Upimaji ni Ufundishaji Ikiwa Walimu Wataamua


  Mfano wa Andalio la Somo: Picha kwa hisani ya www.Jiandae.wordpress.com

Katika Makala zilizopita nimekuwa nikijadili mambo mbali mbali yanayohusu ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi. Huu ni mfumo wa uwezeshaji na ujifunzaji unaompa mwanafunzi fursa ya kutumia muda wake, maarifa yake na uwezo wake kiakili na kiuchumi katika kujifunza.

Kwenye makala zilizotangulia, kuna wakati nilisisitiza kuwa, madarasa yanapaswa kutazamwa kama “karakana za kujifunzia”. Hata hivyo, hali ni tofauti kwenye shule zetu. Madarasa yamekuwa kama vikao vya walimu vya kuwasilisha wanayojifunza wao. Ili elimu yetu iwe na manufaa, hatuna budi kubadili mtazamo kuhusu namna wanafunzi wanavyopaswa kujifunza.

Wanafunzi watambue wajibu wao wa kujituma katika kujifunza. Wafahamu kuwa wao ndio watendaji wakuu kwenye ujifunzaji wao. Kupitia ushiriki wao, wanafunzi wanajifunza stadi muhimu kama vile kujifunza namna ya kujifunza, kuwasiliana, uwezo mkubwa wa kufikiri na kutatua changamoto.

Katika kufanikisha haya, walimu hawana budi kubadili mtazamo wa namna wanavyopaswa kusimamia ujifunzaji. Wanapaswa kuongozwa na falsafa ya ujifunzaji na ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi. Makala zilizotangulia, zilijadili angalao kwa kina kuhusu ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi. Makala haya yanalenga kujadili nafasi na wajibu wa mwalimu lipapokuja suala la upimaji wa mwanafunzi kwenye ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi.

Upimaji ni mchakato wa kutambua ni kwa kiasi gani wanafunzi wanajifunza kile kinachokusudiwa kwao. Kuna aina kuu nne za upimaji ambazo ni awali, endelevu, tatuzi na tamati. Kwa ujumla, upimaji husaidia kuboresha namna ya kuwezesha na namna wanafunzi wanavyopaswa kujifunza vizuri zaidi.

Elimu inayozingatia uwezo imeweka msisitizo mkubwa kwenye upimaji endelevu. Hii ni aina ya upimaji inayolenga kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi kwa kila hatua ya ujifunzaji wake ili kuboresha ujifunzaji na uwezeshaji. Ndio maana, katika mitaala inayosisitiza ujifunzaji huu, ama upimaji endelevu umepewa nafasi kubwa zaidi kwenye alama za mwisho za mwanafunzi au angalao uzito ni nusu kwa nusu.

Katika mazingira kama haya, upimaji kwenye ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi ufanyike kwa namna gani?

Kwanza, ni vizuri tukafahamu kuwa kwenye ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi, ni vigumu kutenganisha njia/ mbinu za ufundishaji na upimaji. Kimsingi, mbinu za ufundishaji ndizo mbinu za upimaji ikiwa tunahitaji kuwezesha kwa ufasaha. Yawezekana ninakuchanganya. Tuendelee kutafakari kwa pamoja.

Kutafakari namna wanafunzi wanavyoweza kushiriki somo ni kutafakari kuhusu namna ya kuwasadia mwanafunzi wajifunze kupitia ushiriki wao. Kwa mfano, mwalimu anaweza kupanga wanafunzi wafanye kazi mradi. Hii ni njia ya ufundishaji. Pia ni shughuli kubwa ambayo wanafunzi wanapaswa kuikamilisha. Bila shaka, mbali na kuwa njia ya ufundishaji, inabaki pia kuwa ni njia ya upimaji.

Ndio maana, upimaji wa mwanafunzi kwenye ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi upo kwenye kila hatua ya ujifunzaji wa mwanafunzi. Ni sawa na kusema kuwa, upimaji ni shughuli ya msingi kabisa ya mwalimu kwa kila hatua ya ujifunzaji wa mwanafunzi.

Kwa mantiki hii, upimaji ni jambo linalopaswa kupangwa mapema kabisa kabla ya kuanza uwezeshaji. Kuamua kuhusu mbinu/ njia za kufundisha, ndio kuamua kuhusu mbinu/ njia za upimaji. Msingi wa hili ni kuwa, wanafunzi ndio watendaji wakuu. Kazi kubwa ya mwalimu ni kusaidia mazingira rafiki ya kujifunza. Msaada ambao utokana na ufuatiliaji wa namna mwanafunzi wanavyojifunza.

Wajibu wa mwalimu ni upi basi kwenye upimaji endelevu wa mwanafunzi?

Wajibu wa mwalimu ni kufuatilia namna wanafunzi wanavyofanya shughuli zao. Ufuatiliaji huu hufanyika ili kufahamu ni wapi mwanafunzi/ wanafunzi wanahitaji msaada na wa namna gani ili wajifunze kwa ufasaha.

Kuna wakati mwalimu anaweza kutoa ufafanuzi wa jambo. Pengine tunaweza kusema hii ni njia ya mhadhara. Hata hivyo, huu ni mrejesho anaoutoa kufuatia upimaji wake. Kwa hiyo, unaweza kujenga picha kuwa, kwenye ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi, mfululizo ni wanafunzi kupatiwa mazingira rafiki ya kujifunza kwa kutenda, mwalimu kufuatilia kwa ukaribu shughuli za wanafunzi na kupokea na kutoa mrejesho wa ujifunzaji.

Mwalimu atumie zana zipi kwenye upimaji?

Aina ya mbinu/ njia za upimaji/ ufundishaji huamua zana za upimaji. Unafikiri ikiwa mbinu ya ufundishaji/ upimaji ni maswali na majibu, zana ya upimaji itakuwa ni ipi? Inaweza kuwa ni mtihani, “checklist”, “rating scale” n.k? Ni kwa nmana gani mwalimu utajihakikishia kuwa mwanafunzi wanajibu inavyotakiwa? Pengine unaweza kuwa na orodha ya majibu yanayotarajiwa na kisha kufananisha orodha hiyo na majibu ya mwanafunzi. Hii inaweza kuwa “checklist” au “rating scale”.

Mtazamo huu ni wa muhimu kwa maoni yangu, hususani linapokuja suala la kuelewa vyema ni kwa nini kwenye maandalio ya masomo ya elimu inayomzingatia mwanafunzi, upimaji upo kila hatua ya somo. Kwa ujumla, mwalimu anaweza kujenga picha kuwa, njia anazofikiri ni za ufundishaji, ndizo njia za upimaji.

Ukitaka wanafunzi wajadili, utasikiliza wanachojadili. Ukitaka waandike, utasoma wanachoandika. Ukitakata wanafunzi waunganishe sakiti, utatazama wanavyounganisha nyaya n.k. Hizi ni njia/ mbinu za upimaji. Utajuaje kuwa wamefikia viwango vinavyokubalika? Kumbuka kuwa na zana ya kukupatia taarifa hizi muhimu kwa ajili ya mrejesho utakaosaidia kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi.

Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?