Ufundishaji wa Kiudadisi: Maana, Faida na Namna Unavyoweza Kutumiwa
Picha kwa hisani ya UNESCO learning Portal
Matumizi ya njia ya ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi
umeenea maeneo mbalimbali duniani na hususani katika nchi za Ulaya. Ufundishaji
Unaomzingatia Mwanafunzi ni mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji unaompa
mwanafunzi fursa ya kujibidisha ili kujipatia maarifa na kutumia maarifa yake
ya awali katika kujenga maarifa mapya badala ya kuwa mpokeaji wa maarifa na
kisha kuyatumia kwa namna ya kuyakariri.
Katika machapisho mbalimbali, Ufundishaji Unaomzingatia
Mwanafunzi umekuwa ukipewa majina anuai kama vile ufundishaji shirikishi,
ufundishaji unaomzingatia mtoto, ufundishaji wa Kiudadisi na majina mengine.
Hata hivyo, watumiaji wengi wa mfumo huu wa kufundishia na kujifunzia wanatumia zaidi istilahi ya
Ufundishaji wa Kiudadisi.
Ufundishaji wa Kiudadisi bila shaka ni istilahi pendwa kwa
kuwa inasadifu moja ya tabia muhimu ya udadisi anayopaswa kuwa nayo mwanafunzi
wakati wa ujifunzaji wake na hata katika maisha ya kawaida. Kwa msingi huu,
katika makala haya, mwandishi anajikita kwenye Ufundishaji wa Kiudadisi kama
moja ya mbinu na namna ya kutekeleza ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi.
Maana, faida na namna ya kutumia aina hii ya ufundishaji na ujifunzaji
itajadiliwa.
Maana ya Ujifunzaji
wa Kiudadisi
Ufundishaji wa kiudadisi ni aina ya ufundishaji unaompa mwanafunzi
fursa ya kujiuliza maswali yanayomuibulia hamasa ya kutaka kujua na hivyo
kujenga mabunio (hypotheses) na kisha kujituma kupata majibu ya maswali yake
kwa kurejea vyanzo mbalimbali ili hatimaye aweze kuongeza maarifa yake na ya
wengine kupitia majadiliano, uwasilishaji, machapisho, kazi mradi n.k. Vyanzo
mbalimbali anavyoweza kuvitumia mwanafunzi ni kama vile kuchunguza, kusoma
maandiko mbalimbali (kama vile vitabu, majarida n.k) pamoja na vyanzo vingine kama
vile internet, kutazama video, midahalo n.k.
Kama umeielewa vyema maana ya ujifunzaji wa Kiudadisi,
utagundua kuwa, maswali makini anayoweza kujiuliza mwanafunzi huku akisaidiwa
na mwalimu ni kiini cha mchakato wa kujifunza kwa udadisi. Mwanafunzi
anapojiuliza maswali, inamaanisha kuwa anahitaji majibu. Hivyo anakuwa amejipa
wajibu wa kujibidisha kupata majibu ya maswali yake. Maarifa ayapatayo
mwanafunzi anategemewa aweze kuyatumia katika kujenga na kutetea hoja zake
sambamba na kutatua changamoto halisi zinazomkumba yeye na jamii yake.
Faida za Ujifunzaji
wa Kiudadisi
Kama nilivyotangulia kugusia hapo awali, ufundishaji
unaomzingatia mwanafunzi umekubaliwa na unatumika kwa kiasi kikubwa sana na
mataifa ya Ulaya, kwa uchache huko bara Asia na kwa kiasi kidogo kabisa Barani
Afrika. Kutokana na umuhimu wa mfumo huu wa utoaji elimu, mataifa mengi ya Afrika kwa nyakati tofauti yamekuwa yakifanya mabadiliko yanayolenga kukidhi matakwa ya ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi.
Nchini Tanzania, kwa mfano, katika shule za msingi,
sekondari na vyuo vya ualimu, ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi
ulirasimishwa tangu mwaka 2005. Ni takribani miaka 12 ya utekelezaji wake. Hata hivyo, tafiti nyingi za hivi karibuni nchini Tanzania zinaonesha mfumo
huu hadi sasa haujafanikiwa kutokana na sababu mbalimbali. (Wasome watafiti kama vile Alberto Paulo,
Tillya, Mosha, Kafyulilo, Salema, Mtitu, Makunja na wengine wengi).
