Ufundishaji wa Kiudadisi: Maana, Faida na Namna Unavyoweza Kutumiwa



                                           Picha kwa hisani ya UNESCO learning Portal


Matumizi ya njia ya ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi umeenea maeneo mbalimbali duniani na hususani katika nchi za Ulaya. Ufundishaji Unaomzingatia Mwanafunzi ni mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji unaompa mwanafunzi fursa ya kujibidisha ili kujipatia maarifa na kutumia maarifa yake ya awali katika kujenga maarifa mapya badala ya kuwa mpokeaji wa maarifa na kisha kuyatumia kwa namna ya kuyakariri.  

 Katika machapisho mbalimbali, Ufundishaji Unaomzingatia Mwanafunzi umekuwa ukipewa majina anuai kama vile ufundishaji shirikishi, ufundishaji unaomzingatia mtoto, ufundishaji wa Kiudadisi na majina mengine. Hata hivyo, watumiaji wengi wa mfumo huu wa kufundishia na kujifunzia wanatumia zaidi istilahi ya Ufundishaji wa Kiudadisi.

Ufundishaji wa Kiudadisi bila shaka ni istilahi pendwa kwa kuwa inasadifu moja ya tabia muhimu ya udadisi anayopaswa kuwa nayo mwanafunzi wakati wa ujifunzaji wake na hata katika maisha ya kawaida. Kwa msingi huu, katika makala haya, mwandishi anajikita kwenye Ufundishaji wa Kiudadisi kama moja ya mbinu na namna ya kutekeleza ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi. Maana, faida na namna ya kutumia aina hii ya ufundishaji na ujifunzaji itajadiliwa. 

Maana ya Ujifunzaji wa Kiudadisi
Ufundishaji wa kiudadisi ni aina ya ufundishaji unaompa mwanafunzi fursa ya kujiuliza maswali yanayomuibulia hamasa ya kutaka kujua na hivyo kujenga mabunio (hypotheses) na kisha kujituma kupata majibu ya maswali yake kwa kurejea vyanzo mbalimbali ili hatimaye aweze kuongeza maarifa yake na ya wengine kupitia majadiliano, uwasilishaji, machapisho, kazi mradi n.k. Vyanzo mbalimbali anavyoweza kuvitumia mwanafunzi ni kama vile kuchunguza, kusoma maandiko mbalimbali (kama vile vitabu, majarida n.k) pamoja na vyanzo vingine kama vile internet, kutazama video, midahalo n.k.

Kama umeielewa vyema maana ya ujifunzaji wa Kiudadisi, utagundua kuwa, maswali makini anayoweza kujiuliza mwanafunzi huku akisaidiwa na mwalimu ni kiini cha mchakato wa kujifunza kwa udadisi. Mwanafunzi anapojiuliza maswali, inamaanisha kuwa anahitaji majibu. Hivyo anakuwa amejipa wajibu wa kujibidisha kupata majibu ya maswali yake. Maarifa ayapatayo mwanafunzi anategemewa aweze kuyatumia katika kujenga na kutetea hoja zake sambamba na kutatua changamoto halisi zinazomkumba yeye na jamii yake. 

Faida za Ujifunzaji wa Kiudadisi
Kama nilivyotangulia kugusia hapo awali, ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi umekubaliwa na unatumika kwa kiasi kikubwa sana na mataifa ya Ulaya, kwa uchache huko bara Asia na kwa kiasi kidogo kabisa Barani Afrika. Kutokana na umuhimu wa mfumo huu wa utoaji elimu, mataifa mengi ya Afrika kwa nyakati tofauti yamekuwa yakifanya mabadiliko yanayolenga kukidhi matakwa ya ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi. 

Nchini Tanzania, kwa mfano, katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu, ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi ulirasimishwa tangu mwaka 2005. Ni takribani miaka 12 ya utekelezaji wake. Hata hivyo, tafiti nyingi za hivi karibuni nchini Tanzania zinaonesha mfumo huu hadi sasa haujafanikiwa kutokana na sababu mbalimbali. (Wasome watafiti kama vile Alberto Paulo, Tillya, Mosha, Kafyulilo, Salema, Mtitu, Makunja na wengine wengi).

Hali ni tofauti katika nchi za Ulaya. Tafiti mbalimbali zimeonesha mafaniko makubwa ya ufundishaji wa kiudadisi. Kwa mujibu wa tafiti hizo, ufundishaji wa kiudadisi umeonekana kuwa na matokeo chanya yasiyo na mashaka kama vile kumuwezesha mwanafunzi kupata mafanikio zaidi kielimu, kumjengea mwanafunzi stadi za kujitegemea na kushirikiana na wanafunzi wenzake, na kumjengea mwanafunzi stadi muhimu za karne ya 21 kama vile uwezo mkubwa wa kupambanua, kufikiri, kutatua changamoto na stadi za uvumbuzi.

Faida nyingine ni pamoja na kukuza uwezo wa mwanafunzi wa kujiamini, kuwafanya wanafunzi kupenda kujifunza, kukuza stadi za kusoma (vitabu, majarida n.k), kumjengea mwanafunzi stadi ya ujifunzaji endelevu, nikizitaja kwa uchache. 

Ufundishaji wa namna hii siyo tu una manufaa kwa wanafunzi, bali hata kwa mwalimu. Uzoefu wangu mdogo wa kutumia njia hii ya kujifunzia  unanionesha kuwa, ikiwa mwalimu atajiandaa vyema, ufundishaji huu huleta hamasa kubwa ya kusimamia ujifunzaji. 

Kulingana na maandalizi niliyokuwa ninayafanya, nilijikuta nikitamani muda wa kuingia darasani ufike ili nisimamie ujifunzaji unaoongozwa na falsafa ya kuwashirikisha wanafunzi kwenye ujifunzaji wao. Ewe mwalimu au mwezeshaji yeyote, tumia njia hii leo na utakubaliana na hili nisemalo. 

Wajibu wa Mwalimu na Mwanafunzi 
Kabla ya kurasimisha ufundishaji/ ujifunzaji unaowazingatia wanafunzi, mitaala iliyokuwa inatumika shule za msingi hadi vyuo vya ualimu, ilikuwa ni ile inayomtambua mwalimu kuwa ni chanzo pekee cha maarifa. Katika mazingira haya, mwanafunzi alichukuliwa kama stoo ya kuhifadhia maarifa.

Wajibu wa mwanafunzi ulikuwa ni kusikiliza anachoambiwa kisha anafanya kila juhudi ya kukihifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadae. Mara nyingi mwanafunzi amekuwa akipimwa uwezo wake wa kukumbuka maarifa aliyopaswa kuyahifadhi. Hali hii imepelekea, mfumo wa pekee wa kujifunza kwa wanafunzi kuwa ni wa kukariri. Hata hvyo, pamoja na Tanzania kubadili mitaala, hali ya ufundishaji imeendelea kuwa ile ile. Mwalimu ndiye chanzo cha maarifa na mwanafunzi anabaki kuwa msikilizaji.

Hali inapaswa kuwa tofauti kwenye ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi. Mwalimu ana wajibu wa kumsadia mwanafunzi kujifunza yeye mwenyewe. Hivyo basi, jukumu kuu la kwanza kabisa la mwalimu ni kuwaelekeza wanafunzi namna ya kujifunza (learn to learn). 

Kuwasaidia wanafunzi kujifunza namna ya kujifunza ni wajibu wa msingi wa mwalimu. Wanafunzi wanapaswa kufahamu njia bora za wao kujifunza. Stadi hii inawapa uwezo wa kujisimia wakati wa ujifunzaji wao sambamba na kujitathmini ili kujua mwenendo wao wa ujifunzaji. Kujua namna ya kujifunza ni njia ya kuwaleta wanafunzi karibu zaidi na ujifunzaji wao na hivyo kujiona wanawajibika moja kwa moja.
 Kujua namna ya kujifunza huweza pia kuwa fursa ya wanafunzi kuyafahamu mazingira yao ya kujifunzia na kuyageuza kuwa fursa kuliko laana inayokwamisha maendeleo yao kitaaluma. 

