Mbinu za Kusaidia Kujenga Utamaduni wa Ufundishaji wa Kiudadisi Mashuleni
Picha kutoka tovuti ya Linkedin
Moja ya changamoto zinazokwamisha matumizi ya ufundishaji wa
kiudadisi mashuleni ni hali ya utayari wa walimu, wakuu wa shule, viongozi wa
kisiasa na wadau wengine wa elimu.
Changamoto kadhaa zinatajwa kukwamisha utekelezaji wa ufundishaji na ujifunzaji huu. Baadhi zikiwemo uhaba wa nyenzo za kujifunzia na walimu kukosa maarifa ya namna ya kutumia njia za ufundishaji zainazoendana na matakwa ya mfumo huu.
Hata hivyo, katikaki ya changamoto hizi, bado utekelezaji wa ufundishaji na ujifunzaji huu unawezekana. Utayari wa wadau wa elimu ndio chachu pekee ya kufanikisha hili. Palipo na utayari, changamoto kama hizi huweza kuonwa kama fursa na kuzifanyia kazi na hatimaye kufanikisha utekelezaji wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi.
Ni heri mwalimu wa darasa la wanafunzi 50 aliye
na kitabu kimoja na nia thabiti ya kutafuta namna ya kuwapa wanafunzi kitabu
hicho wajifunzie, kuliko mwalimu wa darasa kama hilo aliye na vitabu kumi
anayelalamikia upungufu wa vitabu kiasi kwamba asione hata umuhimu wa kuwapatia
wanafunzi vitabu hivyo ambavyo yeye anaviona ni vichache.
maneno hapa juu yana maana moja kubwa. Utayari wa kufanya jambo ni
nguvu inayoweza kukutengenezea njia ya kufanya mambo ambayo wengi huweza
kuyaona yasiyowezekana. Nia ya dhati ya utekelezaji wake huweza kujengwa na wadau
wenyewe wa elimu. Walimu, viongozi wa shule, wanafunzi, wazazi n.k. Katika
Makala haya, mandishi analenga kujadili namna anuai za kusaidia kukuza
utamaduni wa matumizi ya ufundishaji wa kiudadisi mashuleni.
Kujifunza na
kuukubali mfumo huu kama muongozo wa utoaji elimu
Maisha ya jamii fulani huongozwa na misingi ambayo kila
mwanajamii anaifahamu na anajua umuhimu wa kuifuata. Mfano mzuri ni imani. Ili
uitwe mfuasi wa Imani fulani, ni sharti uwe unaifahamu na kuitekeleza misingi
ya imani hiyo.
Hali kadhalika, ikiwa shule inahitaji kuutumia mfumo huu,
haina budi kuukubali kama msingi wa kusimamia na kuongoza utoaji wa elimu
shuleni hapo. Kuukubali ni pamoja na kuuelewa vyema na kuweka mikakati thabiti
ya namna ya kutekeleza.
Ni wajibu wa wasimamizi wa shule kuweka mikakati mahususi ya kupata maarifa ya utekelezaji wa ufundishaji wa kiudadisi unaoweza kufanyika kupitia mafunzo kabilishi kwa kuwasiliana na wataalam. Pia, mwalimu mmoja mmoja anaweza kupanua uelewa wake kupitia tovuti mbalimbali mitandaoni zilizo na maarifa yanayohusiana na ufundishaji wa kiudadisi.
Ikumbukwe, yote haya yanawezekana palipo na utayari wa dhati usiobabaishwa na kukatishwa tamaa na changamoto za hapa na pale.
Wasimamizi wa shule
kuwa na maono juu ya Ufundishaji wa Kiudadisi
Wasimamizi wa shule ni watu muhimu sana wa kufanikisha
utekelezaji wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi. Wana mchango mkubwa kuhusu
upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia, rasilimali watu, fedha na motisha nyingine
kwa walimu.
Wasimamizi wa shule wana mchango mkubwa wa kiushawishi kwa
watu wa chini yao. Hivyo, wanapaswa kuwa na maono ya mbali sana kuhusu namna
wanavyoweza kufanikisha matumizi ya mchakato wa ujifunzaji wa kiudadisi.
Wanapaswa kuwa na mipango thabiti na endelevu. Maono yatasaidia
watekelezaji wa chini kuyasimamia kwa kuweka mipango thabiti ya
utekelezaji.