Hali ni tofauti katika nchi za Ulaya. Tafiti mbalimbali
zimeonesha mafaniko makubwa ya ufundishaji wa kiudadisi. Kwa mujibu wa tafiti
hizo, ufundishaji wa kiudadisi umeonekana kuwa na matokeo chanya yasiyo na
mashaka kama vile kumuwezesha mwanafunzi kupata mafanikio zaidi kielimu, kumjengea
mwanafunzi stadi za kujitegemea na kushirikiana na wanafunzi wenzake, na kumjengea
mwanafunzi stadi muhimu za karne ya 21 kama vile uwezo mkubwa wa kupambanua,
kufikiri, kutatua changamoto na stadi za uvumbuzi.
Faida nyingine ni pamoja na kukuza uwezo wa mwanafunzi wa
kujiamini, kuwafanya wanafunzi kupenda kujifunza, kukuza stadi za kusoma
(vitabu, majarida n.k), kumjengea mwanafunzi stadi ya ujifunzaji endelevu,
nikizitaja kwa uchache.
Ufundishaji wa namna hii siyo tu una manufaa kwa wanafunzi,
bali hata kwa mwalimu. Uzoefu wangu mdogo wa kutumia njia hii ya
kujifunzia unanionesha kuwa, ikiwa
mwalimu atajiandaa vyema, ufundishaji huu huleta hamasa kubwa ya kusimamia
ujifunzaji.
Kulingana na maandalizi niliyokuwa ninayafanya, nilijikuta
nikitamani muda wa kuingia darasani ufike ili nisimamie ujifunzaji unaoongozwa
na falsafa ya kuwashirikisha wanafunzi kwenye ujifunzaji wao. Ewe mwalimu au
mwezeshaji yeyote, tumia njia hii leo na utakubaliana na hili nisemalo.
Wajibu wa Mwalimu na
Mwanafunzi
Kabla ya kurasimisha ufundishaji/ ujifunzaji unaowazingatia
wanafunzi, mitaala iliyokuwa inatumika shule za msingi hadi vyuo vya ualimu,
ilikuwa ni ile inayomtambua mwalimu kuwa ni chanzo pekee cha maarifa. Katika
mazingira haya, mwanafunzi alichukuliwa kama stoo ya kuhifadhia maarifa.
Wajibu wa mwanafunzi ulikuwa ni kusikiliza anachoambiwa
kisha anafanya kila juhudi ya kukihifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadae. Mara
nyingi mwanafunzi amekuwa akipimwa uwezo wake wa kukumbuka maarifa aliyopaswa
kuyahifadhi. Hali hii imepelekea, mfumo wa pekee wa kujifunza kwa wanafunzi
kuwa ni wa kukariri. Hata hvyo, pamoja na Tanzania kubadili mitaala, hali ya ufundishaji imeendelea kuwa ile ile. Mwalimu ndiye chanzo cha maarifa na mwanafunzi anabaki kuwa msikilizaji.
Hali inapaswa kuwa tofauti kwenye ufundishaji
unaomzingatia mwanafunzi. Mwalimu ana wajibu wa kumsadia mwanafunzi kujifunza
yeye mwenyewe. Hivyo basi, jukumu kuu la kwanza kabisa la mwalimu ni kuwaelekeza
wanafunzi namna ya kujifunza (learn to learn).
Kuwasaidia wanafunzi kujifunza namna ya kujifunza ni wajibu wa msingi wa
mwalimu. Wanafunzi wanapaswa kufahamu njia bora za wao kujifunza. Stadi hii
inawapa uwezo wa kujisimia wakati wa ujifunzaji wao sambamba na kujitathmini ili kujua
mwenendo wao wa ujifunzaji. Kujua namna ya kujifunza ni njia ya kuwaleta
wanafunzi karibu zaidi na ujifunzaji wao na hivyo kujiona wanawajibika moja kwa
moja.
Kujua namna ya kujifunza huweza pia kuwa fursa ya wanafunzi kuyafahamu
mazingira yao ya kujifunzia na kuyageuza kuwa fursa kuliko laana inayokwamisha
maendeleo yao kitaaluma.
