Kiswahili na Kiingereza; Twazitaka lugha hizi kwa pupa, na tunazikosa zote.

Kiswahili ni lugha kuu ya mawasiliano kwa watanzania na ndio maana inatambulika pia kama lugha ya Taifa. Kiingereza ni lugha rasmi ambayo hutumika maofisini na mashuleni, hususani shule za upili hadi vyuo vikuu. Hutumika kama lugha ya kufundishia na mawasiliano mengine.

Kinyume na matarajio, sehemu ambazo kiingereza kilipaswa kutumika, maofisini na shuleni, hakitumiki ipasavyo, bali kiswahili ndicho kinachoshika hatamu.

Mbali na kutoitumia lugha ya kiingereza mashuleni na kwenye ofisi, nje ya maeneo haya hali ni hiyo hiyo, watu wanatumika kiswahili kwa uhuru wao kwani ndiyo lugha pekee ituunganishayo watanzania bila kujali sana elimu aliyonayo mtu. Wapo watanzania wachache wasiokijua kiswahili vizuri kwa sababu wamekuwa wakitumia lugha za makabila yao kiasi cha kukisahau kiswahili lakini asilimia kubwa tunakizungumza vizuri. Mashuleni, walimu wanawahimiza wanafunzi wao kutumia kiingereza hata wawapo majumbani kwao kama namna ya kuijua zaidi lugha hii. Kwa mantiki hii, kiswahili kinapewa msisitizo mdogo kwa maana kwamba hatuna haja ya kuendelea kukijifunza. Au niseme kuwa kiswahili kinapuuzwa.

Kwa bahati mbaya sana, pamoja na msisitizo wa matumizi ya kiingereza majumbani na mitaani, watu bado tumekuwa hatuitumii lugha hii ya kigeni; imebaki kutumiwa mashuleni na maofisini na watu wachache. Wapo pia baadhi ya walimu (yawezekana ni idadi kubwa) wafundishao kwa kiswahili masomo yaliyotakiwa kufundishwa kwa kiingereza.

Vuguvugu hili la namna tutumiavyo lugha hizi mbili ni janga kubwa kwetu watanzania. Kwa uvuguvugu huu, kiswahili na kiingereza zitazidi kuwa tatizo kwetu. Kiingereza kitazidi kuwa ni janga letu watanzania, na kiswahili vile vile.

Matumizi ya kiswahili na kiingereza kwa wakati mmoja yameshamiri sana hususani katika maongezi, hotuba na hata kwenye filamu za kitanzania. Ni za kiswahili lakini, kiingereza kinapachikwa pachikwa si mchezo. Sina hakika kama ni kusudio la watunzi, na kama ndivyo kwa maudhui yapi?

Ni juzi hapa Raisi wakati akitangaza baraza la mawaziri, alikuwa akiingiza maneno ya kiingereza. Japokuwa haikuwa kwa wingi, lakini alichanganya kiswahili na kiingereza. Si kiashirio kizuri, hususani kwa Raisi wa nchi pale anapoongea na wananchi ambao inajulikana wazi kuwa wapo wasiojua kiingereza. Wapo watanzania wengi wasiokijua kiingereza, waliokuwa wanafuatilia Raisi akitangaza baraza la mawaziri. Ni wazi kuwa kuna sehemu waliachwa, hasahasa wale ambao hawakuwa na mtu wa kuwapa maana ya maneno yale ya kiingereza kwa kiswahili.

Si yeye tu, kwenye vikao vya bunge, kiswahili na kiingereza vimekuwa vikisikika mara kwa mara vikitumiwa kwa wakati mmoja. Watanzania wa kawaida mitaani na majumbani, mseto huu wa lugha ni jambo la kawaida sana.

Sina hakika kama mchina wakati anaeleza jambo kwa wananchi wake kwa lugha yao, au mjerumani, au mkorea, na ikafika sehemu akaingiza kiingereza. Kama ndivyo, lugha zao wamezipa msisitizo stahiki mbali na kuwa nao pasi na shaka wanajifunza pia kiingereza. Wanazitumia lugha zao katika nyanja zote. Mtanzania aendae China kusoma, hana budi kukijua kichina kwanza, Ujerumani vile vile. Huku kwetu bongo, mwingereza anaishi hapa miaka mitano, hajajua kuongea kiswahili. Watanzania hatuna msisitizo kwa wageni kuijifunza lugha yetu.

