Saturday, June 25, 2011

Pengine haikuwa busara kuwafukuza; labda harakati za kutafuta haki na usawa wa binadamu.

Tanzania tunakaribia kuadhimisha miaka hamsini ya Uhuru. Lakini kwa hali duni ya kiuchumi na kisiasa ilivyo, haitamnyima raia wa kwaida kabisa kuamini kuwa uhuru hauna maana kwake. Tazama vita kati ya wananchi na wawekezaji (wakoloni wa kizungu wa karne ya leo) unavyogharimu maisha ya watanzania. Umeme umekuwa ni tatizo sugu ambalo linaweza kutatulika. Waandishi wa habari wanakosa uhuru wao wa kufanya kazi. Haishangazi sana kwa wafanyakazi wa umma kufanya kazi nusu mwaka, mwaka mzima na hadi miaka bila kulipwa stahiki zao ikiwemo mishahara yao. Huu ni utumwa. Inaashiria kuwa bado tuna haja ya kuutafuta uhuru ambao tunadhani tayari tunauogelea.
Hali ya utumwa unaoendelea Tanzania unanifanya niamini kuwa, kwa kuwafukuza wakoloni wa kizungu haikumaanisha kuwa tulipata uhuru na hivyo tukawa huru. Nadhani tulipaswa kutambua tu kuwa, waafrika asili yetu ni Afrika na ili tuwe huru hakukuwa na umuhimu wa sisi (waafrika) kuishi peke yetu(kujitenga) kama ishara ya kuwa huru. Hata hivyo jambo hili halijawezekana.

Binafsi ninaona ni bora harakati za kutafuta haki za binadamu zingepewa kipau mbele kuliko kutafuta uhuru kwa kuwafukuza wale walioonekana kuficha na kuwakosesha uhuru wazawa.

Inashangaza kidogo kwani wale tuliowafukuza katika harakati zetu za kutafuta uhuru, ndio haohao leo hii wamekuwa ndio kimbilio letu. Leo hii tunawafuata na kuwaomba waje kwetu kutusaidia kutumia rasilimali zetu; wawezeshe mipango ya muda mrefu na mfupi kwa kuwa wahisani wetu katika bajeti ya serikali. Miaka hamsini tutajivunia kuwa tumejenga barabara kwa hisani ya watu wa china, hospitali zimejengwa kwa hisani ya serikali ya Uingereza na kadhalika. Kwa mwendo huu sisiti kusema kuwa, nishati ya umeme imekuwa ni tatizo kwa kuwa hakuna wahisani!

Miaka hii hamsini sijui tunajivunia nini wakati wale tuliowafukuza ndio hao tunawarudia na kuwapigia magoti warudi kiuwekezaji. Uwekezaji katika maeneo mengi umeshagharimu maisha ya watanzania wengi. Migogoro kati ya wananchi na wawekezaji haiishi. Idadi kubwa ya wananchi wapo gerezani bila ya hatia kwa sababu ya wawekezaji kulindwa. Tunarudi kule kwenye utumwa. Tofauti na hivi sasa ni kuwa, badala ya watu kuteswa vibaya hadharani (kuna hofu ya wanaharakati wa haki za binadamu) kwa kuchapwa viboko, kufanyishwa kazi za sulubu na hata kuuawa, wanaswekwa gerezani, na mambo mengine yanaendelea chini kwa chini. Hakuna atakayebisha kuwa, vita vile vya majimaji vimerudi tena. Utaratibu wa Ngwale upo; uwekezaji unavaa sura ya maji yale ya Ngwale.

Tanzania bado tunahitaji umakini zaidi. Pengine ifikie mahali tufikirie kuwa inawezekana kujitegemea. Ifikie mahali tusipige magoti ili kupata tunachohitaji; ifike mahali tusifikirie kutembeza "kibaba" ilihali rasilimali zituwezeshazo kukijaza kibaba chetu wenyewe zipo. Na,haina maana kupewa fedha ili kukuza uchumi, ni afadhali kuwezeshwa kujipatia fedha ili kujikuzia uchumi wetu wenyewe. Tukiendelea kutembeza kibaba hasahasa kwa wale tuliowafukuza katika harakati za kudai uhuru, basi mimi, wewe na yule (pengine) hatutashindwa kufikiri kuwa, haikuwa busara kuwafukuza wakoloni, badala yake kumbe kilichotakiwa ni kuanzisha "harakati za kutafuta haki na usawa wa binadamu".

0 comments: