Uwezo wa Kujiajiri na Kuajirika Una Uhusiano na Namna za Ujifunzaji: Wanafunzi Wanahitaji Ujifunzaji Unaochochea Udadisi.
Picha Kutoka kwenye Video ya Wanafunzi wa Shule Wildwood IB World Magnet wakitumia mfumo wa ujifunzaji wa Udadisi. Video hii unaweza kuitazama hapa.
Kati mwaka 2005 hadi
2007, Tanzania ilibadili mitaala kutoka kwenye mtazamo wa Mwalimu kama chanzo cha
maarifa hadi ile ya Mwanafunzi kama kiichi na chanzo cha ujifunzaji wake.
Mabadiliko haya yalihusisha shule za msingi, sekondari na Vyuo vya Ualimu.
Mabadiliko ya mitaala yalilenga
kuandaa wahitimu watakaoweza kukabiliana na soko la ajira, kuweza kujiajiri,
kuajirika, kuendana kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kukabiliana na kutatua
changamoto zinazokabili jamii zinazowazunguka. Kwa bahati mbaya sana, haijakuwa
wazi kama kumekuwa na mabadiliko yoyote ya mitaala kwenye elimu ya Juu. Pengine
hali hii inaweza kuchangiwa na ukweli kuwa, mitaala ya vyuo vikuu bado haijaunganishwa
pamoja.
Hata hivyo, Tafiti nyingi zilizofanyika
nchini Tanzania, zinaonesha kuwa, mitaala hiyo haijaweza kutekelezeka kwa
kiwango kilichokusudiwa. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa, walimu hawana uelwa wa
kutosha wa mitaala hii. Upungufu wa uelewa unaelezwa haswa upo kwenye namna wanavyopaswa kuitafsiri mitaala hii. Changamoto kubwa nyingine ni uhaba wa rasilimali watu na vitu kama vile vitabu vya kutosha, samani na madarasa.
Aina ya ufundishaji unaotumiwa kwa
sasa nchini Tanzania, hususani kwa shule nyingi za serikali, ni ule wa mwalimu
kufaulisha maarifa kwa wanafunzi. Ujifunzaji ni ule wa kukariri na upimaji wa
mwanafunzi ni ule wa kuangalia ni kwa kiasi gani mwanfunzi anakumbuka yale
aliyojifunza. Mwanafunzi anapewa nafasi ndogo sana ya kushiriki kwenye
ujifunzaji wake mwenyewe.
Madarasa yamekuwa kama vyumba vya
mahubiri. Mwalimu anaingia darasani, anaeleza kile kilichomleta. Akimaliza,
anaondoka, anakuja mwalimu mwingine, naye anafanya vivyo hivyo. Wakati wote,
wanafunzi wanakuwa wamekaa, wanamsikiliza mwalimu, wanachukua nukuu.
Wasipoulizwa maswali, wao ni nadra sana kuuliza. Uzoefu unaonesha, wanafunzi hawapendi
hata kuuliza maswali.
Katika hali hii, ni ukweli usio na
shaka kuwa, mfumo huu haumuandai mwanafunzi
kuwa mbunifu, mvumbuzi wala mdadisi. Ni vigumu sana kutegemea mwanafunzi wa
aina hii kuleta ushindani unaokusudiwa kwenye soko la ajira, kutatua changamono
zake na za jamii, kuendana na mahitaji yanayokuwa kwa kasi ya kiteknolojia na
kiuchumi. Tusitegemee kamwe vijana wa aina hii wawe na mtazamo wa kujiajiri na
kutengeneza ajira.
Ni ukweli usiopingika kuwa, leo kuna
ajira nyingi sana ambazo ziliandaliwa miaka mingi iliyopita na watu
waliojipambanua kuwa ni wabunifu, wadadisi, wanaojituma na wenye uwezo wa
kufikiri kwa kina. Chukulia mfano wa mitandao ya kijamii kama vile Twitter na
Facebook ilivyoshika kasi miaka ya hivi karibuni. Watu wanaajiriwa kufanya kazi
kama wasimamizi wa mitandao hii, watu wanafanya biashara kupitia mitandao,
wanajifunza, wanawasiliana kwa urahisi na kwa haraka. Haya yote ni matokeo ya
watu wanaojituma. Wanaothubutu wao wenyewe kufanya mambo yaliyo na jita kwao na
kwa jamii.
Wanafunzi wetu tunawaandaa kuwa sehemu
ya mabadiliko yatakayoibadilisha Dunia kwa namna chanya? Watu wanaofanikiwa na
waliofanikiwa wana tabia ya kujituma bila kukata tamaa. Kama wanafunzi wetu ni
wa aina ya kukaa na kuhubiriwa tu, sifa hii muhimu wanafunzi wetu watajifunza
lini?
