Soko la Magulioni-Singida Mashariki

Kati ya sehemu ambazo wananchi wake wanahatarisha maisha yao, basi ni hapa katika soko hili liitwalo MAGULIONI ambalo lipo eneo maarufu liitwalo Njia panda ya Makiungu pembezoni mwa barabara ya Singida-Manyara. soko hili huwa kila siku ya Jumamosi na husheheni vitu vya kila aina kuanzia mboga mboga, nguo, kuku, miwa, vyungu, vyakula mbali mbali vikiwemo viazi vitamu vilivyopikwa na ambavvo havijapikwa, majembe n.k Kiujumla, halitofautiani na masoko mengine ambayo ulishawahi kuyaona.

Mbali na upatikanaji wa vitu mbali mbali nilivyojitahidi kuvitaja, lakini pia, kila Jumamosi idadi kubwa ya watu hulitegemea sana soko hili kwa kitoweo cha nyama: kuanzia ya ng'ombe hadi ya mbuzi. Walaji wa nyama hizi kwa hakika wapo katika hatari kubwa sana kwani kulingana na uchunguzi wangu niligundua kuwa hakuna dakitari wa kuangalia uhalali wa matumizi ya nyama hizo, machinjio duni na pia sehemu za kuuzia nyama hizo ni hatari kabisa kwa afya za walaji.

Picha hapa chini zinaonesha baadhi ya mabucha ambayo watu kutoka sehemu mbalimbali hufika hapo kujinunulia nyama kwa ajili ya  mahaitaji mbalimbali ya nyumbani, mahotelini, mashuleni, maofisini na sehemu nyingine zenye uhitaji.



Hili ni Bucha lililokuwa kwenye maandalizi ya kuwekewa nyama tayari kwa kuanza kuuzwa. Nyama zinazowekwa hapa ni zile mbuzi na kondoo au na za Punda kama zipo maana nilisikia hata za Punda mara nyingine huwa zinaletwa kwa uficho.





Hili ni Bucha la nyama ya mbuzi. Kama uonavyo, nyama ya mbuzi imetundikwa wateja wakisubiriwa.

 Na hili ni bucha la nyama ya ng'ombe kama uonavyo. Nyama zipo wazi sana kiasi kwamba vumbi na wadudu wasambaza vimelea vya magonjwa wanaweza kutua kwenye nyama kwa urahisi kabisa.




Hii pia ni sehemu iliyotayarishwa kwa ajili ya kuwekea nyama za kuuzwa.


Hakika ni mazingira ya kutisha. Mheshimiwa Tundu Lissu, haya yapo katika jimbo lako la Singida Mashariki. Wewe na viongozi wengine wahusika, liangalieni hili kwa umakini. Eneo hili likiangaliwa vizuri litaboresha sana maisha ya wanavijiji wa vijiji vya karibu na wanaSingida kwa ujumla. Tofauti na hapo, utakuja wakati ambapo kwa ubovu wa huduma, basi wanaSingida na waTanzania kwa ujumla watagubikwa na simanzi maana kuna wakati watu watalishwa vibudu vya wanyama vilivyosababishwa na magonjwa hatari yatakayogharimu maisha ya watu.



Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Kubadilika kwa Mitaala: Walimu na Wanafunzi Wabadilike kwa Namna Gani?