Wajibu wa pili wa mwalimu ni kuwaongoza mwanafunzi kuandaa
maswali yenye mantiki yanayoendana na mtaala na kile wanachopaswa kujifunza.
Katika kuhakikisha wanafunzi wanaweza kujiandalia maswali yatakayowalazimisha
kuyapatia majibu, nafasi ya mwalimu ni ya muhimu sana katika hatua hii.
Angalau, uzoefu wangu unaonesha kuwa, moja ya mbinu nzuri ya
mwalimu ni kuwa na utangulizi chokonozi. Wakati fulani nilipokuwa
ninafundisha walimu wanafunzi mada ya kupanua Bainomio (Binomial Expansion), nilianza kwa kuwapa
maswali rahisi ya kutanua
, nikawa ninaongeza kipeo, cha tatu, cha
nne, hadi cha tano. Upanuzi unakuwa mgumu kwa kadiri kipeo kinavyozidi
kuongezeka.
Wanafunzi walipofika kipeo cha tano na
sita, kazi ikawa ngumu zaidi, nikawauliza wafikirie ikiwa watakutana na
changamoto ya kupanua bainomio kama ya kipeo cha 10.
Baadhi ya wanafunzi walitoa uzoefu wao wa namna ya kushughulikia kipeo
kikubwa kama cha 10.
Niliwauliza wanafunzi ikiwa walikuwa
tayari kujifunza namna ya kupanua bainomio zenye vipeo vikubwa. Walionesha
kuwa tayari kujifunza. Niliwauliza pia, kwenye mada hii ni mambo yapi walipenda
kuyajifunza.
Katika hatua hii, wanafunzi walitarajia,
kama kawaida, nianze kuwaelezea namna ambavyo wangeweza kupanua bainomio.
Kinyume chake, niliwapatia nyenzo ambazo niliamini zingewasaidia
kujifunza namna ya kupanua binomio yoyote ile sambamba na dondoo ambazo zingewaongoza kujifunza. Na huu ndio
wajibu wa tatu wa mwalimu. Kuwapatia wanafunzi vitendea kazi vitakavyowasaidia kujifunza.
Katika kuwasaidia wanafunzi kutumia
nyenzo za ujifunzaji, kuna mambo mawili ya kufahamu. Moja ni kuamua ikiwa
mwalimu atawapa wanafunzi dondoo ambazo zitawaongoza kutafuta majibu ya maswali
yao. Namna nyingine ni ya kuwaacha watafute maarifa kwa wigo wao wenyewe hadi
watakapoona wana taarifa za kutosha kujibu maswali yao.
Kila namna inategemea na aina ya
wanafunzi na urahisi wa upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia. Watoto
wadodo kama vile wa shule za msingi wanaweza kuelekezwa nini watafute. Wanafunzi
wa shule za sekondari na kuendelea wanaweza kupewa uhuru wa kutafuta taarifa,
kuzijifunza na kisha kuzitumia kujibia maswali yao ya kiudadisi. Mwalimu mgeni wa njia hii ya ufundishaji, ni vyema akatumia mfumo wa kuwapa
wanafunzi dondoo.
Wajibu wa tatu wa mwalimu ni kuandaa
nyenzo watakazozitumia wanafunzi kujifunzia. Upatikanaji wa nyenzo za
kujifunzia mashuleni umetajwa kwenye tafiti nyingi za Ufundishaji unanaowazingatia wanafunzi kuwa ni tatizo kubwa nchini
Tanzania.
Lakini, tujiulize, mwalimu anatumia nini
wakati wa kujiandaa kwenda darasani kufundisha?
Mwalimu anajua wajibu wake ni kusoma kwa
kina ili ayafahamu vyema yale anayopaswa kuyafundisha. Ni kweli, kujua vyema maudhui yanayopaswa kujifunzwa na wanafunzi ni muhimu.
Swali la kujiuliza ni kama walimu huwa wanajiuliza ni kwa namna gani watafikisha kwa wanafunzi nyenzo hiyo ya kujifunzia wanayoitumia wao. Ukweli ni kuwa, wengi wetu hatufikiri hivi. Tunachoona kuwa ni wajibu wetu ni sisi kujifunza na kisha kwenda darasani kutoa taarifa ya ujifunzaji wetu.
