Friday, December 30, 2016

Unapenda Kutumia Vitumizi vya Android kwenye Kompyuta Yako? Mfumo Endeshi wa Remix ni Jibu Lako.


                                                Skrinishoti kutoka Tovuti ya RemixOS

Hakuna shaka kuwa ili uifaidi simu yako vizuri, inapendeza sana ikiwa utaweza kuweka vitumizi (applications) unavyovipenda. Ni muhimu kutambua kuwa, aina na wingi wa vitumizi vizuri unavyoweza kuvitumia hutegemea na aina ya Mfumo Endeshi (Operating System) wa simu au kifaa chako. Hii ina maana kuwa, unaponunua simu, ni vyema ukafahamu ni aina gani ya Mfumo Endeshi ungependa kuutumia na ikiwa utakuwezesha kutumia vitumizi unavyovipenda.

Kwa sasa, moja ya Mfumo Endeshi pendwa kabisa wa simu ni Android. Ni dhahiri kuwa, Mfumo Endeshi huu una mkusanyiko wa vitumizi vizuri sana kwa simu. Haishangazi kuona kitumizi fulani kinapatikana kwenye Android lakini hakiwezi kutumika kwenye mazingira mengine kama vile ya Windows na mifumo endeshi mingine. Mara nyingi, kitumizi kikiweza kutumika kwenye Windows, ni vigumu sana kukikosa kwenye mfumo wa Android. Ila, kinyume chake, inawezekana kabisa.

Umekipenda kitumizi fulani cha simu na ukashindwa kukitumia kwa kuwa hakiendani na mfumo wa simu yako? Bila shaka hali kama hizi zimesha kukuta. Unaweza kuona ni kwa namna gani hali kama hizi zinavyokuwa ngumu kukubalika. Unaweza kujuta ni kwa nini ulinunua simu inayotumia mfumo endeshi fulani. Hata hivyo, tukubaliane kuwa, si rahisi kupata simu inayokidhi kila hitaji lako.

Hali kama hii imenikuta mimi. Nimeshindwa kutumia kitumizi cha simu nilichotokea kukipenda kwa kuwa mfumo endeshi wa simu yangu hauruhusu. Kwa sasa, kitumizi hiki kinaweza kutumiwa tu kwenye Mfumo Endeshi wa Android. Bahati mbaya, simu yangu inatumia mfumo wa Windows ambao hauniruhusu kutumia kitumizi hiki. Kwa namna nilivyokipenda, nililazimika kufanya utafiti mtandaoni ili kupata namna ya kuweza kukitumia kitumizi hiki katika mfumo wa windows.

Kama kawaida yangu, nisiyependa kushindwa, hususani linapokuja suala la simu na Kompyuta. Siku zote, nipo tayari kuweka rehani simu/ kompyuta yangu, alimradi nimejaribu kutatua changamoto ya kiteknolojia inayonikabili. Ikibidi kuondoa mfumo uliopo na kuweka mwingine. Katika hali kama hii, simu na Kompyuta hugeuka vifaa vya majaribio. Kwangu si tatizo ikiwa vifaa hivi vitaharibika. 

Nimesoma machapisho na kuangalia video kadhaa za namna ya kuingiza vitumizi vya Android kwenye simu ya mkononi inayotumia mfumo wa Windows. Nimejifunza kuhusu Project Astoria ya Windows ya kusaidia kutumia vitumizi vya Android kwenye simu za mfumo wa windows. Hata hivyo, nimegundua kuwa, Microsoft walishasitisha mradi huu. Nimepitia maelezo kadhaa ya namna ya kuweka vitumizi vya Android katika simu zinazotumia windows. Yapo mtandaoni. Kwa bahati mbaya, sikufanikiwa kwa aina ya simu ninayoitumia. Hata hivyo, sikukata tamaa.

Nilihamia kwenye Kompyuta. Huku nimejifunza namna nyingi sana za kutumia vitumizi vya Android kwenye mfumo wa Windows. Namna hizi kwa kimombo zinaitwa "Android Emulators". Baadhi ya Emulators ni kama vile Blue Stacks ambayo bila shaka ni maarufu sana miongoni mwa watu wengi. Emulators nyingine ni kama vile Manymo, Genymotion na nyingine nyingi ambazo unaweza kuzisoma zaidi hapa.