Uwepo wa
Wahamasishaji wakuu
Ni jambo la kawaida kabisa, wakati fulani pamoja na kuamua
jambo kwa pamoja, kuna wakati hufika watu wakakata tamaa na kuona mambo
hayawezekani. Ili kufanikisha hazma ya kutumia mfumo wa ufundishaji wa
kiudadisi, inashauriwa kuwepo na watu walio na utayari thabiti.
Watu hawa watasaidia kutoa hamasa, kuonesha njia ili
kuhakikisha hakuna kikwazo katika utekelezaji. Hata pale vikwazo vinapotokea,
viweze kubadilishwa na kuwa fursa na hivyo kuendeleza utamaduni wa ufundishaji
wa kiudadisi.
Kutokukatishwa tamaa
na Changamoto wakati wa utekelezaji
Hili ni jambo la muhimu sana. Miongoni mwa changamoto
zinazosemwa kukwamisha utekelezaji wa
ufundishaji unaowazingatia wanafunzi ni kukosekana kwa hamasa miongoni mwa
walimu. Hamasa zinazokosekana ni pamoja na mshahara mdogo, mazingira magumu ya
kazi, pamoja na upungufu wa nyenzo za kujifunzia. Katika hali hii, kuna swali la
kiufahamu linapswa kupatiwa majibu.
Ikiwa walimu wanakosa hamasa, kwa nini wasiache kabisa
kufundisha mashuleni na wakafanye mambo mengine yatakayowapa hamasa?
Hili si swali la dhihaka. Ninachopenda kukisisitiza hapa ni
kuwa, kwa kuwa walimu wanaendelea kufundisha mashuleni, ni fursa yao adhimu
kufikiri na kubuni namna ya kutumia mfumo huu wa ufundishaji.
Kimsingi, hakuna wanachopoteza. pengine wanaopotea ni wanafunzi wanaofundishwa ka njia za kukariri maarifa na ambayo hayatawafaa sana maishani. Kukabiliana na changamoto ndio namna pekee ya kusonga
mbele na kuhakikisha mfumo huu unafanikiwa.
Nirudie tena kusisitiza kuwa, ni heri sana kwa mwalimu yule aliye na kitabu kimoja lakini
ana nia ya dhati kabisa na anahaha kutafuta namna ya kufanya kitabu kile
kimfikie kila mwanafunzi kuliko mwalimu aliye na vitabu kumi na hata asiweze
kuwapatia wanafunzi wakavitumia. walimu wakisubiri wapate vitabu vitakavyomtosha kila mwanafunzi. Kwa hakika, tutasubiri milele.
Uaminifu miongoni mwa
watekelezaji
Uaminifu wakati wa utekelezaji wa mchakato wa ufundishaji wa
kiudadisi ni muhimu. Inapotokea baadhi ya watekelezaji kuwa na mawazo kinzani,
ni dhahiri watu hawa watafanya kila hila kukwamisha utekelezaji. Uaminifu baina
ya watekelezaji husaidia kuweka mipango ya pamoja, kutumia rasilimali vizuri na
kuwa na mwisho unaofanana.
Ushirikiano
Moja ya nyenzo muhimu ya kufanikisha ujifunzaji wa kiudadisi
ni ushirikiano. Ushirikiano unaweza kuwa wa aina na ngazi tofauti. Ushirikiano
baina ya wasimamizi wa shule/ elimu na watekelezaji wengine, ushirikiano baina
ya walimu wa masomo na ushirikiano baina ya walimu na wanafunzi.
Katika ngazi ya ufundishaji madarasani, inapendeza sana
walimu wa somo husika wakashirikiana. Ushirikiano unaweza kuanza wakati wa
maandalizi. Maandalizi haya ni pamoja na kujenga uelewa wa pamoja sambamba na
kupanga namna ya kufanikisha somo. Pamoja na maandalizi haya, walimu wanapaswa
kutafakari njia bora watakazozitumia kuwapatia wanafunzi nyenzo za ujifunzaji.
Ikumbukwe kuwa, wajibu wa mwalimu ni kusimamia ujifunzaji wa
mwanafunzi. Usimamizi huu ni pamoja na kuhakikisha mwanafunzi anajifunza yale
yaliyokusudiwa kwake kwa kupatiwa nyenzo sahihi zitakazofanikisha azma ya
ujifunzaji wake.
