Utaratibu Huu wa Kuoa/Olewa ni Mzuri, Unahitaji Kuboreshwa Kidogo.
Picha kwa hisani ya Gospel Kitaa.
Hakuna asiyejua shughuli ya kuoa/olewa ilivyo na pilika
pilika nyingi na za kuchosha. Siyo tu
hupoteza muda na fedha, mara nyingine huishia kwa watu kugombana, kuwekeana
chuki na vinyongo visivyoisha. Asilimia kubwa
ya fedha za harusi hutokana na michango ya watu mbalimbali kuanzia ndugu, jamaa
na marafiki.
Harusi ni sherehe ifanywayo kwa ajili ya kufurahia tukio muhimu
la kufunga ndoa. Sherehe hii huja mara baada ya wapendanao kufunga ndoa kanisani, msikitini, serikalini ama kwa
utamaduni. Hadi siku ya ndoa, sherehe
ndogo ndogo za awali kama za kutambulishana, yaani ndugu wa pande mbili
kufahamiana, kuvishana pete za uchumba, utoaji wa mahari, kapu la mama na send off hufanyika.
Sherehe ya awali kabisa inayowashirikisha watu nje ya
familia ni kapu la mama. Sherehe hii ni sehemu ya maandalizi ya sherehe ya
kumuaga msichana (mara nyingi hufanywa upande wa msichana). Hapa mama wa
msichana ndiye mhangaikaji mkuu. Hugharamia kiasi cha chakula na vinywaji
akitegemea kupata fedha za zaidi za kuandaa sherehe ya kumuaga msichana wake. Yawezekana utaratibu huu haupo kwa makabila
mengine (au upo wa namna kama hii), lakini kwa wachaga, utaratibu huu upo. Baada
ya kapu la mama, sherehe inayofuata ni ya send off, ile ya kumuaga mtoto wa
kike.
Sherehe ya kumuaga msichana, maarufu kama send off, imekuwa
moja ya sherehe muhimu katika kuelekea kwenye ndoa. Sherehe hii, huwa na
shamra shamra nyingi, wakati mwingine hufana hata kuliko sherehe ya ndoa, yaani
harusi. Sherehe hii (mara nyingi) hufanikishwa pia kupitia michango ya ndugu,
jamaa na marafiki.
Hata hivyo, kwa sasa hali ni tofauti kidogo. Kuna mfumo mpya
unaingia miongoni mwa wanajamii. Ndio unachipukia, lakini nina imani kubwa siku
za usoni, utakuwa ni utaratibu. Kama tu wasichana walivyoanza kuvaa hadharani suruali
na nguo nyingine za kubana. Mwanzo ulikuwa mgumu, walionekana wasiokuwa na
maadili. Kwa sasa, hali ni tofauti, umekuwa ni mfumo wa uvaaji wa kawaida
kabisa. Ninaamini, mfumo huu nao utakubalika katika jamii, pamoja na kuwa,
unahitaji kuboreshwa (kwa mtazamo wangu).
Kwa hakika sherehe hizi zinagharimu fedha na muda mwingi wa
wanajamii. Bahati mbaya, gharama hizi huelekezwa zaidi kwa ndugu, jamaa na
marafiki. Michango ya ugonjwa, masomo, ujenzi
n.k haiwezi kupata fedha za kutosha kama ilivyo kwa sherehe hizi za
harusi. Hata hivyo ni nadra sana kwa mambo mengine ya kimaendeleo (ya mtu
binafsi) na magonjwa kuchangiwa. Watu hawana mpango wa kuchangia mambo
ambayo hawatahusika kwenye matumizi ya walichochanga. Hii ni aibu kubwa sana
kwa jamii yetu ya kitanzania. Hatuna budi kubadilika.
Kuna wimbi kubwa la vijana wanaopata ridhaa ya kuanza kuishi
kama mke na mume mara baada ya kutambulishana. Sherehe ya kutambulishana, mbali
na kuwakutanisha ndugu wa pande zote mbili, majirani pia hualikwa katika
shughuli hii. Kwa hiyo, watu wengi
hukutana na hivyo sherehe hii huwa kubwa kidogo lakini inayoandaliwa na wanafamilia zaidi. Wakati mwingine,
wapendanao hutumia fursa hii kuvishana pete za uchumba. Sherehe hii kwa
wanaotarajia kuishi pamoja, huitumia kama tiketi ya kuanza maisha kama
wanandoa, hata kabla y kufunga ndoa. Utaratibu huu upo, na ni imani yangu kuwa,
siku za hivi karibuni utazoeleka na kuwa utaratibu rasmi.
Kwa mtazamo wangu, mfumo huu unafaa. Ni mfumo nafuu, usiohitaji
muda mwingi na kuchangishana fedha kutoka kwa ndugu, jamaa, na marafiki. Bila kujificha
kwenye shamba la karanga, mimi ni mmoja wa watu wasiyependa sherehe hizi.
Sizipendi kwa kuwa sioni ulazima wake, na pia, wananchi masikini hubebeshwa
mzigo mzito wasioumudu. Kwa sasa, kwa mwaka mtu anaweza kuwa na kadi za
michango ya harusi zisizopungua tano. Kwa bahati mbaya sana, siku hizi kuna
viwango vya kuchanga.Ukichanga chini ya kiasi kilichokubaliwa, adhabu ya kwanza ni kutopewa kadi ya mwaliko.
