
Wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao kunaweza kuchangiwa na mambo mengi. Wengi tujuavyo au tuzanivyo; mwanafunzi akifeli mitihani hususani ile ya taifa, tunachukulia kuwa ni uzembe wake kwani hakuzingatia vyema masomo au uwezo wake darasani ni mdogo. Ndivo ambavyo wazazi/walezi hata na walimu wengi wajuavyo.
Kweli, hizi zaweza kuwa ni sababu lakini zipo sababu nyingine ambazo watu wengi huwa hawazidhanii kuwa zaweza kusabisha mwanafunzi kufeli.
Leo nina nia moja tu ya kuzungumzia uzembe ujitokezao mara kwa mara katika mitihani ya taifa, yani ile ya kumaliza shule ya msingi na sekondari(kidato cha nne na cha sita). Uzembe niuongeleao ni huu wa kukosewa kwa baadhi ya maswali ya mitihani ya taifa inayosimamiwa na baraza la mitihani la taifa.
Mitihani hii pamoja na umuhimu wake kwa watahiniwa( kwani ndio inayoamua mustakabali wa watanzania wengi kimasomo na kimaisha kwa wale waliopata bahati ya kusoma na wale waliopata bahati ya kusomesha), imekuwa ikija na makosa mbali mbali ambayo mengine yanaweza kupelekea wanafunzi kuchanganyikiwa na kushindwa kufanya mitihani yao ipasavyo.
Nakumbuka wakati ninafanya mtihani wangu wa Chemistry wa kumaliza kidato cha sita, kuna swali lilikuwa limeandikwa hivi, .... 25cm3 of solution was prepared, and from that solution, 250cm3 was taken and titrated against..... Kiuhalisia haiwezekani kuchukua sentimita za ujazo 250 kutoka kwenye sentimita za ujazo 25. Ni kosa la uchapaji lakini kosa kama hili kwa hakika halikustahili na kama kungekuwa na umakini, pengine marekebisho yangewezekana kabla au wakati wa mtihani. Hakukuwa na marekebisho yoyote na hadi leo sijui baraza liliangaliaje swali hilo kwa wale waliolifanya. Na pia sijui kwa wale ambao hawakulifanya waliangaliwa vipi. Swali likuwa ni rahisi, lakini kwa kuwa lilikosewa na hakukuwa na marekebisho yoyote, basi yawezekana wapo wengi walioliacha na kulazimika kufanya maswali wasiokuwa na uhakika nayo wa kutosha.
Kosa kama hili, bila shaka lina athari kubwa tu kwa watahiniwa. Huu ni uzembe kwa baraza la mitihani na pengine wizara ya elimu. Inashangaza mitihani hii muhimu kuwa na makosa kama haya. Maswali ya hisabati mathalani, yanakosewa na wanafunzi wanatumia muda mwingi kufikiria na kukokotoa maswali yasiyowezekana, halafu mwisho wa siku wanaanguka na somo la hesabu linachukuliwa kuwa ni gumu.
Kukosewa huku kwa mitihani kunakatisha tamaa kwa wanafunzi walio na roho nyepesi. Maswali yanaonekana ni magumu kumbe yanaupungufu.
Practical ya somo la fizikia katika mtihani wa kidato cha nne mwaka huu ulileta kizaazaa pale ambapo maelezo ya utangulizi ya uandaaji wa practical hiyo yalipokuwa tofauti na miongoni mwa maswali yaliyokuwemo kwenye mtihani. Kuna "mass" iliyotakiwa kuandaliwa kabla, lakini maelezo ya awali hayakusema hivyo. Wanafunzi walipotaka kuitumia "mass" hiyo, hawakuiona na hapo ndipo kasheshe ilipoanzia.
Hali ile iliwasumbua akili kwa kiasi chake. Juhudi za ziada ilibidi zifanyike kuwasiliana na wahusika ili kutatua kadhia hiyo. Hapa nalazimika kujiuliza kama mitihani hii huwa inafanyiwa uhakiki au la? Je, kama unafanyika, ni wa umakini kweli? NECTA yapaswa kuwa zaidi ya makini!
Ni uzembe mkubwa kabisa kwa makosa kama haya kujitokeza, hususani kwa mitihani hii muhimu inayoamua mustakabali wa mtu kimasomo na kimaisha.
Kinachonishangaza zaidi ni kuwa, kwa makosa kama haya na mengine, vyombo husika, NECTA na wizara ya elimu huwa havitoi tamko lolote kuelezea yaliyotokea na pengine kutoa sababu na pia kueleza ni hatua gani watachukua na hata kuwaomba radhi watahiniwa, walimu na wananchi kwa usumbufu uliojitokeza. Kinyume chake, huwa wanapiga kimya na kufanya kwa kadiri ya wao waamuavyo.
Wito wangu kwa baraza la mitihani na wizara ya elimu ni kuwa, umakini uongezwe katika swala zima la kuandaa mitihani ya taifa. Mitihani ile inapaswa ije na ukamilifu wake. Mitihani ya taifa kama haitaandaliwa vizuri kwa umakini, basi hata hatma ya wanafunzi nao ni wazi haitakuwa na nzuri. Kuna wanafunzi ambao kwa sasa wapo kwenye mazingira magumu ya kushindwa kuendelea na masomo baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa na yawezekana ni kwa sababu ya uzembe wa vyombo husika. Kwa mfumo wetu wa elimu, baraza la mitihani lazima mtambue ninyi mna mustakabali wa watahiniwa wa kila mwaka, kimasomo na kimaisha, hivyo muwe makini katika utaratibu mzima wa uandaaji mitihani ili basi watahiniwa wasilazimike kucheza mchezo wa patapotea. NECTA ijitahidi na ihakikishe haiwi miongoni wa sababu za wanafunzi kufeli.

1 comments:
Uliyosema yote ni kweli, kuna hatari kama mfumo wa mitihani hautabadilika.
Post a Comment