Uyoga huu wa Ajabu!



Dunia ina mengi ya kufurahisha na pia ya kustaajabisha kama sio kushangaza.

Juzi nikiwa nyumbani nimejipumzisha chini ya mti wenye kivuli kizuri huku nikipata upepo mwanana,ghafla nilianza kuhisi harufu kama ya mzoga(mnyama aliyekufa). Harufu ile iliniwewesesha kwa kweli na ndipo iliponilazimu kuanza kufuatilia huo mzoga ambao nilijua lazima utakuwa ni wa mnyama tu.


Nilifuatilia kwa makini katika eneo lile na kwa msaada wa kundi la inzi(ati wanasema inzi wana busara sana,huwa wako makini sana kutujulisha pale penye mzoga au kinyesi ili tusikanyage au kusogea karibu) niliweza kuona ulipo mzoga huo.


Nilisogea karibu pamoja na harufu kali ya mzoga. Kinyume na matarajio yangu, niliuona UYOGA unaostawi vizuri ndio huo hasa uliokuwa umezingirwa na nzi pale nchani. Niliona ni vema niupige picha na kisha nikauondoa nikaenda kuutupa mbali na harufu ile ikawa imetoweka.


Siku tatu baadae nikaihisi harufu ile na cha kwanza nilichofanya ni kwenda eneo lile na kukagua kama kuna uyoga wa aina ile. Kweli niliikuta miwili na nzi walikuwa wameizingira. Ilinibidi kwa mara nyingine tena iiondoe na kwenda kuitupa mbali na harufu ile inukayo kama ya mnyama aliyekufa ikakoma na hali ya hewa ikawa safi na mpaka sasa sijaona uyoga huo na sijahisi tena harufu hiyo kali.


Ni uyoga wa ajabu kwa kweli, na kama kuna yeyote aliyewahi kukutana nao au wenye utaalamu kuhusu uyoga(bila shaka ndugu Bennet,mzee wa Mitiki ni miongoni mwao)watupe maelezo ya kina kuhusu uyoga huu kwa kadiri wawezavyo.

Comments

Nami nilitaka kusema kuwa Kaka Benet atakuwa na utaalamu juu ya hili.
Tusubiri utaalamu wake.
Albert Kissima said…
Ni kweli kaka. Uyoga huu umeendea kuota, na nimeendelea kuuchunguza. Nimefanikiwa kupata hatua ya mwanzo kabisa ya ukuaji wa uyoga huu. Hivi punde nitaweka picha ionyeshayo hatua hiyo.
Bennet said…
Hii ni aina ya uyoga uitwao stinkhorns mushroom ni uyoga toka jamii ya phallales ambao mara nyingi hupatikana kama taka za mbao zimemwagwa sehemu
Uyoga huu pamoja na kuwa na harufu mbaya lakini hauna sumu lakini huwa na sumu unapoanza kuota tu
Njjia za kupambana nao ili kuuondoa ni kuondoa mara unapoanza kuota kabla ya kutoa harufu mbaya au mwagia copper sulphate iliyochanganywa na maji, pia unaweza kuondoa mabaki ya mbao ili usiote tena
Albert Kissima said…
Nashukuru kaka Bennet kwa maelezo yako mazuri, nimeifurahia elimu hii kwa hakika.

Kwa bahati nzuri niliweza kupata hatua ya mwanzo kabisa ya uotaji wa uyoga huu. Nitaiweka pia kwa manufaa yangu na ya wengine katika harakati za kujifunza zaidi.

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili