Saturday, March 12, 2011

Inatosha sasa kuona, bora mimi kusema: Serikali yangu iharibuyo kioo itegemeacho kujitazamia.

Ni siku nyingine ya Jumamosi ambapo blogu yako ya Mwangaza inakuletea kipengele cha "Inatosha sasa kuona, bora mimi kusema".

Naam, wiki hii tarehe nane mwezi huu, wanawake duniani waliadhimisha siku yao almaarufu Siku ya Wanawake duniani. Hapa Tanzania, kilele cha maadhimisho hayo yalifanyika pia, kama ilivyozungumziwa hapa katika tovuti ya Startv.
Sina hakika sana kama maadhimisho haya yalifanyika kuanzia ngazi ya kijiji hadi kitaifa. Mimi katika pitapita yangu ya kimajukumu, nilikumbana na maadhimisho hayo katika shule ya msingi Tumuli iliyopo wilayani iramba mkoani Singida, pamoja na kuwa sikuwa na muda mwingi wa kufuatilia maadhimisho hayo.

Mgeni rasmi alikuwa mkuu wa Wilaya ya Iramba akiwa na msafara wake uliosheheni vigogo mbali mbali wa chini yake.
Mengi yaliongewa na kukamilishwa na kauli mbiu isemayo "Fursa sawa katika elimu,Mafunzo na Teknoloji:Njia ya wanawake kupata ajira bora" ambayo ndiyo kauli mbiu ya siku ya wanawake kwa mwaka huu. Iinigusa sana na kunifanya nitafakari kuhusu juhudi za serikali na hatma ya akina mama hawa wa miaka ijayo wanavyojaribu kuufikia ujumbe huu mzito katika mazingira magumu kama inavyoonekana pichani hapa chini.





















 mazingira yenyewe ndio haya, lengo litatimia?















Watoto hawa ni wa shule ya msingi Tumuli, shule ambayo maadhimisho haya yalifanyikia. Mkuu wa wilaya na wajumbe wake walifika shuleni hapo na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha kupata kifungua kinywa(darasa ambapo masomo yalilazimika kusitishwa) na kisha kuelekea sehemu iliyotengwa kwa ajili ya tukio hilo.
Sina hakika kama mkuu wa Wilaya ama kiongozi mwingine aliwaza kutazama mazingira halisi ya kusomea ya akina mama hawa wa miaka ya kesho kutwa na kutathmini kama, na ni kwa namna gani ujumbe katika siku hii ya wanawake ungeweza kufikiwa katika mazingira magumu wanayokabiliana nayo akina mama hawa wa miaka ijayo kama ionekanavyo pichani juu.

Baada ya Sherehe, wakubwa hawa walirudi tena kwenye darasa maalumu kwa ajili ya kupata chakula cha mchana kilichoandaliwa vyema kabisa; wanafunzi nao walienda kupata chakula chao cha mchana (kama ionekanavyo pichani hapa chini wakiwa kwenye foleni na baadae wakiwa wamekaa "bwaloni" wakipata chakula cha mchana ) ambapo chakula kilikuwa ni mahindi makavu yaliyochanganywa na maharagwe na kupikwa kwa pamoja (almaarufu ngararimo/ndutu au makukuru kwa wachaga). Walituliza njaa yao huku wakiishia kula kwa harufu tu vile vinono vilivyoandaliwa kwa ajili ya wakubwa hao waliofanya masomo yao yasiende kama kawaida baada ya maadhimisho hayo kufanyikia shuleni hapo.



















 Wanafunzi wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kuchukua chakula.


Picha hapa chini, wanafunzi wakila chakula cha mchana (mahindi na maharage vilivyopikwa kwa pamoja)















Shule hii ni mchanganyiko, yani wanafunzi wa kike na kiume. Nimewaongelea hawa wa kike kwani siku hii iliwahusu sana na kauli mbiu ilikita kwenye elimu ambayo msingi wake ndipo hasa walipo akina mama hawa wa miaka kadhaa ijayo.

Naam, bado nikiwa nimejikita zaidi katika kuwaangalia akina mama wa ziku zijazo, serikali yangu ya Tanzania inashindwa kutambua (kwa makusudi) kuwa kutokutimiza wajibu wake katika nyanja mbalimbali za kielimu, kijamii na kiuchumi ni kikwazo namba moja cha kukwamisha ufikiwaji wa kauli mbiu kama hizi za siku ya Wanawake duniani(sina hakika hata kama huwa wanakumbuka kutoa tathmini ya kauli mbiu iliyopita; imefanikiwa ama haijafanikiwa na kwa kiwango gani)

Ni serikali hii hii inayoruhusu msongamano mkubwa wa wanafunzi madarasani ambapo matokeo yake ni mwalimu mmoja kuwahudumia wanafunzi wengi kuliko uwezo. Hapa bado akinamama wa kesho wanazidi kukandamizwa(akina baba wa kesho hali kadhalika) tazama darasa hili pichani. Ni chuo cha ualimu Kinampanda kilicho na uwezo wa kuchukua wanafunzi 240 tu lakini kwa sasa kina wanafunzi 577. Labda niiulize serikali katika hali hii, kauli mbiu kama hii ya mwaka huu ya wanawake itafikiwa kweli? Serekali itakwepa kulamumiwa kuwa yenyewe ndio inaongoza katika kuisaliti kauli hii ilihali haipitwi na maadhimisho haya kila mwaka na yenye kufana? Hapa sio kwamba serekali inavunjavunja kioo inachokitegemea kujitazamia?



