Elimu Inayozingatia Uwezo: Bado Inasuasua, Wapi tunakosea?
Picha kwa hisani ya gettingsmart
Elimu inayozingatia uwezo imeshika kasi zaidi kipindi
cha hivi karibuni, hususani kwa mataifa ya Ulaya. Nchi kama Marekani imewekeza
kiasi kikubwa cha fedha kuhakikisha elimu hii inatumiwa mashuleni na vyuoni ili
kuleta ufanisi unaopaswa. Kwa mfano, blogu ya BlackBoard
kwa kushirikiana na Baraza
la Elimu la Marekani, tayari wameungana
kufanya Tafiti
za Elimu Inayozingatia Uwezo.
Utafiti
wa hivi karibu wa BlackBoard na Baraza la Elimu la Marekani umejaribu kuangalia
ni kwa kiasi gani Elimu Inayozingatia Uwezo inavyoweza kutekelezwa na pia
mafuaa yake kijamii na kisera na namna ambavyo mfumo wa krediti na uwezo unavyotafsiriwa
na wadau mbalimbali wa elimu.
Kutokana na ukweli kwamba, kiwango cha elimu nchini
Tanzania kwa kipindi kirefu kimekuwa kikidorora kadiri siku zilivyokuwa
zinaenda, moja ya muarobaini ulionekana ni kuazima mfumo wa Elimu unaozingatia
Uwezo. Hivyo basi, mwaka 2004, Tanzania
kupitia Taasisi ya Elimu iliamua kubadili mitaala ya shule za msingi hadi vyuo
vya ualimu ili iendane na matakwa ya aina hii ya elimu.
Mtaala uliokuwepo ulionekana umeshindwa kukidhi
mahitaji ya sera na mikakati mbali mbali ya kielimu na ya kimaendeleo. Pia,
tafiti mbalimbali zilzofanywa na wadau wa elimu ikiwa ni pamoja na Taasisi ya
Elimu Tanzania zilionesha umuhimu wa kufanyika kwa mabadiliko ya mitaala ya
shule za msingi, sekondari na vyuo vya Ualimu.
Kwa shule za msingi, mitaala inayozingatia ujifunzaji
wa kuzingatia uwezo ilianza kutumiaka rasmi mwaka 2006, kwa shule za sekondari na
vyuo vya ualimu, mtaala mpya ulianza kutumika rasmi mwaka 2005. Hakuna uhakika
kama mabadiliko haya yalihusisha pia vyuo vikuu ambavyo huandaa walimu wa
kusimamia utekelezaji wa mitaala mipya mashuleni inayohamashisha ufundishaji na
ujifunzaji unaozingatia uwezo.
Hata hivyo, mara baada ya kufanyika mabadili haya ya
mitaala, mafanikio katika elimu yameendelea kulegalega kwa kiasi kikubwa. Ni
takribani miaka kumi ya utekelezaji wa mitaala inayozingatia Ujifunzaji
unaozingatia uwezo. Tumezidi kushuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za
msingi wanaomaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma, kuandika kuhesabu.
Utafiti
wa Twaweza wa mwaka 2012 unaonesha kuwa
nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 55 ya wanafunzi wa darasa la tatu hawakuweza
kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili huku wanafunzi 8 kati ya 10 wa
darasa la tatu wakishindwa kusoma hadithi ya kiingereza ya darasa la pili. Pia, utafiti huo unaonesha kuwa, wanafunzi 7
kati ya 10 wa darasa la tatu hawakuweza kufanya hesabu ya kuzidisha ya darasa
la pili.
Elimu ya sekondari nchini Tanzania nayo imekuwa
ikisuasua kila kukicha. Matokeo ya mitihani Taifa ya kidato cha nne ya mwaka
2012 ndiyo yaliyokuwa matokeo mabaya katika historia ya mitihani ya Taifa
inayosimamiwa na baraza la mitihani la Tanzania ambapo zaidi ya asilimia 65 ya watahiniwa walifeli
mtihani huo.
Kufuatia kusuasua huku wa elimu, watafiti na
wadau mbali mbali wa elimu wamekuwa wakitafiti mfumo huu wa
elimu elimu ili kubaini mafanikio, changamoto na kisha kutoa mapendekezo ya
nini cha kufanya.
Tafiti nyingi zilizofanyika nchini Tanzania zinaonesha
kuwa walimu hawana uelewa wa kutosha kuhusu ufundishaji na ujifunzaji
unaozingatia uwezo. Kupitia tafiti hizi, imefahamika kuwa, walimu wengi wa
shule za msingi na sekondari hawafahamu nini wanapaswa kutekeleza ili
kuhakikisha wanafundisha kwa mujibu wa mitaala ya sasa. Hali kadhalika, tafiti
zinaonesha kuwa waalimu wanafunzi wanaotarajiwa kwenda kufundisha mashuleni,
hawana uelewa wa kutosha wa kuweza kufundisha kwa kuzingatia matakwa ya
ufundishaji unaozingatia uwezo. Pia,
hali isiyoridhisha ya mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji inaonekana kuwa ni
moja ya mambo yanayopelekea elimu inayozingatia uwezo wa mwanafunzi kuonekana
kushindwa.
Wakati tafiti nyingi zinazohusu ufundishaji na
ujifunzaji unaozingatia uwezo zikiwa zimeelekezwa zaidi kwa walimu, tuna mswali
kadhaa ya kujiuliza.
Kwanza, wahadhiri wa vyuo vikuu wanaufahamu vyema
mfumo huu wa ufundishaji na ujifunzaji? Wanapofundisha walimu wanafunzi, fikra
zao, ufundishaji wao na maono yao yanasimia kwenye mfumo huu? Vyuo Vikuu nchini
Tanzania vinautumia mfumo huu kuwafundisha wanafunzi? Je, vyuo vikuu vinafahamu
kwa upana wake misingi ya Elimu Inayozingatia uwezo na inaisimamia ipasavyo
kwenye kutoa elimu? Pengine, maswali haya yanapaswa kujibiwa kupitia tafiti.
Hata hivyo, kuna ukweli kuwa, vyuo vikuu vinatumia zaidi njia ya
mihadhara kwenye ufundishaji. Labda wingi wa wanafunzi katika darasa moja
inaweza kuwa ni moja ya sababu. Swali la kujiuliza ni kama, ufundishaji wa
kuzingatia uwezo unaathiriwa na wingi wa wanafunzi darasani. Kujibu swali hili,
ni vizuri kwanza tukaifahamu Elimu inayozingatia ujuzi pamoja na misingi
yake. Tukutane katika makala ijayo.
Comments