Hii ni Sayansi au Imani?




Kuna mambo mengine katika hali ya kawaida, tunayatenda lakini kuyaelezea inakuwa vigumu. Tunatumia dawa na kusubiri kupona. Wengine wanatumia chakula na kusubiri wapate nguvu na kuona miili inajengeka. Maelezo ya nini kinatokea hadi haya yanafanyika, mara nyingi yanakuwa si muhimu.

Picha hapo juu, inaonesha gunzi likiwa limefungwa kwenye shina na mpapai. Madhumuni ya gunzi hili ni kuzuia mpapai usiwe dume kwa maana ya kutoa maua ambayo yatatoa mapapai yasiyo ya kawaida na ambayo hayatafaa kuliwa.Nami nilishawahi kutumia njia hii miaka fulani iliyopita. Ni kweli mipapai ilikuwa inabadilika; kutoka mipapai dume na kuwa mipapai yenye kutoa mapapai mazuri yenye kufaa kula. Mapapai dume huwa yanakuwa marefu isivyo kawaida na huwa hayafai kula.

Ninachojiuliza hapa ni kuwa, gunzi hili linafanyaje kazi? Labda hii ni Sayansi na pengine yapo maelezo ya kinachotokea. Au labda, hii ni imani. Kwa maana kuwa gunzi halina msaada wowote, kwamba kingine chochote kingeweza kufungwa na muhusika akaamini kuwa mpapai ule utabadilika na kuwa jike. Si haba pia kufikiri kuwa kama hii ni imani, basi hata matumizi ya gunzi ni sehemu ya imani hiyo. Kwamba imani haitafanya kazi kama gunzi halitahusishwa.
Binafsi nilishatumia njia hii na ikafanya kazi, lakini maelezo sina. Sijui kama ni Sayansi, au ni imani. Hebu tuwaachie wataalamu (kama mzee wa Mitiki) na wengine wote wenye ufahamu na mambo haya wapate kutuondolea dukuduku hili ili hatimaye tupate kujua kama hii ni Sayansi au ni Imani.

Comments

Duh!!!
Ni SAYANSI YA IMANI hiyo. Duh!
Anonymous said…
sawa kabisa ni sayansi ya imani hiyo

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?