Akina mama hawa wa leo na kesho (wapo pia akina baba wa leo na kesho) wasomao katika chuo hiki ambao nao wanatazamiwa kwenda kuwafundisha akina mama wa miaka ijayo wanatendewa haki kweli? Haitoshi, mazingira ya Wakufunzi bado nayo ni duni. Wakufunzi wapya katika chuo hiki hata na vyuo vingine kama hiki, mambo ni haya haya. Mwezi wa pili huu wanasota chuoni; hakuna hela ya kujikimu wala mishahara. Hapo hapo serekali inategemea Mkufunzi huyu atimize wajibu wake wa kutoa elimu bora ipasavyo! Jambo ambalo kwa kiasi kikubwa haliwezekani. Ndivyo serikali yangu inavyozidi kujipoteza katika harakati za kujitafuta na kama jinsi inavyozidi kuvunja kioo inachokitegemea sana katika kujiangalia taswira ya uso wake.
Tukutane tena wakati mwingine (jumamosi ijayo) katika safu hii. Jumamosi njema, mwisho na mwanzo mwema wa juma kwenu nyote. Hadi wakati mwingine, mara nyingine.

12 comments:

SIMON KITURURU said...

Mmmh!

Albert Kissima said...
This comment has been removed by the author.
Albert Kissima said...

Ndio mazingira ya watoto wetu kaka. Hali inatisha, hatma ya viongozi hawa na akina mama na akina baba wa miaka ijayo kwa kweli haijulikani. Nimepata fursa ya kutembelea shule kadhaa za Msingi hapa Singida hususani wilaya ya Iramba na singida vijijini, wengi wa wanafunzi wanasoma katika mazingira magumu sana!

Anonymous said...

Umesema kweli na endelea na kazi nzuri ya kuonesha ugonjwa badala ya kuuficha. Si vijijini tu. Hata mijini na majijini kama dar es Salaam tumekuwa tukioneshwa watoto wa shule waliorundika ndani ya chumba kimoja cha darasa na huku wamekaa sakafuni - karne ya 21. Kuhusu mustakabali wa akina mama (na akina baba)wa siku zijazo ni kwamba utaratibu ama niseme mfumo wa kijamii na kiuchumi tulioamua kuukumbatia (yaani ubepari uchwara)uko wazi kuhusu swali lako - tunatengeneza matabaka makuu mawili: tabaka la walalaheri (ambao ndio watakuwa watawala) na walalahoi (wapiga kura ambao kazi yao kuu ni kuhalalisha uwepo wa watawala). Hili linajidhihirisha kwa uwazi katika hayo mazingira ya kielimu unayoyazungumza. Hali hii haizuiliki kadri tunavyoendelea kukumbatia mfumo huu. Hayati Baba wa taifa, JKN, alisema "ubepari ni unyama" - sisi tukambishia!!!!!!

Mzee wa Changamoto said...

Naaaaaam...
Hiki ni kipengele MWANANA saana Kaka. Wakati umeika wa kuamka na kuwaeleza wanandugu kuwa BILA KUSEMA, SERIKALI ITADHANI HATUONI.
Ni kweli kuwa INATOSHA KUONA, BORA TUSEME.
I love this

chib said...

Wenyewe wanaotoa kauli mbiu zote hizo sina hakika kama hawana habari na hali mbaya iliyopo.
Tumechoka na hizo kauli mbiu, yaonekana hawana jipya vichwani mwao zaidi ya kauli mbiu

SIMON KITURURU said...

Inatosha sasa kuona, bora mimi kusema: Albert umepotea Mkuu hapa kijiweni! Salama lakini?

Albert Kissima said...
This comment has been removed by the author.
Albert Kissima said...

Shwari kabisa Mtakatifu Simon,yeah, ni kweli, inatosha sasa kuona;nimekuwa bize kidogo kwa upande mwingine, lakini Mkuu Mtakatifu pamoja na bloggers wote, tupo pamoja sana. Nitumie nafasi hii kuwatakia bloggers wote sikukuu njema ya kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo. Siku hii na zijazo, ziwe na amani, upendo, furaha na mafanikio tele kwa kila mema.

Raymond Mkandawile said...

Kazi nzuri kaka kaza buti na kila la kheri...

Teuvo Vehkalahti said...

Greetings from Finland. Thus, through a blog is a great get to know other countries and their people, nature and culture. Come take a look Teuvo images and blog to tell all your friends that your country flag will stand up to my collection of flag higher. Sincerely, Teuvo Vehkalahti Finland

emu-three said...

Sema ukweli, ingawaje unauma, lakini ni bora kuliko kunyamaza