Nimezisikiliza hotuba kadhaa za hayati Mwalimu Nyerere. Sijamsikia akichanganya lugha, yani Kiswahili na Kiingereza. Alizitambua na alikuwa na hisia sahihi na watu wake. Alikienzi kiswahili ipasavyo. Alitaka watanzania wapate ujumbe husika bila kukwazika na kubabaika.

Binafsi naona kuna haja ya kuondokana na vuguvugu hili la lugha. Tunazikosa zote, hakuna upande ambao tunaweza kuusimamia kikamilifu na kujidai nao. Wimbi la kuchanganya kiingereza na kiswahili linazidi. Litatugharimu hapo mbeleni

Harakati za katiba mpya ziambatane na mabadiliko yahamasishayo matumizi ya lugha moja ya watanzania wote. Hapa namaanisha kuwa kiswahili kipewe msisitizo na nafasi ya kutosha kujidai. Itumike mashuleni; shule za msingi hadi vyuoni. Kiingereza kibaki kama lugha muhimu ambayo kila mmoja kwa wakati wake ataona kuna umuhimu wa kuifahamu.

Ni uamuzi mgumu kulingana na hali ya Taifa letu la utegemezi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kielimu, kiutawala n.k. Watu wanaweza kufikiri kuwa muda wa mageuzi haya ya kihistoria ni bado, labda baada ya Tanzania kuwa imara kiuchumi kiasi cha kutokutegemea sana misaada. K ipindi ambacho tutakuwa tunawategemea wanasayansi wetu, kipindi ambacho tutakuwa miongoni mwa vyanzo vya teknologia mpya. Yote haya binafsi naona mwanzo wake ni mageuzi ya kihistoria ya kuthubutu kutumia Kiswahili katika nyanja zote za kimaendeleo; kuanzia elimu na shughuli zote rasmi na zisizo rasmi.

Ni uamuzi mgumu ambao utahitaji muda, gharama na uvumilivu wa watu. Lakini mimi naona kuwa tuna haja ya kufanya hivi. Tumekuwa tegemezi kwa mambo mengi, ajabu sana hadi lugha tunakuwa tegemezi!

Comments

Amos Msengi said…
Mimi naona tunashindwa kumudu lugha zote mbili kutokana na asilimia kubwa ya watanzania hawana elimu ya kutosha,wengine hata kusoma hawajui. Pia kuna hisia kuwa mtu akiongea kingereza huonekana msomi. Hii inasababisha watu wavamie lugha hiyo bila ufanisi na mwisho wa siku tunajikuta hatujui lugha zote.
Huku hatuko na huku hatuko. Inabidi tuamue moja ingawa pengine njia bora zaidi na inayofaa ni kutumie lugha zoe mbili kwa pamoja (active bilingual language policy). Kama tungeweza kukifundisha Kiingereza vizuri kiasi kwamba vijana wetu wanaoingia kidato cha kwanza wakawa wanakimudu vizuri, mimi nisingekuwa na tatizo lolote. Sera yetu ya lugha kama ilivyo kwa sasa ni mojawapo ya sera za lugha za kuchekesha sana duniani; na imegeuka kuwa chombo cha kudunisha elimu tunayowapa watoto wetu hasa wale wa sekondari ambao kimsingi tunawafundisha katika lugha wasiyoielewa halafu eti kimiujiza ujiza tu tunawategemea waweze kuzielewa "Newton's laws of motion" bila wasiwasi wo wote.

