Nimepata nafasi; ninaitumia vizuri.

Nimepata nafasi; ninaitumia vizuri

Ni dhahiri shahiri kuwa watanzania wengi hatuna utamaduni wa kusoma vitabu. Kusoma vitabu ni tabia na wengi wetu hatuna tabia hii. Ila jambo la kutia moyo ni kuwa watu tuna uwezo wa kubadili tabia endapo tutakuwa na moyo wa kufanya hivyo. Mimi sikuwa na tabia ya kusoma vitabu, lakini nimejizoesha na sasa angalau kusoma vitabu pamoja na kuwa, kasi sio kubwa sana.

Nimepata bahati ya kuwa mwalimu wa kuwaandaa walimu wa shule za msingi. Jukumu hili ni nyeti sana pamoja na kuwa serikali ya Tanzania haitambui umuhimu wa walimu hawa wa shule za msingi. Mazingira ya kufundishia bado ni magumu yenye kukatisha tamaa kabisa. Bila shaka, ni walimu wachache sana wenye (angalao) kuridhika na mazingira ya kazi yao ya kufundisha.

Pamoja na ugumu wa kazi, lakini nimejitwika jukumu, jukumu la kuwajengea tabia na kuwakumbusha walimu watarajiwa umuhimu wa kusoma vitabu. Ninatambua nafasi waliyonayo walimu hawa wa shule za msingi katika kukabiliana na wimbi la watanzania kuwa wavivu wa kusoma vitabu. Walimu wa msingi ndio wa kuujenga msingi huu wa kuwa na watanzania wanaopenda kusoma vitabu.

Niingiapo darasani nimekuwa nikianza kipindi kwa kuwakumbusha wanafunzi wangu juu ya usomaji wa vitabu kwa kuwakumbusha wao wenyewe kujisomea vitabu ili kujijengea tabia hii njema na kisha kuiambukiza kwa wanafunzi watakaokutana nao katika shule za msingi. Wakati mwingine nimekuwa nikiwasimulia maudhui ya vitabu nilivyovisoma kama namna ya kuwafanya nao wapende kusoma vitabu kwani kwa namna moja ma nyingine, wanaweza kuvutiwa na vitabu hivyo. Nimeanza mwenyewe, lakini nitawahimiza pia na walimu wenzangu kuniunga mkono katika usisitizaji wa kusoma vitabu ikiwa ni pamoja na wao wenyewe kuwa mfano katika usomaji wa vitabu.

Ninatoa wito pia kwa waalimu katika ngazi zote, watumie fursa walizonazo kuwasisitiza wanafunzi wao kujijengea tabia ya kusoma vitabu. Wazazi na walezi, hali kadhalika, wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wana msingi mzuri na ari ya kujisomea sio tu vitabu vinavyopaswa kusomwa katika mitaala mashuleni, pia vitabu mbalimbali vyenye kupanua maarifa zaidi ya yale ya darasani.

Mbali na usomaji, lakini pia tuna jukumu kubwa la kuhimiza uandishi wa vitabu. Uhimizaji wa kuandika vitabu uwe kwa vitendo, kwa maana kuwa wenye uwezo wa kufundisha njia bora za uandishi wa vitabu, wawe pia mstari wa mbele katika uandishi. Shukrani kwa mzee Joseph Mbele na kaka Fadhy Mtanga kwa kuwa mfano. Hawa ni miongoni mwa wadau wachache ninaowatolea mfano. wanasoma na pia kuandika vitabu. Yawezekana sana watu wengi wakapenda kusoma vitabu lakini, miongoni mwao, wachache wakawa pia ni watunzi wa vitabu. Bila shaka, watunzi wote wa vitabu ni wasomaji wazuri wa vitabu, vyakwao na vya wengine.

Niseme ukweli, miongoni mwa watu walionijengea tabia ya kusoma vitabu, ni kaka Christian Bwaya. Niliwahi kumtembelea kwake na nilifurahi kuona hazina kubwa ya vitabu alivyokuwa navyo na alipata kunisimulia namna vilivyoweza kumsaidia katika harakati mbalimbali za maisha. Nilipata pia kujifunza umuhimu wa kusoma vitabu kupitia mijadala mbalimbali katika blogu anuai mtandaoni ikiwemo ya mzee Joseph Mbele ambaye ni mwalimu msomaji na mtunzi mkubwa wa vitabu. Kaka Fadhy Mtanga naye amekuwa chachu kubwa kwangu katika kunijengea tabia ya kujisomea vitabu.




Comments

Unknown said…
Hongera kaka,mimi pia nimejijengea mazoea ya kusoma na kuandika mambo mbalimbali lakini nashindwa kupublish,je unaweza kunisaidia nifanyeje?Asante

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?