Kuhakikisha Nyenzo za
ujifunzaji zinapatikana
Jukumu la kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatika mashuleni
ni la kila mmoja kwa nafasi yake. Wasimamizi wa shule wana mchango mkubwa
katika hili. Maadam msimamizi amekuwa na utayari na nia ya dhati,
atahakikisha nyenzo stahiki
zinapatikana, hata kama ni kwa awamu.
Wajibu huu pia, wanao walimu, wazazi, wanafunzi na wadau
wote wa elimu. Kinachoongoza mafanikio ni utayari na nia. Mambo mengine kama
nyenzo za ujifunzaji zitapatikana palipo na nia. Wakati mwingine hata hizo
zinazoonekana hazitoshi zinaweza kutosheleza.
Mahitaji ya nyenzo za kujifunzia,
hata hivyo yanategemea na mpangilio wa somo wa mwalimu husika. Si kila mwalimu
anahitaji mahitaji yanayofanana.
Upatikanaji wa nyenzo za ufundishaji imekuwa ni moja ya
changamoto kuu inayotajwa kukwamisha kufanikisha ujifunzaji wa kiudadisi. Hata
hivyo, ikiwa walimu hawataanza kutumia nyenzo chache zilizopo, ni vigumu sana
wadau wengine wa elimu kuona umuhimu wa kusaidia kupatikana kwa nyenzo
zinazohitajika.
Kila shule inaweza kuwa na mahitaji yake. Hivyo, ni muhimu pia,
kila shule iweke mikakati ya kutekeleza ufundishaji huu kwa kutumia rasilimali
chache zilizopo.
Wazoefu wa utumiaji wa ufundishaji wa kiudadisi wanashauri
walimu wajaribu kutumia rasilimali zinazoendana na mazingira yao. TEHAMA inaonekana ni kiungo muhimu katika kufanikisha ufundishaji wa kiudadisi.
Hata hivyo, shule nyingi za Tanzania bado hazijakuwa na miundombinu rafiki.
Pamoja na hali hii, walimu wanashauriwa kutumia rasilimali zilizopo bila kujali
uchache wake.
Watekelezaji kuwa huru kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili
Hili ni jambo la muhimu, tena ndio kiini cha ufundishaji na
ujifunzaji wa kiudadisi. Walimu wapewe fursa ya kutatua changamoto
zinazowakabili pale inapowezekana. Mawazo yao yatambuliwe na
yafanyiwe kazi. Hali kadhalika kwa wanafunzi, kwa kuwa wao ndio kiini cha
ujifunzaji wao, wanapaswa kuwa pia sehemu ya kutatua changamoto zao za
ujifunzaji.
Utaratibu huu unawakuzia wanafunzi stadi za kiuvumbuzi na kuweza kutatua changamoto mbalimbali. Hii ni
sehemu muhimu inayowajengea uwezo wa kujisimamia kwenye ujifunzaji wao. Katika
kujifunza, matatizo yao ni kiu ya kutaka kujifunza. Ili kukidhi kiu hii, ni
lazima watafute mbinu, wafanye utafiti, wahoji, wahojiane, ili wajenge uelewa
unaotakiwa.
Mwisho, ni rai yangu kwa wadau wote wa elimu, tuone umuhimu
wa kutumia njia hizi za kuwaleta wanafunzi kwenye ujifunzaji wao. Walimu
kuendelea kuwa chanzo kikuu cha maarifa kwa wanafunzi ni mfumo usio na tija
yoyote zaidi ya kuwadumaza vijana wetu. Ikiwa tunahitaji taifa la wasomi wenye
tija kwenye jamii, hatuna budi kuwekeza katika njia hizi za ufundishaji na
ujifunzaji.
Tusitegemee kijana asiyeweza kutambua wajibu wake katika ujifunzaji wake akapata elimu bora na itakayomfaaa katika maisha.
Ataweza kujibu mtihani na atarudi nyumbani na elimu yake isimfae kabisa. Kuna
uwezekano mkubwa akawa changamoto badala ya kuwa msaada katika jamii.
Uwezo na utayari wa kujiajiri na kuajirika unapaswa kujengwa kupitia namna mwanafunzi anavyojifunza. Ufundishaji wa kiudadisi unamsaidia kijana kukuza stadi za kudadisi, kuhoji, kuchambua na kufikiri kwa kina, miongoni mwa stadi muhimu kwenye karne ya 21 za kusaidia kuleta mageuzi chanya ya kiuchumi, kielemu na kijamii.
Comments