Na hapo bado hujataja ule ukweli wa kuumiza moyo kwamba kimsingi watu walioshindwa katika mitihani yao ndiyo tunawapeleka kusomea ualimu - na wengi wao Kiingereza hawakimudu vizuri!
emu-three said…
Kuna kasumba moja ya kusema `kasoma' eti kwasababu anajua kiingereza. Najiuliza huyu Mjapani, huyu Mjerumani, huyu Mchina, ambaye Kiingereza kwake sio muhimu, na mtaalamu kiwandani, ni dakitari, yeye tutamuitaje, kasoma au hakusoma!
Hapa ni vyema tukasema, `hakusoma Kiingereza' itakuwa imekaa vyema. Kama alivyo Muingereza, asiyejua Kiawahili tutamuita `hakusoma Kiswahili.
Tukirudi kwenye kuchanganya hizi lugha mbili na mtaka yote kwa pupa hukosa yote, nafikiri kosa kubwa ni letu wenyewe. Kwa mfano kama tungeamua kuwa lugha yetu ni Kiswahili, ingekuwaje, wakija wageni lazima wajifunze kiswahili, na wewe kama unataka kwenda nje, jifunze Kiingereza...swali linakuja, je vitabu vya taaluma, utavisomaje na wakati vimeandika kiingilishi?
Lugha huwakilisha utamaduni, kwa vyovyote iwavyo, kiswahili ndicho kinachomuwakilisha Mtanzania katika maswala ya lugha, sio Kingereza...ni vyema viongozi mnapokwenda nje, tayarisheni hotuba zetu kwa kiswahili, ili mwisho wa siku mataifa makubwa yahangaike kuweka `vitafsiri' vya lugha hii na baadaye iwekwe kwenye lugha za mataifa kama kijerumani, kifaransa nk. Lakini kama tutafanya hivyo, tutajulikanaje kuwa `tumesoma' na tafsiri ya kusoma kwetu ni kujua `kiingilishi'!
Albert Kissima said…
Amos, kusoma si tatizo sana. Watoto wanakiongea Kiswahili vizuri, si kwa kuwa wanakisoma shuleni, bali ndiyo lugha pekee ya kuwasiliana. Ni lazima wakijue. Angalia Kenya, Kiingereza ndio lugha kuu ya mawasiliano. Wakenya hawategemei kiingereza cha kufundishwa darasani, ni lugha kuu ya mawasiliano. Watoto wanakuwa wakiitumia.

Prof Masangu; wapo wanaoweza kukiandika kiingereza vizuri tu kulingana na taratibu zake, lakini kwenye kuongea ikawa taabu. Wapo pia wanaokiongea bila utata lakini kiingereza cha kuandika kikampiga chenga. Wapo pia wasiojua kukiandika na kukiongea. Pia, wapo wanaokiongea na kukiandika vyema (kuna uwezekano mkubwa,wengi wa hawa wamesoma au kuishi nje ya Tanzania au wanasoma kwenye Shule zenye kutumia kiingereza kama lugha ya kufundishia na kwa mawasiliano mengine, kiswahili hakiruhusiwi katika mazingira ya shule)
Makundi haya yapo Tanzania.

Watoto wanaweza kufundishwa kiingereza vizuri shuleni, lakini nje ya darasani, hawatumii walichofundishwa, mfano matumizi ya nyakati, sehemu za sentensi, n.k. Nje ya darasani, wanatumia Kiswahili. Wanachojifunza darasani, wanategemea kukitumia kwenye kujibia mitihani tu na si kujifunza na kujiimarisha katika kukitumia kiingereza kwa ufasaha wakati wa mawasiliano. Nasema hivi kwa kuwa hakitumiki kwenye mawasiliano ya kawaida nje ya kipindi cha kiingereza darasani.

Emmu3, kati ya mambo yanayokwamisha matumizi ya kiingereza ni hili wazo la kusema aongeaye kiingereza ndiye aliyesoma. Hili lipo sana akilini mwa watu.
Hili limekuwa kizingiti kikubwa kwa wale wanaotaka kukitumia kiingereza kwa kuwasiliana nje ya kipindi cha darasani cha kiingereza, au nje ya shule ama ofisi.

