Tunawezaje Kuongeza Ufanisi na Ubora wa shule? Watafiti wa Masuala ya Ubora na Ufanisi wa Shule Wanatujuza.
Wanafunzi wakiwa wamekaa chini darasani huku somo likiendelea katika moja ya shule za msingi mkoani singida.
Kwa kipindi kirefu sasa, shule za msingi na za sekondari za Tanzania zimekuwa na matokeo yasiyoridhisha. Kuna idadi kubwa ya watoto wanaomaliza elimu ya msingi pasi kujua kusoma na kuandika. Hali kadhalika, wapo vijana wengi wa sekondari wanaomaliza na kushindwa kupata alama stahiki za kuwawezesha kuendelea na elimu ya juu. Kufuatia hali hii, yapo mengi yaliyozungumzwa na mikakati kadhaa kufanyika. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuandaa walimu wengi wa elimu ya awali kwa shule za msingi. Katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa walimu hasa wa sayansi kwa shule za sekondari, mikakati kama ya kutumia teknologia katika ufundishaji na ujifunzaji imeanzishwa.
Kuhusu ubora
wa shule, kuna mambo mengi yamefanyika. Kwanza, kuongeza idadi ya shule za
serikali, alimaarufu, shule za kata. Kwa bahati mbaya, shule hizi siku hadi
siku zimeendelea kukosa ubora na ufanisi. Mazingira yasiyoridhisha ya
kujifunzia na kufundishia imekuwa ni moja ya changamoto kubwa. Changamoto nyingine zimekuwa ni pamoja
na kukosekana kwa maabara na maktaba zenye ubora unaotakiwa. Uchakavu wa
madarasa na ofisi za walimu imekuwa pia ni sehemu ya changamoto katika shule
zetu za msingi na sekondari.
Swali la
kujiuliza hapa ni kuwa, katika kukabiliana na changamoto hizi, tunasikiliza na
kufuata ushauri wa wataalamu wa tafiti za ubora na ufanisi wa shule au
tunafanya lile linalowezekana au kwa kuwa tu wenzetu walipitia huko na wakafanikiwa?
Ubora na
ufanisi wa shule ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanana lakini yana
utofauti fulani. Kimsingi, mambo haya yanategemeana na yanakwenda pamoja. Mara nyingi, ni vigumu kuyatofautisha. Ufanisi wa shule maana yake ni nini? Ufanisi wa shule ni utendaji
wa shule ambao hupimwa kwa kuangalia matokeo ya shule husika. Matokeo ya shule
husika pia hupimwa kwa kuangalia wastani wa mafanikio ya wanafunzi kwa kipindi
chote cha ujifunzaji wao. Mafanikio ya mwanafunzi kwa kipindi chote cha mafunzo
hupiwa kwa mtihani wa mwisho unaompima mwanafunzi mambo yote aliyojifunza kwa kipindi kilichopangwa. Mitihani ya taifa, ni moja ya njia ya kupima ufanisi wa shule.
Katika lugha
ya kawaida, ninaweza kusema kuwa, ufanisi wa shule hupimwa kwa kuangalia
kiwango cha ufaulu wa wanafunzi. Ndio maana hata wazazi hushawishika haraka
sana kuwapeleka watoto wao kwenye shule zinazoongoza kwa ufaulu katika mitihani
ya taifa. Wakati mwingine, ubora wa shule huwa hauzingatiwi, bali ufanisi wake.
Kwa upande
mwingine, ninaposema ubora wa shule nina maana gani? Ubora wa shule ni
mjumuisho wa mikakati ya mabadiliko ya kielimu yenye lengo la kuongeza ufanisi wa shule
ikiwa ni pamoja na mikakati ya shule kuweza kuendana na mabadiliko husika. Miongoni
mwa mabadiliko haya ni pamoja na kuongeza idadi ya madarasa, kuongeza idadi ya
walimu na wafanya kazi, kuwaendeleza wafanyakazi n.k Mambo yote haya yanahitaji
maandalizi makini ili kuyafanikisha. Shule husika haina budi kujiandaa kikamilifu kupokea mabadiliko haya. Vinginevyo, mikakati itaishia vitabuni tu, utekelezaji utakuwa ni ndoto.
Ufanisi wa
shule unaweza kufikiwa kwa namna gani?
Kwa bahati
nzuri, hadi sasa, zipo tafiti nyingi zilizokwisha kufanyika zinazohusiana na
mambo ya kuzingatia katika kuboresha na kuongeza ufanisi wa shule. Tafiti hizi zimefanyika
maeneo mbali mbali ulimwenguni. Watafiti wengi
wa tafiti za uboreshaji na ufanisi wa shule wamegundua mambo kadhaa ya msingi
ya kuzingatiwa katika kuhakikisha ubora na ufanisi wa shule unafikiwa.
Watafiti wamegundua
kuwa, uongozi (kuanzia ngazi ya serikali hadi mashuleni), ushirikishwaji wa
wazazi na jamii, mazingira ya shule, aina ya mwanafunzi na familia atokayo,
ubora na wingi wa walimu, njia na mbinu bora za kufundishia, ubora na wingi wa
vifaa vya kujifunzia na kufundishia na muda wa mwanafunzi kujifunza, ni
baadhi ya mambo ya msingi ya kuzingatia katika kuleta ufanisi wa shule.
Katika makala
zitakazofuata, nitajaribu kufafanua, ni kwa namna gani mambo haya, na mengine
ambayo hayaja tajwa, yanavyoweza kuchangia ufanisi wa shule. Hata hivyo, mambo
haya ya msingi yanayoelezwa na watafiti mbalimbali hayawezi kuleta mabadiliko
kama hakuna uwajibikaji. Binafsi,
ninaona uwajibikaji utakaoleta uwajibishwaji ndio msingi wa mambo mengine yote
niliyoyataja hapo juu. Kwa maana hii, katika makala zinazofuata, swala hili
nalo litajadiliwa kwa kina.
Comments