Watu hawasemi lakini michango hii imekuwa kero kubwa sana
kwa wanajamii. jamii haipendi, wengi
hulazimika kuchanga, msukumo mkubwa
ukiwa ni kuchangiwa pindi watakapokuwa na shughuli kama hizo na kutokutengwa katika shughuli za namna hiyo(watu husahau namna wanavyotengwa wakati wa matatizo). Na sababu
nyingine ni kuwa, wachangiaji hutegemea kurudisha sehemu ya fedha yao kwa kula
na kunywa siku ya sherehe husika. Kununiana na sintofahamu huweza kujitokeza
pale mtu aliyechanga fedha yake na hakualikwa kwenye hafla.
Nimeanza kwa maelezo
marefu ili upate picha halisi ya namna shughuli ya ufungaji ndoa inavyoambatana
na sherehe zinazotegemea kufanikishwa
kupitia nguvu ya kifedha na muda wa ndugu, jamaa na marafiki.
Mfumo huu wa wapendanao kuanza kuishi mara baada ya kutambulishana,
ni mwanzo mzuri wa kuepuka kuitwika jamii gharama zisizo za lazima. Katika mfumo
huu (mpya), wapendanao huishi kwa muda, na baadae huja kubariki ndoa kwa
gharama nafuu bila ya kuandaa harusi. Pamoja na kuwa watu hawa wanaishi bila
kukamilisha ndoa, huu ni mwanzo mzuri wa kupunguza kuitumikisha jamii kwa
kuwapotezea muda wao pamoja na kuingia gharama zisizo za lazima.
Ningependa utaratibu huu uboreshwe kidogo. Ndoa ifungwe siku
hiyo hiyo ya kutambulishana. Badala ya kuvishana pete ya uchumba, wavishane pete za ndoa kwa kufuata utaratibu wa imani zao. Yaani ndoa ifungwe siku hiyo hiyo ya
kutambulishana. Hatua hii ya kuwakutanisha ndugu wa pande mbili, ni ishara kuwa
wawili hao, wameshakubaliana kuoana. Taratibu za ndoa zifanyike kama kawaida,
ile siku ya kutambulishana, ndoa ifungwe. Mambo yaishie hapo. Huu utakuwa
utaratibu nafuu kabisa wa ufungwaji ndoa usiotumia muda mwingi na fedha nyingi
za watu.
Natamani vijana wangenielewa. Ninatamani wale wanaotarajia
kufunga ndoa wangepanga utaratibu huu. Natamani viongozi wa dini wangeuchukua
ushauri huu. Ninafahamu taratibu za kuoa/olewa zinaweza kutofautiana kulingana na mahali, imani, hata na utamaduni.
Lakini, katika hali zote hizi, shughuli hii ni dhahiri kuwa, mfumo wake hugharimu
sana fedha na muda wa watanzania.
Vijana sisi ndio wa kuleta mabadiliko, hatuna budi
kuyakubali mabadiliko yenye tija, hususani katika zama hizi za ugumu wa ajira.
Si sahihi sana kuendelea kushikilia taratibu zisizo na tija, zinazochukua muda
na fedha nyingi ambazo zingetusaidia katika shughuli za maendeleo. Ninatambua
ni vigumu kuibadili jamii, hususani katika hili, lakini, tukiamua tunaweza.
Nitakuwa mjinga kabisa kama nitapiga vita michango ya
kuwasaidia waliopenda kusoma lakini wakakosa fursa hii kwa sababu ya kukosa ada,
au kupiga vita mchango wa kumsaidia mtu mgonjwa aliyekosa matibabu bora kwa
kukosa fedha ya kugharamia matibabu.
Tumekosa maabara mashuleni, tumekosa nyumba za walimu,
tumekosa vyoo vya wanafunzi na walimu, tumekosa fedha ya kuwapa motisha walimu,
tumekosa fedha ya kujenga wodi za akina mama wanaolala zaidi ya mmoja
katika kitanda kimoja, lakini tunaweza kukusanya mamilioni ya kumwambia mototo wa
kike kwa heri, na mamilioni ya harusi ya siku moja.
Wazazi chonde chonde,
tubadilike, huu siyo ustaarabu wala ishara ya ushirikiano. Bila kujali jamii
nyingine zinafanyaje, lakini ninapaza sauti yangu kwa jamii ya watanzania,
tubadilike. Niungeni mkono, kwa pamoja tuibadili jamii yetu. Tuungane katika
mambo ya maendeleo. Inawezekana wazazi
wakakaa na mtoto wao sebuleni, wakampa wosia, wakampa na fedha walizotaka
kumuagia kwa send off, aende akaanzie maisha. Ndoa inaweza kufungwa kanisani,
msikitini au serikalini na watu wakafurahia siku hiyo majumbani kwao, au kama
wanauwezo wa kutosha, wakaalika watu wajumuike nao bila kuwachangisha
mamilioni ya shilingi. Mambo haya yanawezekana tukiamua.
Comments