Katika mfumo wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi, moja ya wajibu
wa msingi wa mwalimu ni kuandaa nyenzo kwa ajili ya wanafunzi kuzitumia kujenga
uelewa wao. Hata hivyo, miongoni mwa walimu wengi, huu ni wajibu wa msingi
sana unaopuuzwa. tusipolitambua hili, wimbo wa kukosekana kwa nyenzo za wanafunzi kujifunzia litaendelea kuwa tatizo kubwa.
Kwa kuwa hatufanyi hivi, hata kwa kitabu kimoja kilichopo shuleni, ni vigumu sana kutambua uhalisia wa upungufu wa nyenzo hizo.
Kama sehemu ya maandalizi, mwalimu anapaswa kutumia muda wake mwingi kupitia,
kutathmini na kukusanya nyenzo ambazo wanafunzi watazitumia kujifunzia. Kama sehemu ya wajibu wake, wamwalimu anapaswa kutafakari na kubuni
njia ambazo mwalimu atazitumia kuwasilisha nyenzo hizo darasani. Katika hatua hii, ni muhimu
kutambua umuhimu wa TEHAMA kwenye kurahisisha kuwasilisha
nyenzo za ujifunzaji madarasani.
Kipengele
hiki ni cha muhimu sana. Kwa hali ilivyo sasa, ninaweza kusema kuwa, walimu
wengi wamekuwa wakijifundisha wenyewe madarasani. Wanakuja na taarifa zao
walizozikusanya wakati wa kile wanachokiita maandalizi ya kufundisha.
Kimsingi, darasani hakuna kinachoendelea
zaidi ya mwalimu kufanya mazoezi ya kukumbuka na kurejea yale aliyokuwa
anayasoma wakati akijiandaa kwenda kufundisha. Hii ni kusema kuwa, mara nyingi mwalimu huwa anajifundisha mwenyewe: Mtazamo unaoshabihiana vyema na ule msemo kuwa, anayefundisha ndiye anayejifunza zaidi. mtazamo huu, unarejea sawia aina ya ufundishaji ambao mwalimu ndiye chanzo kikuu cha maarifa.
Mwalimu anapaswa kutumia muda
wake mwingi kutafuta nyenzo kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia na kuwaza na
kubuni namna ya kuziwasilisha nyenzo hizo madarasani. Wanafunzi nao, wanapaswa kuwa na mtazamo wanahitaji zaidi nyenzo za kujifunzia na mtu (mwalimu) wa kuwaongoza na kuwasaidia kutumia nyenzo hizo kwa ufanisi.
Wajibu wa mwisho wa mwalimu, lakini siyo
wa mwisho kwa umuhimu ni kuwa na uwezo usio na mashaka wa maudhui wanayopaswa
kujifunza walengwa. Ikumbukwe kuwa, baada ya wanafunzi kufanya utafiti wao,
watawasilisha yale waliyojifunza. Wanafunzi wanaweza kuwa na muda wa
kujadiliana. Hapa kunaweza kutokea mawazo kinzani kulingana na vyanzo na uelewa wa
awali wa wanafunzi. Ni wajibu wa mwalimu kuongoza wanafunzi kujifunza mambo
sahihi na hivyo hana budi kuwa na weledi wa kutosha wa maudhui hayo.
Madarasa yanapaswa kuwa karakana za
wanafunzi za kujijengea stadi na maarifa mapya. Ifahamike pia kuwa, madarasa ya karne ya 21 siyo
lazima yawe kuta nne zenye viti, meza na ubao. Kwa kasi ya ukuaji wa TEHAMA,
ujifunzaji unaweza kufanyika popote na kwa wakati wowote.
Pamoja na changamoto zilizopo, zikiwemo za upatikanaji wa nyenzo kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia, walimu hawana budi kuanza kutumia rasilimali chache zilizopo. Utayari huu ni mwanzo wa kuonesha kwa vitendo upungufu uliopo. Kusema kuwa nyenzo za kufundishia hazitoshi, ilihali chache zilizopo hazitumiki, si namna nzuri ya ushawishi. tusisubiri kibaba kijae, tutumie kidogo kilichopo, tutaongezewa kwa kuwa tunaonesha tuna uhitaji.
Comments