Wajibu wa pili wa mwalimu ni kuwaongoza mwanafunzi kuandaa maswali yenye mantiki yanayoendana na mtaala na kile wanachopaswa kujifunza. Katika kuhakikisha wanafunzi wanaweza kujiandalia maswali yatakayowalazimisha kuyapatia majibu, nafasi ya mwalimu ni ya muhimu sana katika hatua hii. 

Angalau, uzoefu wangu unaonesha kuwa, moja ya mbinu nzuri ya mwalimu ni kuwa na utangulizi chokonozi. Wakati fulani nilipokuwa ninafundisha walimu wanafunzi mada ya kupanua Bainomio (Binomial Expansion), nilianza kwa kuwapa maswali rahisi ya kutanua , nikawa ninaongeza kipeo, cha tatu, cha nne, hadi cha tano. Upanuzi unakuwa mgumu kwa kadiri kipeo kinavyozidi kuongezeka. 

Wanafunzi walipofika kipeo cha tano na sita, kazi ikawa ngumu zaidi, nikawauliza wafikirie ikiwa watakutana na changamoto ya kupanua bainomio kama ya kipeo cha 10.  Baadhi ya wanafunzi walitoa uzoefu wao wa namna ya kushughulikia kipeo kikubwa kama cha 10. 

Niliwauliza wanafunzi ikiwa walikuwa tayari kujifunza namna ya kupanua bainomio zenye vipeo vikubwa. Walionesha kuwa tayari kujifunza. Niliwauliza pia, kwenye mada hii ni mambo  yapi walipenda kuyajifunza. 

Katika hatua hii, wanafunzi walitarajia, kama kawaida, nianze kuwaelezea namna ambavyo wangeweza kupanua bainomio. Kinyume chake, niliwapatia nyenzo ambazo niliamini zingewasaidia kujifunza namna ya kupanua binomio yoyote ile sambamba na dondoo ambazo zingewaongoza kujifunza.  Na huu ndio wajibu wa tatu wa mwalimu. Kuwapatia wanafunzi vitendea kazi vitakavyowasaidia kujifunza.

Katika kuwasaidia wanafunzi kutumia nyenzo za ujifunzaji, kuna mambo mawili ya kufahamu. Moja ni kuamua ikiwa mwalimu atawapa wanafunzi dondoo ambazo zitawaongoza kutafuta majibu ya maswali yao. Namna nyingine ni ya kuwaacha watafute maarifa kwa wigo wao wenyewe hadi watakapoona wana taarifa za kutosha kujibu maswali yao. 

Kila namna inategemea na aina ya wanafunzi na urahisi wa upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia. Watoto wadodo kama vile wa shule za msingi wanaweza kuelekezwa nini watafute. Wanafunzi wa shule za sekondari na kuendelea wanaweza kupewa uhuru wa kutafuta taarifa, kuzijifunza na kisha kuzitumia kujibia maswali yao ya kiudadisi. Mwalimu mgeni wa njia hii ya ufundishaji, ni vyema akatumia mfumo wa kuwapa wanafunzi dondoo. 

Wajibu wa tatu wa mwalimu ni kuandaa nyenzo watakazozitumia wanafunzi kujifunzia. Upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia mashuleni umetajwa kwenye tafiti nyingi za Ufundishaji unanaowazingatia wanafunzi kuwa ni tatizo kubwa nchini Tanzania. 

Lakini, tujiulize, mwalimu anatumia nini wakati wa kujiandaa kwenda darasani kufundisha?
Mwalimu anajua wajibu wake ni kusoma kwa kina ili ayafahamu vyema yale anayopaswa kuyafundisha. Ni kweli, kujua vyema maudhui yanayopaswa kujifunzwa na wanafunzi ni muhimu. 

Swali la kujiuliza ni  kama walimu huwa wanajiuliza ni kwa namna gani watafikisha kwa wanafunzi nyenzo hiyo ya kujifunzia wanayoitumia wao. Ukweli ni kuwa, wengi wetu hatufikiri hivi. Tunachoona kuwa ni wajibu wetu ni sisi kujifunza na kisha kwenda darasani kutoa taarifa ya ujifunzaji wetu.

