Sunday, November 14, 2010

Jamii yangu; kijijini Siuyu.


Kizazi cha sasa na upotezaji wa muda usio na tija yoyote.



Asubuhi ya leo vijana wakijiburudisha na pool table.


Wazee nao asubuhi hiyo hiyo wakicheza bao.

Kwenye makala yangu iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosema "NIPO SINGIDA" nilieleza kushangazwa na hali ya vijana na wazee kuonekana asubuhi wakicheza bao na pool table. Hali ndio kama muionayo pichani.

Sehemu hii ni maarufu kidogo. Pamechangamka kwa kiasi, panaitwa "madukani" kwani ni sehemu yenye maduka kadhaa yanayohesabika lakini.

Cha ajabu kabisa pamoja na uwepo wa maduka haya, hukuna duka liuzalo "mikate". Nakumbuka siku nilihitaji mkate na nilitembelea maduka yote bila mafanikio kama vile nilikuwa na mpango wa kuwasalimia wauzaji.

Ni kweli kuwa mikate hiyo ikiwepo haitanunuliwa? Ingenunuliwa, na mimi ningekuwa miongoni mwao. Tatizo watu hawana elimu ya ujasiriamali. Vijana hawasomi majira ya wakati. Hawaumizi kichwa. Utaratibu ni ule wa bora kumekucha, nimepata ugali mlenda mchana, usiku ugali chumvi, siku imekwisha, Mungu anashukuriwa.

Vijana hawa wenye nguvu asubuhi na mapema wanacheza pool table. Asubuhi yote wangeshaingiza pesa kwa kuuza bidhaa adimu ya mikate! Mkoa wa Singida una mawe mengi yapatikanayo kirahisi sana. Kungekuwa na wajasiriamali wa Dar es Salaam wawezao kufanikiwa kupitia mazingira ambayo mwanzoni yalionekana yasiyowezekana, wangeshatumia mawe haya kujipatia kipato kwa kuyageuza kuwa kokoto kwa kadiri ya nipatavyo hisia za wajasiriamali hawa wa Dar es Salaam. Maisha ya Dar es Salaam hakika yanamlazimisha mtu kuumiza kichwa hasa! Watu wanawalazimisha wengine kuingia gharama ya vitu wasivyokuwa wanavitegemea kupitia ubunifu wao.

Nani ambaye angeamini kuwa "chenchi" ipo siku zingeuzwa badala ya mtaka "chenchi" kupewa bure? Ukihitaji chenchi ya elfu moja leo hii hususani jijini Dar, muuzaji anakupa mia tisa.

Wapo pia wale wanaouza betri za simu zilizokwisha tumika na vifaa vingine vya simu vilivyokwisha tumika pia kule kariakoo. Ni kazi ambazo pengine mtu anaweza kuona wauzaji wanapoteza muda, lakini ndio kazi waitegemeayo na wanaridhika.

Vijana wa hapa naona hawajui maana ya ujasiriamali na nini wanatakiwa kukifanya. Wanaweza kuhisi kuwa hakuna watakaonunua mikate mathalani, pindi watakapoanza kuiuza, au hawatapata wateja wa vocha za kurusha, kwani nalo ni tatizo sana hapa. Hawajajua ujasiriamali wahitaji kutafuta soko, wahitaji kuwalazimisha au kuwashawishi watu kununua bidhaa husika pamoja na kuwa haukuwa utaratibu wao. Bado hawajatambua haya.
Binafsi naona nina wajibu wa kuzungumza na vijana wenzangu hawa na kupata mawazo yao. Na hili bila shaka panapo wasaha nitalifanya.

7 comments:

Mbele said...

Hii habari imenigusa sana. Inasikitisha kuona jinsi nchi yetu ilivyo. Nami nimeona hayo hayo unayoelezea kule kwetu Umatengo, wilaya ya Mbinga, ambako zamani watu walikuwa wanafanya kazi siku nzima, mashambani, hata tukatungiwa wimbo, "Wamatengo ni hodari, katika kazi...," wimbo uliochapishwa katika kitabu kiitwacho "Chiriku," ambacho kilikuwa maarufu mashuleni.

Leo ukienda Umatengo unakuta watu vilabuni saa za asubuhi, kama huko kijijini Siuyu.

Anonymous said...

Umenikumbusha mbali sana kule kijijini kwetu Mbutu wilaya ya Igunga. Watanzania tunakila haja ya kubadilika.

Amos Msengi said...

Michezo ni mizuri kama itafanyika katika muda unaokubalika.
NAKUKARIBISHA KWENYE HII BLOG, http://www.amosmsengi.blogspot.com/

SIMON KITURURU said...

KAZI IPO!:-(

Albert Paul said...

Hali hii inasikitisha sana. Sijui hii operesheni ya "ondoa tembe" itafanikiwa vp, au pengine vijana wanadhani watasaidiwa kila kitu.

Niliongea na baadhi ya vijana wakanieleza kuwa kazi hakuna na wapo wanaosubiri kuajiriwa. Sio kwamba wamemaliza elimu ya juu, ni vijana wa mtaani wanaochagua kazi. Wanasubiri kuajiriwa na si kufikiri wao wanaweza kufanya nini.

Upo mchezo mwingine wa kamari uitwao "korokoro". Mchezo huu hukusanya watu si pungufu ya kumi na tano, watoto, vijana kwa wazee. Watu hutegemea kamari hii kama sehemu ya kujipatia kipato.

Niliongea na mcheza kamari mmoja ambae alikuwa ameshajikusanyia pesa nyingi tu. Nilimuliza kama angalao kuna kazi ameshafanya kabla ya kufika kwenye kijiwe cha korokoro kwani ilikuwa muda wa saa nne asubuhi. Yeye aliniambia kuwa alitoka kulima na alifika pale angalao kutafuta hela ya kula.

Ninachojiuliza ni kuwa hela za kucheza kamari wanazitoa wapi? Jamaa huyu aliniambia kuwa wapo wacheza kamari wanaojizolea hadi shilingi elfu arobaini kwa muda mfupi. Pesa ambazo zingetumika katika maendeleo, zinapelekwa kwenye kamari. Ama kweli wajinga ndio waliwao.

Serina said...

Nilipitia Singida miezi sita iliyopita na kwa kweli, nilishangazwa sana na kutoka kwangu ilikuwa kwenda tu dukani kununua hiki ama kile... siku tatu nzima nilihisi kama mtu aliyebwagwa kwenye karne nyingine... kilichonifurahisha kama kawaida ni ungwana wa watanzania..

Albert Paul said...

Pole sana dada Serina, ndio mazingira yetu. Yanakatisha tamaa ya kuishi, ila kwa wazawa, wamesharidhika.

Nashukuru kwa kuridhishwa na ukarimu wa wanaSingida hususani wa sehemu uliyofikia.