Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani? Sehemu ya Pili.
Picha kutoka Mtandaoni na kuboreshwa na mwandishi wa Makala haya. |
Makala haya yanalenga kuendelea kujadili namna nyingine tatu zinazoweza kuzingatiwa na walimu na wanafunzi ili kufanikisha utekelezaji wa mitaala inayomzingatia mwanafunzi. Kwenye makala haya, tutaaangalia wajibu wa kujifunza, nafasi ya mwalimu na mwanafunzi kuhusu masuala ya ujifunzaji na malengo ya upimaji wa mwanafunzi.
Wajibu wa Kujifunza.
Wajibu wa kujifunza ni hali ya utayari wa mwanafunzi kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji bila kulazimishwa ama kushurutishwa. Hali ilivyo sasa, wanafunzi wanafahamu wajibu wa mwalimu ni kuleta maarifa darasani na wajibu wa wanafunzi ni kumsikiliza mwalimu na kuandika nukuu.
Katika mfumo huu, mwalimu ndiye anayehangaika kujifunza kisha anakuja darasani kufafanua kile alichojifunza. Huu ndio mfumo wa ujifunzaji unaomzingatia mwalimu. Kazi ya wanafunzi angalao inakuwa ni kunakili nukuu na nadra sana kuuliza maswali.
Ili kutimiza matakwa ya ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi, wanafunzi ndio wanaopaswa kuwa wajifunzaji wakuu. Hii ni kusema kuwa, ule wajibu wa mwalimu wa kujifunza kisha anakuja darasani kuelezea aliyojifunza, unapaswa sasa kufanywa na wanafunzi wenyewe. Hapa unaweza kuwaza pia ni kwa kiasi gani darasa linavyoweza kuwa na walimu wengi.
Wanafunzi wanapojenga tabia ya kujituma kwa bidii, ujifunzaji unakuwa ni wajibu wao wa msingi. Hali hii inapelekea wanafunzi kujenga tabia (nzuri) ya kutokumuhitaji sana mwalimu na badala yake, atahitaji zaidi "resources" za kujifunzia. Hapa ndipo tunapojenga jamii ya watu wenye tabia ya ujifunzaji endelevu (life long learners).
Ujifunzaji wa namna hii una maana kubwa sana kwa maisha ya mwanafunzi na kwenye maisha ya kazi. Kwanza, mwanafunzi anakuwa amejenga tabia ya kuwa mjifunzaji mwendelevu. Hii ni moja ya sifa ya muhimu sana kwenye kujiajiri au kwenye ajira. Ukichunguza vyema kwenye matangazo ya kazi, utakuta moja ya sifa ni uwezo wa kuwa tayari kujifunza mambo mapya pale inapobidi. Tabia hii si rahisi sana kuonekana kwa mtu ambaye amezoea kuhadithiwa kila anachopaswa kukijifunza.
Faida nyingine ni kujenga uwezo wa stadi muhimu kama vile kutatua changamoto, fikra tunduizi, udadisi, kuwa mbunifu, kuwasiliana na kadhalika. Stadi hizi hazina somo maalum za kuzifundisha bali mwanafunzi huzipata kwenye mchakato wa ujifunzaji. Kinachotokea ni kuwa, mwalimu kwa kuwa anaweka juhudi nyingi kujiandaa, yeye ndiye anayeboresha stadi hizi zaidi na hivyo kujifunza zaidi.
Malengo na Mchakato wa Upimaji na Tathmini ya Wanafunzi
Hili ni eneo jingine la msingi kabisa la kujadili na kulielewa katika ufundishaji na ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi. Upimaji na tathmini ndio dira ya mchakato wa ujifunzaji. Mchakato huu unasaidia kutoa taarifa ya mwenendo wa ujifunzaji; wanafunzi walikuwa wapi, wapo wapi, wanakwenda wapi na nini kifanyike ili wafikie wanapotakiwa kwenda.
Kwa mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji wa sasa, mchakato wa upimaji na tathmmini hufanywa kwa kuzingatia muda fulani na hufanyika kwa msimu. Kwa mfano, ni utaratibu wa kawaida kabisa katika mfumo wa mafunzo wanafunzi kuelezwa kuwa testi itafanyika wiki ya tano na ya saba. Mara nyingi majaribio haya huwa kwa ajili ya tathmini pekee kwa maana ya kuhitaji alama na si kwa lengo la kuboresha ujifunzaji.
Katika ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi, kuna mambo kadhaa yanapaswa kutiliwa maanani. Jambo la kwanza ni taasisi au walimu kuwekeza zaidi kwenye upimaji endelevu. Hii ni aina ya upimaji inayofanywa wakati wote wa ujifunzaji wa mwanafunzi kupitia kazi za kila siku anazozifanya mwanafunzi.
Lengo la upimaji huu ni kufuatilia namna mwanafunzi anavyojibidisha kufikia malengo ya ujifunzaji, wapi anakwama, wapi anapatia na ni kwa namna gani anaweza kusaidiwa kusonga mbele.
Jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa ni kufahamu kuwa upimaji unapaswa kuwa endelevu na usiotofautishwa na mchakato wa ujifunzaji. Mwalimu ana wajibu wa kufuatilia namna wanafunzi wanavyotatua changamoto. Pia, ana wajibu wa kuweka rekodi ya namna wanavyoweza na namna wanavyoshishwa na kisha kujadiliana ni vitu gani vinahitajika ili kufikia kile kinachokusudiwa.