Shukrani kwa Mradi wa Android X86. Huu ni mradi unaowawezesha watumiaji wa Android kuweka mfumo Endeshi wa Android kwenye kompyuta zao. Hii ina maana kuwa, kwa sasa, unaweza kutumia toleo la Android 6 Marshmallow kwenye Kompyuta yako. MarshMallow ni moja ya matoleo ya android ya hivi karibuni ukiachilia toleo jipya kabisa la hivi karibuni la Android 7.0 Nougat. Unaweza kuingia kwenye You Tube na kuangalia namna ya kuweka Android X86 kwenye Kompyuta yako.

Hata hivyo, kilichonishawishi zaidi kuandika makala haya, ni kukutana na namna nyingine ya kutumia vitumizi vya Android kwenye Kompyuta yako. Namna hii ni ile ya kuweka Remix OS kwenye Kompyuta kama jinsi unavyoweka Mifumo Endeshi mingine.  Remix OS ni mfumo kama ilivyo mifumo ya Windows, Android, Ubuntu, Linus n.k inayokuwezesha kutumia vitumizi vya Android kwenye Kompyuta yako.

Awali, Remix OS  ilifahamika kama Remix OS Player iliyokuwa na Madhumuni ya kuwasaidia wanaopenda michezo ya Android kuchezea kwenye Kompyuta zao. Kwa sasa, kwa kutumia Remix Os, unaweza kufanya chochote ambacho unaweza kukifanya kwenye mifumo mingine kama vile ya Windows, Android n.k. Vitumizi kama vile vya MS Office na PDF vipo. Unaweza kutumia mtandao wa Internet, kutumia WhatsApp, email, kusikiliza mziki na mengine mengi.

Kwa sasa, hii ndio njia muafaka zaidi ninayoiona ikiwa unapenda kutumia vitumizi vya Android kwenye Kompyuta yako.  Angalau, Remix OS imekuwa suluhisho kwa hitaji langu. Bila shaka, inaweza kuwa pia njia mbadala kwako ikiwa huna simu inayotumia mfumo wa Andoid na ungependa kutumia vitumizi vya Android.

Uzuri wa Remix OS ni kuwa, si lazima uiweke (Install) kwenye "Local Disk C". Unaweza kuweka kwenye hifadhi nyingine kama "Local Disk D" na pia kwenye diski mweko (Ubs Flash disk) au kwenye kadi sakima (Memory Card) na ukaitumia pale unapoihitaji. Katika mtandao wa You tube, kuna maelekezo anuai ya namna unavyoweza kutumia Remix OS.

Habari njema ni kuwa, Mradi wa Android X86 na Remix OS wameamua kushirikiana ili kuongeza ufanisi zaidi katika miradi yao. Bila shaka, siku za usoni tunaweza kupata mambo mazuri zaidi. Kila la kheri kwa waanzilishi wa miradi hii, Jide na Huang.

Ninakutakia Mwaka Mpya Mwema wa 2017.


Thursday, October 8, 2015

Elimu inayozingatia uwezo(Competence Based Education): Maana na Misingi yake MikuuMatumizi ya TEHAMA ni moja ya njenzo muhimu ya kufanikisha Elimu inayozingatia uwezo mashuleni. Kupitia TEHAMA, wanafunzi wanaweza kujisomea popote na kwa wakati wao huku wakishirikiana na wenzao popote pale walipo. Picha kutoka HakiElimu


Kama nilivyotangulia kuandika katika makala iliyotangualia, ni takribani miaka kumi na ushei tangu elimu inayozingatia uwezo ilipoanza kutumika rasmi nchini Tanzania. Katika kipindi hiki, hakujakuwa na mafanikio ya kuridhisha sana katika ngazi zote za elimu. 

Wanafunzi wengi wanamaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wala kuandika, wanafunzi wengi wanamaliza shule za sekondari wakiwa wamepata madara yasiyoridhisha. Vile vile, vijana wa vyuo vikuu wanamaliza vyuo bila kuwa na stadi stahiki za kukabiliana na changamoto za kukosekana kwa ajira n.k.

