa wakati huo, wanafunzi wengine
wanapaswa pia wawe wamefikia malengo ya ujifunzaji yaliyokusudiwa. Kila mwanafunzi
hujifunza kwa wakati wake kulingana na uwezo wake.
Msingi wa pili wa elimu inayozingatia Uwezo ni
ujifunzaji unaozingatia matokeo (Outcome Based).
Hii ni aina ya ujifunzaji ambayo hujikita zaidi kwenye
kuhakikisha mwanafunzi amefanikiwa kupata kile kilichokusudiwa kwenye
kujifunza. Siyo kuwa mwanafunzi ameelewa kwa kiasi gani, bali ameelewa au
hajaelewa, amefikia lengo au hajafikia lengo. Mwanafunzi hataruhusiwa kuendelea
na ngazi nyingine hadi pale kutakapokuwa na ushahidi usio wa mashaka kuwa,
alichopaswa kujifunza amekielewa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Kwa hiyo, katika mfumo huu, jambo la kwanza kabisa
linaloshauriwa ni kuhakikisha malengo mahsusi ya ujifunzaji yanaainishwa kwa
ufahasaha na kwa umakini. Pia, kuhakikisha kuwa kuna vigezo madhubuti vya
kuonesha kama mwanafunzi amefikia malengo au bado hajayafikia. Hii ni pamoja na
kuwa na njia muafaka za upimaji na utoaji wa tathmini ya ufikiwaji wa malengo
yaliyokusudiwa kwa wanafunzi.
Msingi wa tatu wa elimu inayozingatia uwezo ni
ujifunzaji unaozingatia mahitaji maalum ya mwanafunzi (Customized Learning).
Misingi huu una maana kuwa, kila mwanafunzi ana
mahitaji yake ya msingi ili kujifunza kwa tija. Wanafunzi wanatofautiana
mitazamo, uwezo wa kiakili, uwezo wa wazazi kifedha na hata tamaduni. Kwa hiyo,
mazingira ya ujifunzaji ya mwanafunzi mmoja mmoja ni lazima yaboreshwe na
kubadilishwa ili yaendane na mahitaji ya mwanafunzi husika (customized learning).
Nyezo za kujifunzia, mbinu na mazingira yanapaswa kuendana na matakwa ya
mwanafunzi mwenyewe. Hata kile anachopaswa kukisoma, kinapaswa kiendane na
matarajio, malengo na machaguo ya mwanafunzi mwenyewe.
Ukweli ni kuwa, misingi hii ya elimu inayozingatia
uwezo bado ni migumu sana kuitekeleza katika mazingira ya Tanzania. Angalao
msingi mmoja tu wa mwanafunzi kuwa kiini cha ujifunzaji ndio unaotekelezwa.
Hata hivyo, ni kwa kiasi kidogo sana.
Ili kufikia vyema malengo ya kumfanya mwanafunzi kuwa
kiini cha ujifunzaji wake, moja ya nyenzo muhimu sana ni matumizi ya TEHAMA
kwenye ufundishaji na ujifunzaji. Tanzania bado tupo nyuma sana. Vitabu
havitoshelezi, shule nyingi hazina miundombinu rafiki kama ya umeme na
kadhalika. Hali hii bado inapelekea wanafunzi kutumia fursa chache
zinazopatikana mahali Fulani tu kuhakikisha wanajifunza, muda wa kuhitimu
ukifika, wote watahitimu, walioshindwa kufika malengo yao na wale waliofikia
malengo yao ya kujifunza. Na hapa, dahana ya usawa katika kujifunza inakuwa imepotea.
Hata hivyo, hadi sasa, kuna juhudi kubwa nchini
Tanzania zimeshafanyika na zinazoendelea kufanyika kuhakikisha wanafunzi
wanafikiwa walipo katika kupata elimu kupitia TEHAMA. Baadhi ya makampuni
binafsi na taasisi za serikali kama vile Ubongo Kids, Edmodo (Chuo Kiuu cha
Dodoma), elimu popote
(Uhuru One) na wengine wengi wameshafanya kazi nzuri ya kuhakikisha elimu
inapatika popote alipo anayependa kujifunza.
Comments