Ni Kukua kwa Kiswahili, Kuporomoka au ni Mwanzo wa lugha Nyingine?
Pamoja na kuwa Kiingereza ndio lugha rasmi ya kufundishia
katika shule za sekondari na vyuo vikuu, ni muda mrefu sasa kumekuwa na
mijadala ya lugha ipi kati ya hizi mbili ni muafaka katika kufundishia. Mijadala
hii inakuja kufuatia kuendelea kudorora kwa ubora wa elimu nchini Tanzania. Kuhusiana
na hili, tafiti nyingi zimeshafanyika. Lengo si kujadili tafiti hizi, wala ni
lugha ipi ni muafaka katika kufundishia wanafunzi nchini Tanzania. Hii inaonesha kuwa Tanzania tuna utata katika matumizi ya Kiswahili na Kiingereza. Utata unaohitaji suluhisho.
Watanzania tulio wengi tumekuwa na tabia ya kuchanganya
lugha ya Kiswahili na kiingereza katika kuongea. Bahati mbaya sana wengi wa
watumiaji wa mseto huu ni wasomi au
waswahili waliopata bahati ya kujua maneno machache ya kiingerezaa au ni
waongeaji wazuri wa Kiingereza.
Kwa mtazamo wangu, hili ni tatizo letu watanzania. Tena ni
tatizo la msingi kabisa. Kiswahili ni moja ya utambulisho wetu watanzania. Huu ni
utambaduni wetu. Tunapochanganya Kiswahili na kiingereza, tunaupoteza utamaduni
wetu. Tunaidharau fahari yetu.
Sentensi moja inapoundwa kwa Kiswahili na kiingereza,
sidhani kama mhusika atatambulika kuwa anaongea Kiswahili au Kiingereza. Bila shaka
hii ni lahaja mpya kabisa. Mfano wa mseto ni kama vile Leo ninataka kukutoa out, infact
utaratibu huu si mzuri, you messed up ndugu yangu, huyu
ndiye girlfriend wangu, unajua issues kama hizi hazisound
kabisa n.k . Haya ni mazoea mabaya katika matumizi ya Kiswahili.
Watanzania tunaelekea kupata lugha mpya ambayo bado
tutajinadi nayo kuwa ni Kiswahili. Sidhani
kama tutajivunia kuwa tumejenga Kiswahili. Mwisho wa siku, tutajikuta tunaongea
Kiswahili kilicho na viraka vya maneno ya Kiingereza au kilichobandikwa maneno
mengi ya Kiingereza (na lugha nyingine).
Cha kushangaza ni
kuwa, maneno mengi ya kiingereza yanayotumiwa katika sentensi za Kiswahili yana
maneno ya Kiswahili yaliyo rahisi kabisa na yaliyozoeleka. Wazungumzaji,
wataalam na wadau wengine wa lugha ya Kiswahili
wanapaswa kuliona hili na kulisemea.
Ninatambua kuwa, moja ya namna ya kukua kwa lugha, ni kukopa
maneno kutoka katika lugha nyingine. Ni dhahiri kuwa, Kiswahili ni moja ya
lugha zilizokwisha kopa maneno mengi kutoka katika lugha nyingine. Lakini,
namna watanzania tunavyochanganya lugha wakati wa kutumia kiingereza siyo namna
sahihi ya kukikuza Kiswahili.
Ni kweli kuwa watanzania huwa tunakosa maneno ya Kiswahili
hadi tuamue kutumia kiingereza au ndio ustaarabu tulioamua kuuishi? Sidhani kama
hali ndio hii, na ukweli utabaki kuwa huu ni utaratibu tunaojijengea pamoja na
kuwa tuna uwezo wa kuongea Kiswahili bila kuchanganya na Kiingereza.
Kama ni kweli huwa
inafika mahali tunakosa neno sahihi la Kiswahili, tunajibidisha kujifunza kwa kutafuta maneno
hayo sahihi ili wakati mwingine tusirudie makosa haya? Kushindwa kufanya hivi
ni moja ya dalili za kutokujitambua na tusio elewa wajibu wetu wa kukitunza na
kukikuza Kiswahili kama watumiaji wakuu barani Afrika na Duniani kote.
Swali la kujiuliza ni kuwa, katika kuzungumza, ni kweli tumejihakikishia
kuwa hakuna maneno ya Kiswahili ambayo yangeweza kusimama badala ya neno au
maneno ya Kiingereza yaliyotumiwa? Huku ni kwenda na wakati, ni kuvuta hadhira,
ni mkakati wa kukikuza Kiswahili au ni nini? Tutafakari kwa pamoja kilema hiki
kilicho miongoni mwa watanzania wa sasa na wanaoaminiwa kuwa ndio wazungumzaji
wazuri wa Kiswahili.
Comments