Elimu inayozingatia uwezo ilitazamiwa kuwa ingeweza kukabiliana vyema na changamoto hizi za kufeli kwa wanafunzi pamoja na suala la ajira hususani kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu. Lakini, swali la kujiuliza ni kuwa, mfumo huu wa elimu kwa takribani miaka kumi ya uwepo wake, umetendewa haki au tuishie kusema kuwa siyo muafaka kwa mazingira yetu? Walimu wanaufahamu wa kutosha wa elimu hii? Je, ni kweli fikra za walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji zinaongozwa na misingi ya mfumo huu? 

Tafiti mbalimbali zilizoangalia matumizi sahihi ya elimu inayozingatia uwezo zinaonesha kuwa mfumo huu bado haujatumika ipasavyo mashuleni na hata vyuoni. Mambo kadhaa yameoneshwa kuwa yanahitajika kufanyiwa kazi. Suala la kwanza ni elimu kuhusu mfumo huu wa ufundishaji na ujifunzaji. Suala la pili ni uboreshaji wa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Lengo la Makala haya ni kujaribu kutatua changamoto ya kwanza, hii ya ufahamu kuhusu elimu inayozingatia uwezo. Nitajadili kuhusu maana pana ya elimu hii na misingi yake mikuu mitatu. 

Elimu inayozingatia Uwezo (Competency Based Education) ni nini?
Elimu Inayozingatia Uwezo ni mfumo wa elimu usiozingatia muda ambao mwanafunzi anapaswa kuutumia kujifunza kama kigezo cha kuwa amehitimu masomo bali hujikita kwenye maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma kwa kuangalia kama mwanafunzi husika amefikia malengo ya ujifunzaji yaliyokusudiwa au bado hajayafikia. 

Hii ina maana kwamba, muda siyo kigezo cha kumfanya mwanafunzi ahame ngazi moja ya elimu kwenda nyingine au kuhama mada moja kwenda nyingine. Kigezo kikubwa ni kama mwanafunzi amefikia lengo la kujifunza lililokusudiwa. Kama bado, ataendelea kujifunza hadi atakapofanikiwa. 

Kwa mfano, wanafunzi wanaojifunza kusoma na kuandika darasa la kwanza, hawataondoka darasa hilo hadi watakapoweza kusoma na kuandika, hata wakijifunza kwa zaidi ya mwaka mmoja. Wale wanaoweza kusoma na kuandika, wataendelea na ngazi nyingine, hata kama mwaka haujaisha. Huu ndio mfumo wa elimu inayozingatia uwezo kuliko umri au muda alioutumia mwanafunzi kujifunza. 

Bahati mbaya, walimu wengi mbali na kuwa dhana hii bado ni ngeni kwao, lakini pia, ni dhahiri kuwa, kwa mfumo maarufu wa kusoma kwa kuzingatia muda, utekelezaji wa mfumo huu bado una changamoto kubwa ya kuweza kutekelezwa ipasavyo hapa Tanzania. 

Mfumo huu wa elimu una misingi mikuu mitatu. Msingi wa kwanza ni kuwa, mwanafunzi ndiye kiini cha ujifunzaji (Learner-Centric)

Katika msingi huu, ujifunzaji unamlenga mwanafunzi mmoja mmoja (learner-centric). Mwanafunzi anapewa fursa ya kujifunza kwa wakati wake, popote alipo na wakati huo akishirikiana na wenzake kwenye kufikia malengo yake ya ujifunzaji. Mwanafunzi mmoja akifikia malengo yake ya ujifunzaji, haimaanishi kuwa ni lazima kwa wakati huo, wanafunzi wengine wanapaswa pia wawe wamefikia malengo ya ujifunzaji yaliyokusudiwa. Kila mwanafunzi hujifunza kwa wakati wake kulingana na uwezo wake. 

Msingi wa pili wa elimu inayozingatia Uwezo ni ujifunzaji unaozingatia matokeo (Outcome Based). 

Hii ni aina ya ujifunzaji ambayo hujikita zaidi kwenye kuhakikisha mwanafunzi amefanikiwa kupata kile kilichokusudiwa kwenye kujifunza. Siyo kuwa mwanafunzi ameelewa kwa kiasi gani, bali ameelewa au hajaelewa, amefikia lengo au hajafikia lengo. Mwanafunzi hataruhusiwa kuendelea na ngazi nyingine hadi pale kutakapokuwa na ushahidi usio wa mashaka kuwa, alichopaswa kujifunza amekielewa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa. 

