Juhudi Binafsi na Ndoto ya Mafanikio: Chachu ya Ufaulu wa Wanafunzi 10 Bora Matokeo ya Kidato cha Nne 2016
Picha na Mwandishi wa Makala haya
Shule nyingi za serikali hususani za kata, zinafahamika kwa
kukosa miundombinu rafiki ya kufundishia na kujifunzia. Katika kutatua changamoto hii, zipo juhudi
kadhaa ambazo zimefanyika ikiwa ni pamoja na kuanzisha kampeni ya kuhakikisha
kila shule inakuwa na madawati ya kutosha. Hata hivyo, wakati kampeni hii
ikiendelea, kuna baadhi ya shule zimeripotiwa kupungukiwa na madarasa ya
kujifunzia.
Kwa upande mwingine, shule zinazomilikiwa na watu binafsi,
nyingi zinafahamika kuwa na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
Sambamba na hilo, shule hizi zimekuwa makini kuhakikisha wanafunzi
wanaosajiliwa ni wale wenye uwezo mzuri darasani. Hili huhakikishwa kwa
kuwachuja wanafunzi kila wanapomaliza kidato kimoja au muhula. Hii ina maana
kuwa, vijana wanaofikia kufanya mtihani wa kidato cha nne au cha pili ni wale
waliojihakikishia kufanya vizuri.
Matokeo ya kidato cha Nne kwa mwaka 2016 yaliyotangazwa
Januari 31 mwaka huu, yanaonesha shule binafsi zimefanya vizuri Zaidi kuliko
shule za serikali. Kuthibitisha hili, shule 10 bora za kwanza zote zimetoka
miongoni mwa shule binafsi. Pia, wanafunzi 10 wa kwanza wametoka katika shule
hizi.
Katika nyakati tofauti, baadhi ya vijana waliofanya vizuri
katika mtihani huu walizungumza na kuweka bayana siri ya mafanikio yao. Wengi
wetu tunaweza kuishia kusema mafanikio ya shule hizi yanatokana na ukweli kuwa
miundo mbinu ya shule hizi ni rafiki pamoja na malipo mazuri kwa walimu. Kuna zaidi
ya mambo haya. Sifa binafsi za
mwanafunzi ni miongoni mwa chachu za mafaniko yao.
Alfred Shauri ni mmoja wa wanafunzi waliopata fursa ya kuweka
bayana siri ya mafaniko yake kielimu. Huyu ndiye mwanafunzi (wa shule ya
Sekondari ya Feza Boys) aliyefanya vizuri zaidi kuliko wanafunzi wengine wote
aliofanya nao mtihani wa kidato cha Nne mwaka 2016.
Shauri anasema, pamoja na miundombinu mizuri ya kujifunzia
katika shule yake, juhudi binafsi zimechangia kufikia mafanikio aliyoyapata
katika elimu. Akinukuliwa na gazeti la Mwananchi la Februari 1 2017, Shauri
alisema;
“Licha ya Feza kuwa shule nzuri na ninayoipenda tangu nikiwa mdogo, lakini hilo halikutosha kunifanya nifaulu, zaidi ya kuweka juhudi na kuamini kuwa ninatakiwa niunge mkono juhudi za walimu kwa kusoma kwa bidi ili kufaulu”
Mbali na kuelewa kuwa alipaswa kujibidisha katika
ujifunzaji, Shauri anaonesha kutambua umuhimu wa kuwa na ndoto ya mafanikio.
Aliamini kwa kuweka juhudi atafikia ndoto yake ya kufaulu. Hatimaye ndoto
aliyoiishi, ameitimiza kwa kuwa mwanafunzi bora kabisa kwenye matokeo ya Kidato
cha Nne 2016.
Juhudi pamoja na kuwa na ndoto ya mafanikio zimetajwa pia
na wanafunzi wenngine kama sehemu ya mambo yaliyochangia kufaulu kwao. Cynthia
Mchechu ni mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili kutoka shule ya sekondari ya St
Francis ya Mbeya. Mwanafunzi huyu anajivunia kutimiza ndoto yake ya kufaulu
vizuri katika masomo yake. Hata hivyo, Cynthia aliweka bayana kuwa, njia pekee
ya kufanikisha ndoto yake imekuwa ni kufanyia kazi alichokiamini (ndoto yake ya
mafanikio) na hatimaye ikawa kweli.
