Unapenda Kutumia Vitumizi vya Android kwenye Kompyuta Yako? Mfumo Endeshi wa Remix ni Jibu Lako.
Skrinishoti kutoka Tovuti ya RemixOS
Hakuna shaka kuwa ili uifaidi simu yako vizuri, inapendeza sana ikiwa utaweza kuweka vitumizi (applications) unavyovipenda. Ni muhimu kutambua kuwa, aina na wingi wa vitumizi vizuri unavyoweza kuvitumia hutegemea na aina ya Mfumo Endeshi (Operating System) wa simu au kifaa chako. Hii ina maana kuwa, unaponunua simu, ni vyema ukafahamu ni aina gani ya Mfumo Endeshi ungependa kuutumia na ikiwa utakuwezesha kutumia vitumizi unavyovipenda.
Kwa sasa, moja ya Mfumo Endeshi pendwa kabisa wa simu ni Android. Ni dhahiri kuwa, Mfumo Endeshi huu una mkusanyiko wa vitumizi vizuri sana kwa simu. Haishangazi kuona kitumizi fulani kinapatikana kwenye Android lakini hakiwezi kutumika kwenye mazingira mengine kama vile ya Windows na mifumo endeshi mingine. Mara nyingi, kitumizi kikiweza kutumika kwenye Windows, ni vigumu sana kukikosa kwenye mfumo wa Android. Ila, kinyume chake, inawezekana kabisa.
Umekipenda kitumizi fulani cha simu na ukashindwa kukitumia kwa kuwa hakiendani na mfumo wa simu yako? Bila shaka hali kama hizi zimesha kukuta. Unaweza kuona ni kwa namna gani hali kama hizi zinavyokuwa ngumu kukubalika. Unaweza kujuta ni kwa nini ulinunua simu inayotumia mfumo endeshi fulani. Hata hivyo, tukubaliane kuwa, si rahisi kupata simu inayokidhi kila hitaji lako.
Hali kama hii imenikuta mimi. Nimeshindwa kutumia kitumizi cha simu nilichotokea kukipenda kwa kuwa mfumo endeshi wa simu yangu hauruhusu. Kwa sasa, kitumizi hiki kinaweza kutumiwa tu kwenye Mfumo Endeshi wa Android. Bahati mbaya, simu yangu inatumia mfumo wa Windows ambao hauniruhusu kutumia kitumizi hiki. Kwa namna nilivyokipenda, nililazimika kufanya utafiti mtandaoni ili kupata namna ya kuweza kukitumia kitumizi hiki katika mfumo wa windows.
Kama kawaida yangu, nisiyependa kushindwa, hususani linapokuja suala la simu na Kompyuta. Siku zote, nipo tayari kuweka rehani simu/ kompyuta yangu, alimradi nimejaribu kutatua changamoto ya kiteknolojia inayonikabili. Ikibidi kuondoa mfumo uliopo na kuweka mwingine. Katika hali kama hii, simu na Kompyuta hugeuka vifaa vya majaribio. Kwangu si tatizo ikiwa vifaa hivi vitaharibika.
Nimesoma machapisho na kuangalia video kadhaa za namna ya kuingiza vitumizi vya Android kwenye simu ya mkononi inayotumia mfumo wa Windows. Nimejifunza kuhusu Project Astoria ya Windows ya kusaidia kutumia vitumizi vya Android kwenye simu za mfumo wa windows. Hata hivyo, nimegundua kuwa, Microsoft walishasitisha mradi huu. Nimepitia maelezo kadhaa ya namna ya kuweka vitumizi vya Android katika simu zinazotumia windows. Yapo mtandaoni. Kwa bahati mbaya, sikufanikiwa kwa aina ya simu ninayoitumia. Hata hivyo, sikukata tamaa.
Nilihamia kwenye Kompyuta. Huku nimejifunza namna nyingi sana za kutumia vitumizi vya Android kwenye mfumo wa Windows. Namna hizi kwa kimombo zinaitwa "Android Emulators". Baadhi ya Emulators ni kama vile Blue Stacks ambayo bila shaka ni maarufu sana miongoni mwa watu wengi. Emulators nyingine ni kama vile Manymo, Genymotion na nyingine nyingi ambazo unaweza kuzisoma zaidi hapa.
Shukrani kwa Mradi wa Android X86. Huu ni mradi unaowawezesha watumiaji wa Android kuweka mfumo Endeshi wa Android kwenye kompyuta zao. Hii ina maana kuwa, kwa sasa, unaweza kutumia toleo la Android 6 Marshmallow kwenye Kompyuta yako. MarshMallow ni moja ya matoleo ya android ya hivi karibuni ukiachilia toleo jipya kabisa la hivi karibuni la Android 7.0 Nougat. Unaweza kuingia kwenye You Tube na kuangalia namna ya kuweka Android X86 kwenye Kompyuta yako.
Hata hivyo, kilichonishawishi zaidi kuandika makala haya, ni kukutana na namna nyingine ya kutumia vitumizi vya Android kwenye Kompyuta yako. Namna hii ni ile ya kuweka Remix OS kwenye Kompyuta kama jinsi unavyoweka Mifumo Endeshi mingine. Remix OS ni mfumo kama ilivyo mifumo ya Windows, Android, Ubuntu, Linus n.k inayokuwezesha kutumia vitumizi vya Android kwenye Kompyuta yako.
Awali, Remix OS ilifahamika kama Remix OS Player iliyokuwa na Madhumuni ya kuwasaidia wanaopenda michezo ya Android kuchezea kwenye Kompyuta zao. Kwa sasa, kwa kutumia Remix Os, unaweza kufanya chochote ambacho unaweza kukifanya kwenye mifumo mingine kama vile ya Windows, Android n.k. Vitumizi kama vile vya MS Office na PDF vipo. Unaweza kutumia mtandao wa Internet, kutumia WhatsApp, email, kusikiliza mziki na mengine mengi.
Kwa sasa, hii ndio njia muafaka zaidi ninayoiona ikiwa unapenda kutumia vitumizi vya Android kwenye Kompyuta yako. Angalau, Remix OS imekuwa suluhisho kwa hitaji langu. Bila shaka, inaweza kuwa pia njia mbadala kwako ikiwa huna simu inayotumia mfumo wa Andoid na ungependa kutumia vitumizi vya Android.
Uzuri wa Remix OS ni kuwa, si lazima uiweke (Install) kwenye "Local Disk C". Unaweza kuweka kwenye hifadhi nyingine kama "Local Disk D" na pia kwenye diski mweko (Ubs Flash disk) au kwenye kadi sakima (Memory Card) na ukaitumia pale unapoihitaji. Katika mtandao wa You tube, kuna maelekezo anuai ya namna unavyoweza kutumia Remix OS.
Habari njema ni kuwa, Mradi wa Android X86 na Remix OS wameamua kushirikiana ili kuongeza ufanisi zaidi katika miradi yao. Bila shaka, siku za usoni tunaweza kupata mambo mazuri zaidi. Kila la kheri kwa waanzilishi wa miradi hii, Jide na Huang.
Ninakutakia Mwaka Mpya Mwema wa 2017.
Comments