Kwa hiyo, katika mfumo huu, jambo la kwanza kabisa linaloshauriwa ni kuhakikisha malengo mahsusi ya ujifunzaji yanaainishwa kwa ufahasaha na kwa umakini. Pia, kuhakikisha kuwa kuna vigezo madhubuti vya kuonesha kama mwanafunzi amefikia malengo au bado hajayafikia. Hii ni pamoja na kuwa na njia muafaka za upimaji na utoaji wa tathmini ya ufikiwaji wa malengo yaliyokusudiwa kwa wanafunzi. 

Msingi wa tatu wa elimu inayozingatia uwezo ni ujifunzaji unaozingatia mahitaji maalum ya mwanafunzi (Customized Learning). 

Misingi huu una maana kuwa, kila mwanafunzi ana mahitaji yake ya msingi ili kujifunza kwa tija. Wanafunzi wanatofautiana mitazamo, uwezo wa kiakili, uwezo wa wazazi kifedha na hata tamaduni. Kwa hiyo, mazingira ya ujifunzaji ya mwanafunzi mmoja mmoja ni lazima yaboreshwe na kubadilishwa ili yaendane na mahitaji ya mwanafunzi husika (customized learning). Nyezo za kujifunzia, mbinu na mazingira yanapaswa kuendana na matakwa ya mwanafunzi mwenyewe. Hata kile anachopaswa kukisoma, kinapaswa kiendane na matarajio, malengo na machaguo ya mwanafunzi mwenyewe. 

Ukweli ni kuwa, misingi hii ya elimu inayozingatia uwezo bado ni migumu sana kuitekeleza katika mazingira ya Tanzania. Angalao msingi mmoja tu wa mwanafunzi kuwa kiini cha ujifunzaji ndio unaotekelezwa. Hata hivyo, ni kwa kiasi kidogo sana.

Ili kufikia vyema malengo ya kumfanya mwanafunzi kuwa kiini cha ujifunzaji wake, moja ya nyenzo muhimu sana ni matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji na ujifunzaji. Tanzania bado tupo nyuma sana. Vitabu havitoshelezi, shule nyingi hazina miundombinu rafiki kama ya umeme na kadhalika. Hali hii bado inapelekea wanafunzi kutumia fursa chache zinazopatikana mahali Fulani tu kuhakikisha wanajifunza, muda wa kuhitimu ukifika, wote watahitimu, walioshindwa kufika malengo yao na wale waliofikia malengo yao ya kujifunza. Na hapa, dahana ya usawa katika kujifunza inakuwa imepotea.

Hata hivyo, hadi sasa, kuna juhudi kubwa nchini Tanzania zimeshafanyika na zinazoendelea kufanyika kuhakikisha wanafunzi wanafikiwa walipo katika kupata elimu kupitia TEHAMA. Baadhi ya makampuni binafsi na taasisi za serikali kama vile Ubongo Kids,  Edmodo (Chuo Kiuu cha Dodoma), elimu popote (Uhuru One) na wengine wengi wameshafanya kazi nzuri ya kuhakikisha elimu inapatika popote alipo anayependa kujifunza.

