Ukeketaji wa wanawake nchini Tanzania ni jambo ambalo (pengine na kwingineko duniani) kwa miaka iliyopita lilikuwa limeshamiri sana katika jamii zetu kiasi kwamba watu pengine hawakukaa kuwaza kuwa ipo siku jambo hili litapewa kipau mbele kwa kupingwa na wanaharakati duniani kote. Hili limefanyika na sasa jamii kwa kiasi kikubwa imekuwa adui wa jambo hili na kwa miaka ya hivi karibuni ukeketaji umepungua kwa kiasi kikubwa.
Wahusika wa ukeketaji wamejisalimisha, wamesaliti amri kwa wingi wao japokuwa bado wapo pia ambao wanaendelea na ukeketaji.
Uchawi kama ukeketaji ulivyokuwa, ni tatizo kwa Taifa letu watanzania. Sehemu nyingi za Tanzania zinakosa maendeleo ambapo, pamoja na mambo mengine, uchawi unachangia sana.
Ni siku za hivi karibuni tumesikia huko Mbozi mkoani Mbeya, walimu walizikimbia shule walizokuwa wanafundisha kwa madai ya kusumbuliwa na mambo ya kichawi. Si Mbeya tu, hali hizi zipo sehemu nyingi Tanzania.
Si walimu tu wanaathirika, lakini mambo mengine mengi ya kimaendeleo yanashindikana kwa sababu ya uchawi. Vita ya kuupinga uchawi haijapewa msisitizo kabisa na watu mbali mbali duniani huku baadhi ya nchi kama Romania kuuhalalisha. Labda pengine swala hili lipo kiutamaduni zaidi, lakini hata Ukeketaji wa wanawake hapo awali ulikuwa na sura kama hii.
Sidhani kama kuna uchawi wenye tija katika jamii zetu. Mtu mwenye wivu mbaya na mwenzake, anatumia uchawi kumuangamiza, anamzibia njia za mafanikio, twasikia mvua zinazuiwa, yanasikika matukio ya watu kuchukuliwa misukule na kufanyishwa kazi ngumu, radi zisizotegemewa za mchana wa jua kali zinazogharimu maisha ya watu, ajili nyingine za magari zinahusishwa na uchawi n.k Matukio ya aina hii ni mengi katika jamii zetu. Madhara yake ni makubwa likiwemo hili la kutoa uhai wa binadamu. Madhara haya na mengine, yananifanya nione kuwa jambo hili nalo linapaswa kupaziwa sauti ya kulikemea.
Kwa mantiki hii, kama ilivyo kwenye swala la ukeketaji na msisitizo wa vita dhidi yake, nadhani umefika wakati wa kuuvalia njuga uchawi. Njia muhimu na muafaka ni kutoa elimu kwa jamii. Watu waelimishwe kuhusu madhara ya jambo hili, waambiwe kuwa maisha bila uchawi inawezekana, waelimishwe kuwa uchawi nao ni adui wa maendeleo kama jinsi ilivyo rushwa au ufisadi. Wachawi na wote walio katika mrengo huu wataelimika, wataachana nao, watasalimisha zana zao, na mwisho watasaidia kupambana na wakaidi.
Zipo habari za kushangaza sana nchini Romania kuhusiana na uchawi. Nchi hii imehalalisha uchawi. Wachawi katika nchi hii sasa watatambulika kwa vyeti vyao kwa kutunukiwa kulingana na uwezo wao. Swali la kujiuliza hapa ni kuwa uchawi huo wa hali ya juu utaoneshwa kwa watu, wanyama au kwa viumbe wasio hai?
Yupo mchawi mmoja nchi humo aliyesema kuwa yeye atatumia uchawi kuiloga serikali yake ili kodi isikusanywe kutoka kwake. Kauli ya mchawi huyu imekuja baada ya serikali ya Romania kusema kuwa itakusanya kodi kama ilivyo kwa wafanyakazi wa taaluma nyingine. Hii ni kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari.
Kauli ya mchawi huyu bado inadhihirisha kuwa uchawi haufai katika jamii. Tuukemee kwa njia muafaka kama za kuelimisha na si kuwaua kama jinsi wafanyavyo wale jamaa wa kule kanda ya ziwa wanavyowaua vikongwe. Wanasahau kuwa hata vijana wadogo kabisa ni nguli wakubwa wa uchawi!
Wanaharakati tupo? Au ndio yale yale ya nani wa kumfunga paka kengele? Kazi tunayo, tuingie vitani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

6 comments:
Kaka Albert! Nakubalina nawe kabisaaa ili swala inabidi lipigwe vita kwani hii ni imani potovu kabisa katika jamii yetu. Nakumbuka nilikuwa mdogo babu yangu mzaa mama alikuwa mgonjwa na baadaye alifariki na hapo kukazuka kuwa alikuwa kalogwa na kaka yake na uadui wa kifamilia ukwa. Lakini si kweli babu alilogwa kwani alikuwa amepungukiwa damu nao wakasema kakake alikuwa anamfyoza/kunywa ile damu....imani potovu tu...ni lazima lipigwe vita kweli...
Ni kweli Albert, watu pia wamrudie Mungu wao muumba mbingu na nchi, sio miungu ipotoshayo na kuleta uhasama katika jamii.
Imani hizi zinahitaji tafakuri la hali ya juu, kwani kama halijakukuta huwezi kusema kitu , wanasema `aisifuye mvua imemnyea,,'
mmmh ni kweli@emu-three, naona ahta docta amekaribia kubwaga manyanga lakini nina imani atatafuta historia ya nyumba na hatimaye kujua hatma ya nyumba na pengine kupata suluhisho la kudumu na hata kupelekea wahusika wa mauzauza hayo kubwaga manyanga.
Tatizo ni kwa ndugu zangu wa Shinyanga ambao kibibi ajuza hugeuzwa na kuwa mchawi!
Greetings from Finland. This blog is fun to explore, through other countries, people, culture and nature. Come take a look Teuvo pictures blog. And tell all your friend, why you should visit Teuvo pictures blog. Therefore, to obtain your country's flag rise higher Teuvo blog pictures of the flag collection, Happy Thanksgiving to Teuvo Vehkalahti Finland
Post a Comment