Utaratibu Huu wa Kuoa/Olewa ni Mzuri, Unahitaji Kuboreshwa Kidogo.
Picha kwa hisani ya Gospel Kitaa. Hakuna asiyejua shughuli ya kuoa/olewa ilivyo na pilika pilika nyingi na za kuchosha. Siyo tu hupoteza muda na fedha, mara nyingine huishia kwa watu kugombana, kuwekeana chuki na vinyongo visivyoisha. Asilimia kubwa ya fedha za harusi hutokana na michango ya watu mbalimbali kuanzia ndugu, jamaa na marafiki. Harusi ni sherehe ifanywayo kwa ajili ya kufurahia tukio muhimu la kufunga ndoa. Sherehe hii huja mara baada ya wapendanao kufunga ndoa kanisani, msikitini, serikalini ama kwa utamaduni. Hadi siku ya ndoa, sherehe ndogo ndogo za awali kama za kutambulishana, yaani ndugu wa pande mbili kufahamiana, kuvishana pete za uchumba, utoaji wa mahari, kapu la mama na send off hufanyika. Sherehe ya awali kabisa inayowashirikisha watu nje ya familia ni kapu la mama. Sherehe hii ni sehemu ya maandalizi ya sherehe ya kumuaga msichana (mara nyingi hufanywa upande wa msichana). Hapa mama wa msichana ndiye mhanga...