Watu wanaona aibu kukiongea kwa kuwa wataonekana wanajionesha kuwa wamesoma; hali hii inawapa watu woga wa kutumia kiingereza. Hili ni tatizo kubwa kwa hakika.
Watanzania tunakidharau kiswahili, wakati nchi nyingine zisizotumia kiswahili, wanakipa msisitizo mkubwa, tena kwa juhudi zao wenyewe au kupitia kwa baadhi ya watanzania wachache. Viongozi nao kuonesha wamesoma, wakienda nje ya nchi,wanapotakiwa kutoa hotuba, wanatumia Kiingereza. Hawataki kukitangaza kiswahili.

Hata Tanzania, hakuna sheria iwabanayo watu wa nchi nyingine pindi wanapokuja walazimishwe kukijifunza kiswahili, ni uamuzi wao kujifunza au kutojifunza. Kama sheria hiyo ipo, basi haitekelezwi.

Tukiamua kutumia kiswahili tu, hata zana za kufundishia madarasani, itabidi ziwe kwa kiswahili. Tukiamua tutaweza. Ndio maana niligusia kuwa, uamuzi huu utakuwa ni wa kihistoria na pia wahitaji muda kuruhusu mabadiliko kama haya ya vitabu vya kufundishia. Hapa nadhani kazi ndio kubwa.

Binafsi naamini kuwa, mapinduzi ya kweli ya maendeleo Tanzania, yataanza kuonekana pale tutakapothubutu kutumia Kiswahili katika nyanja zote za elimu, uchumi na za kijamii kama lugha pekee ya maendeleo. Uamuzi huu nauona kuwa ni kipimo cha maamuzi magumu ambayo hayakukaa kuamuliwa Tanzania. Hii itakuwa ishara ya kuanza kuwa huru katika maamuzi, ishara ya kuanza kujitegemea kielimu na kiuchumi.
Anonymous said…
真是一个好职位。我真的很喜欢阅读这些类型或文章。我可以?吨等着看别人怎么说。
emuthree said…
Haya huyu hapa kaandika Kichina, ina maana ni Mchina anaithamini lugha yake, kwahiyo ili ujue alichoandika hapa inabidi utafaute tafsiri, na hapo utakuwa umechukua juhudi ya kujifunza lugh za wenzako, ukifanya hivii mara mbili, tatu, utakuwa wapi na lugha hiyo si-itakuwa imejitangaza...mmh,naongezea tu
chib said…
Emu three.. ha ha haaa, hata mimi nilikuwa nashangaa shangaa hiyo michoro sijui ni Kikorea, kichina, kijapani au...
Albert Kissima said…
Anony ni kweli anaitangaza lugha yake. Viongozi wetu bila shaka huwa wanauhuru wa kutumia kiswahili pindi wanapohutubia nchi za watu, na hawaitumii nafasi hii kukitangaza kiswahili kwa kukitumia.


Tafiti nyingi zinazowahusu waTanzania, zinaandikwa kwa kiingereza, watanzania wengi wanaachwa kwenye mataa. Eti baadhi ya wasomi wanasema kiswahili hakina uwezo wa kuelezea vyema misamiati ya kisayansi na kiteknikali. Matokeo mabovu ya mitihani ya taifa, bila shaka kiingereza nacho ni tatizo.


Ni aibu sana kwa masomo kama Uraia, baadhi ya maswali hasa hasa yale ya kujieleza, huwa watungaji wanachomekea misamiati migumu yenye kukanganya kana kwamba lengo ni kupima mwanafunzi kwa kiasi gani anaifahamu misamiati ya kiingereza kuliko kumpima katika mambo yahusuyo Uraia.
Ebou's said…
This comment has been removed by the author.
Ebou's said…
KAKA HAPA NILIMUONA MTU ANA LALA MIKA KUACHA KIBWAGIZO CHA UJUMBE WASIMU KWA KISWAHILI NI NGUMU SANA.. KULIKO KINGEREZA... ALIEKUWA ANAACHIWA MSG NI MTUMZIMA KUTOKA TZ KWA KUWA ALIPONDOKA BONGO HAKUNA VOICE MAIL.. LOL NA ALISHAZOWEA KUACHA KWA KINGEREZA KWASABABU UNAWEZA KUACHA MANENO RAHISI NA MAFUPI. KULIKO KISWAHILI.

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?