Katika mfumo wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi, moja ya wajibu wa msingi wa mwalimu ni kuandaa nyenzo kwa ajili ya wanafunzi kuzitumia kujenga uelewa wao. Hata hivyo, miongoni mwa walimu wengi, huu ni wajibu wa msingi sana unaopuuzwa. tusipolitambua hili, wimbo wa kukosekana kwa nyenzo za wanafunzi kujifunzia litaendelea kuwa tatizo kubwa. 
Kwa kuwa hatufanyi hivi, hata kwa kitabu kimoja kilichopo shuleni, ni vigumu sana kutambua uhalisia wa upungufu wa nyenzo hizo.

Kama sehemu ya maandalizi, mwalimu anapaswa kutumia muda wake mwingi kupitia, kutathmini na kukusanya nyenzo ambazo wanafunzi watazitumia kujifunzia. Kama sehemu ya wajibu wake, wamwalimu anapaswa kutafakari na kubuni njia ambazo mwalimu atazitumia kuwasilisha nyenzo hizo darasani. Katika hatua hii, ni muhimu kutambua umuhimu wa TEHAMA kwenye kurahisisha  kuwasilisha nyenzo za ujifunzaji madarasani. 
  
Kipengele hiki ni cha muhimu sana. Kwa hali ilivyo sasa, ninaweza kusema kuwa, walimu wengi wamekuwa wakijifundisha wenyewe madarasani. Wanakuja na taarifa zao walizozikusanya wakati wa kile wanachokiita maandalizi ya kufundisha. 
 
Kimsingi, darasani hakuna kinachoendelea zaidi ya mwalimu kufanya mazoezi ya kukumbuka na kurejea yale aliyokuwa anayasoma wakati akijiandaa kwenda kufundisha. Hii ni kusema kuwa, mara nyingi mwalimu huwa anajifundisha mwenyewe: Mtazamo unaoshabihiana vyema na ule msemo kuwa, anayefundisha ndiye anayejifunza zaidi. mtazamo huu, unarejea sawia aina ya ufundishaji ambao mwalimu ndiye chanzo kikuu cha maarifa. 

Mwalimu anapaswa kutumia muda wake mwingi kutafuta nyenzo kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia na kuwaza na kubuni namna ya kuziwasilisha nyenzo hizo madarasani. Wanafunzi nao, wanapaswa kuwa na mtazamo wanahitaji zaidi nyenzo za kujifunzia na mtu (mwalimu) wa kuwaongoza na kuwasaidia kutumia nyenzo hizo kwa ufanisi.

Wajibu wa mwisho wa mwalimu, lakini siyo wa mwisho kwa umuhimu ni kuwa na uwezo usio na mashaka wa maudhui wanayopaswa kujifunza walengwa. Ikumbukwe kuwa, baada ya wanafunzi kufanya utafiti wao, watawasilisha yale waliyojifunza. Wanafunzi wanaweza kuwa na muda wa kujadiliana. Hapa kunaweza kutokea mawazo kinzani kulingana na vyanzo na uelewa wa awali wa wanafunzi. Ni wajibu wa mwalimu kuongoza wanafunzi kujifunza mambo sahihi na hivyo hana budi kuwa na weledi wa kutosha wa maudhui hayo. 

Madarasa yanapaswa kuwa karakana za wanafunzi za kujijengea stadi na maarifa mapya. Ifahamike pia kuwa, madarasa ya karne ya 21 siyo lazima yawe kuta nne zenye viti, meza na ubao. Kwa kasi ya ukuaji wa TEHAMA, ujifunzaji unaweza kufanyika popote na kwa wakati wowote. 

Pamoja na changamoto zilizopo, zikiwemo za upatikanaji wa nyenzo kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia, walimu hawana budi kuanza kutumia rasilimali chache zilizopo. Utayari huu ni mwanzo wa kuonesha kwa vitendo upungufu uliopo. Kusema kuwa nyenzo za kufundishia hazitoshi, ilihali chache zilizopo hazitumiki, si namna nzuri ya ushawishi.  tusisubiri kibaba kijae, tutumie kidogo kilichopo, tutaongezewa kwa kuwa tunaonesha tuna uhitaji.









Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?