Saturday, October 3, 2015

Elimu Inayozingatia Uwezo: Bado Inasuasua, Wapi tunakosea?Picha kwa hisani ya gettingsmart
Elimu inayozingatia uwezo imeshika kasi zaidi kipindi cha hivi karibuni, hususani kwa mataifa ya Ulaya. Nchi kama Marekani imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kuhakikisha elimu hii inatumiwa mashuleni na vyuoni ili kuleta ufanisi unaopaswa. Kwa mfano,  blogu ya BlackBoard kwa kushirikiana na Baraza la Elimu la Marekani, tayari wameungana kufanya Tafiti za Elimu Inayozingatia Uwezo.
Utafiti wa hivi karibu wa BlackBoard na Baraza la Elimu la Marekani umejaribu kuangalia ni kwa kiasi gani Elimu Inayozingatia Uwezo inavyoweza kutekelezwa na pia mafuaa yake kijamii na kisera na namna ambavyo mfumo wa krediti na uwezo unavyotafsiriwa na wadau mbalimbali wa elimu.
Kutokana na ukweli kwamba, kiwango cha elimu nchini Tanzania kwa kipindi kirefu kimekuwa kikidorora kadiri siku zilivyokuwa zinaenda, moja ya muarobaini ulionekana ni kuazima mfumo wa Elimu unaozingatia Uwezo.  Hivyo basi, mwaka 2004, Tanzania kupitia Taasisi ya Elimu iliamua kubadili mitaala ya shule za msingi hadi vyuo vya ualimu ili iendane na matakwa ya aina hii ya elimu.
Mtaala uliokuwepo ulionekana umeshindwa kukidhi mahitaji ya sera na mikakati mbali mbali ya kielimu na ya kimaendeleo. Pia, tafiti mbalimbali zilzofanywa na wadau wa elimu ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania zilionesha umuhimu wa kufanyika kwa mabadiliko ya mitaala ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya Ualimu.
Kwa shule za msingi, mitaala inayozingatia ujifunzaji wa kuzingatia uwezo ilianza kutumiaka rasmi mwaka 2006, kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu, mtaala mpya ulianza kutumika rasmi mwaka 2005. Hakuna uhakika kama mabadiliko haya yalihusisha pia vyuo vikuu ambavyo huandaa walimu wa kusimamia utekelezaji wa mitaala mipya mashuleni inayohamashisha ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia uwezo.
Hata hivyo, mara baada ya kufanyika mabadili haya ya mitaala, mafanikio katika elimu yameendelea kulegalega kwa kiasi kikubwa. Ni takribani miaka kumi ya utekelezaji wa mitaala inayozingatia Ujifunzaji unaozingatia uwezo. Tumezidi kushuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi wanaomaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma, kuandika kuhesabu.
Utafiti wa Twaweza wa mwaka 2012 unaonesha kuwa nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 55 ya wanafunzi wa darasa la tatu hawakuweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili huku wanafunzi 8 kati ya 10 wa darasa la tatu wakishindwa kusoma hadithi ya kiingereza ya darasa la pili.  Pia, utafiti huo unaonesha kuwa, wanafunzi 7 kati ya 10 wa darasa la tatu hawakuweza kufanya hesabu ya kuzidisha ya darasa la pili.
Elimu ya sekondari nchini Tanzania nayo imekuwa ikisuasua kila kukicha. Matokeo ya mitihani Taifa ya kidato cha nne ya mwaka 2012 ndiyo yaliyokuwa matokeo mabaya katika historia ya mitihani ya Taifa inayosimamiwa na baraza la mitihani la Tanzania ambapo zaidi ya asilimia 65 ya watahiniwa walifeli mtihani huo.
Kufuatia kusuasua huku wa elimu, watafiti na wadau  mbali mbali  wa elimu wamekuwa wakitafiti mfumo huu wa elimu elimu ili kubaini mafanikio, changamoto na kisha kutoa mapendekezo ya nini cha kufanya.
Tafiti nyingi zilizofanyika nchini Tanzania zinaonesha kuwa walimu hawana uelewa wa kutosha kuhusu ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia uwezo. Kupitia tafiti hizi, imefahamika kuwa, walimu wengi wa shule za msingi na sekondari hawafahamu nini wanapaswa kutekeleza ili kuhakikisha wanafundisha kwa mujibu wa mitaala ya sasa. Hali kadhalika, tafiti zinaonesha kuwa waalimu wanafunzi wanaotarajiwa kwenda kufundisha mashuleni, hawana uelewa wa kutosha wa kuweza kufundisha kwa kuzingatia matakwa ya ufundishaji unaozingatia uwezo.  Pia, hali isiyoridhisha ya mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji inaonekana kuwa ni moja ya mambo yanayopelekea elimu inayozingatia uwezo wa mwanafunzi kuonekana kushindwa.
Wakati tafiti nyingi zinazohusu ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia uwezo zikiwa zimeelekezwa zaidi kwa walimu, tuna mswali kadhaa ya kujiuliza.
Kwanza, wahadhiri wa vyuo vikuu wanaufahamu vyema mfumo huu wa ufundishaji na ujifunzaji? Wanapofundisha walimu wanafunzi, fikra zao, ufundishaji wao na maono yao yanasimia kwenye mfumo huu? Vyuo Vikuu nchini Tanzania vinautumia mfumo huu kuwafundisha wanafunzi? Je, vyuo vikuu vinafahamu kwa upana wake misingi ya Elimu Inayozingatia uwezo na inaisimamia ipasavyo kwenye kutoa elimu? Pengine, maswali haya yanapaswa kujibiwa kupitia tafiti.
Hata hivyo, kuna ukweli kuwa,  vyuo vikuu vinatumia zaidi njia ya mihadhara kwenye ufundishaji. Labda wingi wa wanafunzi katika darasa moja inaweza kuwa ni moja ya sababu. Swali la kujiuliza ni kama, ufundishaji wa kuzingatia uwezo unaathiriwa na wingi wa wanafunzi darasani. Kujibu swali hili, ni vizuri kwanza tukaifahamu Elimu inayozingatia ujuzi pamoja na misingi yake. Tukutane katika makala ijayo.