Mwalimu anapaswa pia kuwasaidia wanafunzi kujiuliza maswali magumu (mabunio, hypotheses) na kisha wanafunzi hao hao kuyatafutia majibu au kuthibitisha mabunio yao. Wakati wote huu, mwalimu anapaswa kuwa anafuatili kwa ukaribu wanafunzi wanavyofanya shughuli hizi na kuwasadia kujiuliza maswali zaidi na sehemu sahihi za kupata nyenzo za kujibia maswali au kuthibitisha mabunio yao.
Kwa utaratibu huu, upimaji unakuwa ni ufundishaji unachagiza uwajibikaji wa wanafunzi. Utayari wa wanafunzi kushiriki somo ikiwa ni pamoja na upimaji binafsi na na wanafunzi kupimana yanakuwa moja ya mambo yanayotarajiwa kujitokeza kwenye darasa la namna hii.
Uhuru wa Kufanya Maamuzi
Uhuru wa kufanya maamuzi ni moja ya mambo kwa walimu na wanafunzi ni moja ya mambo ya msingi kwenye ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi. Hali ilivyo sasa, maamuzi mengi yanaanzia kwenye ofisi au ngazi za juu zinazosimamia elimu au kwa walimu.
Kwa mfano, utaratibu wa upimaji na tathmini unaweza kumuliwa na waandaaji wa mtaala na ikasisitizwa mfumo huo lazima utakelezwe kama ulivyo. Wakati mwingine, mwalimu anaamua leo atumie mbinu zipi za kujifunzia. Wanafunzi wao kinachobaki ni kufuata tu kile wanachoelekezwa.
Hali inapaswa kuwa vipi kwenye ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi? Kwanza, wanafunzi wanaweza kupewa uhuru wa kuamua kwa pamoja na mwalimu wao mambo kadhaa. kwa mfano, kulingana na naina ya lengo kuu au mahususi, wanafunzi wanaweza kujadiliana ni kwa namna gani watajifunza. Kumbuka, kile wanafunzi wanachokubalina kinaweza kuwa kirahisi kukitekeleza kuliko kile wanachoambiwa tu wakitekeleze.
Pia, kushirikishana kwenye maamuzi kunaweza kufanyika pia kwenye upimaji na tathmini. Wanafunzi wanaweza kujadiliana kwa kushirikiana na mwalimu kuhusu njia wanazozipenda kwa ajili ya kufuatilia malendeleo yao na kwa ajili ya tathmini. Kama ni tathmini ifanyike kwa wakati gani na kwa namna gani. Tukumbuke uhuru huu unaweza kuhamasisha uwajibikaji na utayari wa kufanya vizuri shughuli mbalimbali za ujifunzaji.
Mwisho, kuna uwezekano mkubwa kuwa walimu wanaosoma makala haya wakaona utekelezaji wake ni mgumu. Ninachoamini ni kuwa, tunaweza kutumia rasilimali chache kabisa zilizopo kuhakikisha mambo haya yanatekelezwa.
Tufahamu kuwa, wanafunzi wenye tabia endelevu ya kujifunza wanaweza kujifunza popote na kwa kutumia rasilimali chache zilizopo. Tunaweza kuwaza kuhusu idadi kubwa ya wanafunzi. Changamoto kubwa inaanzia kwenye kufanya tathmini badala ya upimaji endelevu.
Ujifunzaji miongoni mwa wanafunzi wenye tabia endelevu ya kujifunza humfanya kila mwanafunzi kujifuatilia mwenyewe na kuwajibika. Kila mwanafunzi ni mwalimu kwa utaratibu huu. Hivyo, ni rahisi mwalimu kufuatilia kile wanafunzi wanachokifanya.
Ujifunzaji miongoni mwa wanafunzi wenye tabia endelevu ya kujifunza humfanya kila mwanafunzi kujifuatilia mwenyewe na kuwajibika. Kila mwanafunzi ni mwalimu kwa utaratibu huu. Hivyo, ni rahisi mwalimu kufuatilia kile wanafunzi wanachokifanya.
Ukipitia mwanafunzi kadhaa kwenye makundi au mmoja mmoja unaweza kuelewa mwenendo wa darasa na hivyo kufahamu mahali palipo na changamoto na panapohitaji mkazo zaidi. Pia kupata wasaha wa kuwaongoza wanafunzi ni nyenzo zipi wanaweza kuzitumia kuhakikisha wanafikia malengo yao.
Ni nafuu kuanza katika changamoto katika kufanya jambo sahihi kwani utakuwa kwenye nafasi sahihi ya kueleza unachokabiliana nacho kuliko kuelezea changamoto za jambo ambalo hujalifanya kabisa. inakuwa vigumu hata mtu kuelewa ni wapi haswa anaweza kusaidia au kuweka nguvu zaidi. Hii ndio namna ya kushawishi watu wanaopaswa kuwajibika, wakawajibika.
Mwisho.
Mwisho.
Msingi wa makala hizi mbili ni andiko la Maryellen Weimer, Learner-Centered Teaching: Five Key Changes to Practice. Pia, Weimer ana kitabu kinachokwenda kwa jina kama la makala haya ambacho unaweza kupata muhtasari wake hapa ili kama utapendezwa nacho ukinunue.
Comments