Ni dhahiri kuwa, tunahitaji kuweka
kipau mbele kwenye aina ya elimu inayomjengea mwanafunzi utamaduni wa
kujibidisha kwenye ujifunzaji wake. Wanafunzi wahame kutoka kwenye mfumo wa
ufundishaji unaowafanya kuwa waumini wanaosikiliza mahubiri katika nyumba za
ibada. Mfumo unaowafanya wanafunzi kujiona wanahusika moja kwa moja kwenye
ujifunzaji wao. Wawaone walimu wao kuwa ni wawezeshaji tu.
Tunahitaji mfumo unaojenga utamaduni
wa kujituma, kujitafutia, kuwa mdadisi, kuvumbua, kuibua mambo mapya na
kufikiri kwa kina na kwa tija. Hakuna shaka kabisa kuwa, wanafunzi wa aina hii,
wataweza kujiajiri, wataajirika na watatumia maarifa yao vizuri katika
mazingira ya kazi na kwenye ulimwengu unaobadilika kwa mambo mengi kila uchao.
Ikiwa tunahitaji kuandaa wanafunzi wanafunzi
wa kaliba hii, tunahitaji aina ya ufunsihaji unaofahamika kwa lugha ya
Kiingereza kama Inquiry-Based Learning.
Sina hakika kama nitakuwa nimetafsiri kwa usahihi wake, ila, kwa Kiswahili, katika Makala haya, na nyingine
zitakazofuata, ninauita mfumo huu kuwa ni
Ujifunzaji wa Kiudadisi.
Kuna ushahidi mkubwa wa tafiti
unaoonesha kuwa, mfumo huu wa ufundishaji umefaulu kwa asilimia kubwa sana.
Kupitia mfumo huu, wanafunzi wanajisikia kuwa sehemu ya ujifunzaji wao wenyewe.
Wanapata fursa ya kutatua changamoto hai za jamii wakiwa wanaendelea na masomo
yao. Kwa mtazamo huu, wanafunzi wanalewa na kujenga maana pana ya ujifunzaji
wao. Hii inakuwa chachu ya kujifunza zaidi na kushiriki kwenye michakato
mbalimbali ya ujifunzaji.
Katika ufundishaji wa aina hii, mwanafunzi
hushiriki kutafuta majibu ya kile anachopaswa kujifunza. Majibu hupatikana kwa
kufanya utafiti, kuchuguza, kuchambua, kujadiliana na kuwasilisha yale waliyojifunza. Ujifunzaji huweza kufanyika kwa kusoma
vitabu, kutazama video, kutembelea maeneo mbalimbali, kuongea na wataalam
husika n.k.
Mwalimu ana wajibu wa kuwapatia
wanafunzi maeneo ya ujifunzaji, vifaa na rasilimali nyingine za kuwasaidia
wanafunzi kufikia malengo yao kulingana na namna walivyojipanga katika kutatua
changamoto inayowakabili. Mwalimu ana
wajibu wa kufanya upimaji na tathmini endelevu ambayo hulenga kufahamu
wanafunzi wamefikia wapi, wanakosa nyezo gani na kipi cha kufanya ili kuboresha
ujifunzaji wao.
Katika hali ya kawaida na kwa
mazingira yetu ya Tanzania, tunaweza kufikiri kuwa aina hii ya ufundishaji
haiwezekani. Tunapozitazama changamoto zilizopo madarasani, kama vile wingi wa
wanafunzi na ukosefu wa vifaa vya ufundishaji na ujifunzaji, tunaweza kusema
kuwa, ufunsihaji huu hauwezekani, ni mgumu, tusubiri hadi hali itakapotengamaa.
Mfumo huu unawezekana kabisa. Suala la
kwanza ni kubadili mtazamo. Walimu hawana budi kufahamu kuwa, mfumo unaotumika
kwa sasa, hauna tija na hivyo kuna ulazima wa kuwafanya wanafunzi wahusike moja
kwa moja kwenye ujifunzaji wao. Hata kama mashule yatakuwa kila aina ya nyenzo
ya ujifunzaji inayotakiwa, unaweza kushangaa kuwa hata wanafunzi ikawachukua
muda kukubali kubadilika. Hii ni kwa sababu ya mazoea na ugumu wa kubadili
mtazamo wa namna ya kufanya jambo. Tukiamua tunaweza.
Katika Makala ijayo, tutaangalia kwa
undani Zaidi ni kwa namna walimu wanavyoweza kutumia aina hii ya ufundishaji
mashuleni.
Comments