Thursday, March 19, 2015

Shairi: Kilio cha Albino                   Picha kutoka Yahoo news

Kisa ni mbovu imani, Ndugu zetu mwawaua, [ Amir Kulanteni]
Mwamuabudu shetani, Mmezitupa sheria,
Twapita tu duniani, Kifo chaja kwenu pia,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Wenye dhima mwafanyani? Uhai kutulindia,
Wananchi mashakani, Nyie kiguu na njia,
Mara mpo marekani, Sisi huku tunalia,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Mwaiba mabilioni, Mwashindwa kututetea,
Ni kama watu usoni, Moyoni mwatumendea,
Ni kama tu hayawani, Imani zimepotea,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Vitendo vyangoja nini?, Matamko tu mwatoa,
Ndugu zetu kaburini, Hamuioni kadhia,
Matendo ya kishetani, Nyie mwayakaushia,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Twendeni makanisani, Tuombe huku twalia,
Twendeni misikitini, Tuzisome kali dua,
Mungu na awalaani, Motoni aje watia,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?  

Amiri wa Kulanteni, Beti umezipatia,       [Mutabazi Muta Mutabe]
Ujumbe zimesheheni, Saluti nakupigia,
Ni qadar ya manani, Si hali walonunua,
Kilio cha Albino, Sioni kama twajali.

Tungeingia vitani, Madhubuti pigania,
Twaishia viririni, Badae twapuuzia,
Mungu tumjibu nini, Siku ikishawadia,
Kilio cha Albino, Sioni kama twajali.

Twakomaa vijiweni, Mpira kuongelea,
Twaingia huzunini, Mechi tukijikosea,
Albino mdomoni, Moyoni twajipetea,
Kilio cha Albino, Sioni kama twajali.

Siishie facebukuni, Makali kuoneshea,
Tuingie mitaani, Watu kuhamasishia,
Aridhia Rahmani, Haki tukipigania,
Kilio cha Albino, Sioni kama twajali.

Simanzi tele moyoni, Binadamu kuuana,     [Albert Kissima]
Tumekuwa hayawani, Rabuka tumemkana,
Utu u wapi jamani, Tunusuru maulana,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Ni ajabu duniani, Ugonjwa kuwa ni dili,
Kisa hii melanini, Binadamu kawa mali,
Potofu hii imani, Tupinge kwa kila hali,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Kwa panga wanawakata, Albino wakiwa hai,
Mateso wanayopata, Nani ambaye halii?,
Dhoruba itawakuta, Kamwe habaki adui,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Viungo vya binadamu, Kutolewa akiwa hai,
Kwa mapanga sina hamu, Kuvumilia haifai,
Na kamwe hayatadumu, Wauaji mabedui,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Hali hii hadi lini, Tunaweza kukabili,
Kwa pamoja tulaani, Sote na tuwe wakali,
Tuwaweke hadharani, Wauaji mafedhuli,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Baraka wa Cosimasi, Albino wa Sumbawanga,
Mungu akupe wepesi, Na azidi kukuchunga,
Upone kwa kasi, Akulinde na majanga,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Ulale pema Yohana, Alubino wa Geita,
Hakupenda Maulana, Madhila yalokukuta,
Tunamuomba rabana, Wengine kutowakuta,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?

Dola chukua hatua, Madhila kuyamaliza,
Raia tukiamua, Kukomesha tunaweza,
Ndugu zetu wanalia, Ni sharti kuwatuliza,
Kilio cha Albino, Hivi kweli tunajali?          

Shairi hili limeandaliwa na Amir, Ashiru na Albert.