Kuwa na ndoto ya kuifikia si jambo geni linapokuja suala la
mafanikio. Hii ni mbinu inayotajwa kuwa mhimili na kiini cha mafanikio ya kila
anayehitaji kufanikiwa. Mifano ipo mingi sana. kuthibitisha hili, mwandishi wa
Kitabu cha "It only Takes A Minute to
Change Your Life" Willie Jolley anasisitiza umuhimu wa kuwa na
ndoto ya kuifikia, kuiamini na kuitekeleza. Katika kitabu chake, anatoa mifano
ya watu wengi sana waliofanikiwa kuweka ndoto zao na kuzifikia, na sasa wana
mafaniko ya kupigiwa mfano.
Uwezo wa kujituma kwa bidii ni tabia inayoongozwa kwa kiasi
kikubwa na ndoto ya mafaniko aliyonayo mtu. Kujituma ni kiashiria cha kuikubali
ndoto yako, kuiamini na kuifanya kuwa kweli.
Wanafunzi wetu wana ndoto wanazoziamini na wanazohitaji
kuzitimiza? Ndoto zao zitatimia kwa kukaa darasani bila kufanya lolote
wakimsikiliza mwalimu anavyotoa taarifa ya aliyoyajifunza?Walimu wanawasadia wanafunzi kuwa na ndoto,
kuzikubali na kisha kuzifanya kuwa kweli?.
Dhana ya kujituma kwa bidii kama msingi wa mafanikio haitawezekana
kwa wanafunzi walio na mtazamo wa kukaa darasani na kusikiliza mawaidha kutoka
kwa mwalimu. Kwa aina hii ya ujifunzaji,
si rahisi kupata wanafunzi wanaoweza kupata ndoto watakazoziamini, kuzikubali
na kuzifanya zikawa kweli.
Tusibaki tunalaumu mazingira magumu ya ufundishaji na
ujifunzaji. Ikiwa walimu wanaweza kupata mahali pa kujifunzia na kupata maarifa
ya kwenda kuwasilisha darasani, ninaamini inawezekana vyanzo hivi vikasogezwa
kwa wanafunzi ili wajitafutie maarifa wao wenyewe chini ya muongozo wa mwalimu
wao.
Akina Shauri na wenzake hawakuridhika na mazingira bora ya
shule zao, walitambua umuhimu wa kujituma kukamilisha ndoto zao walizozikubali
na kuziamini. Vivyo hivyo, wanafunzi mnaosoma shule za kata, msikatishwe tamaa
na mazingira ya shule, weka juhudi, ipate ndoto yako, ikubali, iamini na ifanye
iwe kweli kwa kuweka juhudi.
Kwa mwanafunzi, juhudi ya kwanza kabisa ni kushiriki
kikamilifu kwenye ujifunzaji wako. Shiriki kujifunza kwa bidii yale unayopaswa
kujifunza. Si utaratibu mzuri kwa mwalimu kujifunza na kisha kuleta darasani
yale aliyojifunza na kuyawasilisha kwa wanafunzi.
Wanafunzi jifunzeni kujifunza. Walimu mna kila wajibu ya
kuacha utamaduni wa kuwasilisha yale mnayojifunza kwa wanafunzi. Badala yake,
waongozeni wanafunzi wajifunze yale wanayopaswa kujifunza. Tutafute namna
tunavyoweza kuwapatia vyonzo vya maarifa mnavyovitumia ninyi kujifunzia.
Shukrani kwa ukuaji wa TEHAMA, hii ni moja ya nyenzo muhimu ya kufanikisha
hili.
Tumieni ufundishaji wa Kiudadisi unaomtaka mwanafunzi
kujifunza kwa kuweka juhudi ya kupata maarifa kwa kuuliza maswali, kuchunguza,
kudadisi, kuwa mbunifu n.k. Hii ni hatua ya awali kabisa ikiwa tuna nia ya
dhati ya kuboresha elimu Tanzania. Angalao wanafunzi wabadili fikra zao kuhusu
namna wanavyopaswa kujifunza. Uhitaji wa kitu ndio chanzo na chachu ya juhudi
ya kukipata kitu hicho.
Ikiwa tunahitaji wanafunzi wa kaliba ya akina Alfred shauri
au Cyntia Mchechu na wengine, basi tuhimize ujifunzaji unaochochea wanafunzi
kujituma, kuwa wabunifu na wadadisi. Tuungane pamoja kuhakikisha wawezeshaji
wetu wanabadilika na kutumia "INquiry Based Learning Approach"
wakati wa kufundishia na kujifunzia.
Comments