Kati ya vitu nivipendavyo katika maisha ni kusafiri, hususani kutembelea sehemu ambazo ni ngeni machoni mwangu. Pamoja na sababu nyingine muhimu, hili nalo limekuwa miongoni mwa sababu zinifanyazo kwa sasa nirindime nikiwa hapa Singida.
Nipo kijijini Siuyu. Ni mbali kidogo na Singida Mjini. Nauli ya kwenda na kurudi ni shilingi za kitanzania Elfu nne. Ni pesa nyingi hizi, kwa kuzingatia hali halisi ya asilimia kubwa ya wakazi. Barabara iunganishayo mji na kijiji hiki pamoja na vya jirani haipo katika kiwango cha lami, si nzuri ya kuridhisha, hivyo magari ya abiria ni machache.
Kwa kuzingatia uchache wa magari yapitayo katika barabara hii, magari hayo pamoja na kuchukua abiria, lakini pia yamekuwa yakibeba hata mizigo mingine kama nondo, mbao, mabati n.k Hakika swala la usafiri katika kijiji hiki na vijiji jirani kama Unyamikumbi, Ughaugha, Ngaghe na Unyaghumpi pamoja na vijiji vingine bado ni tatizo kubwa. Gari la abiria laweza kusubiriwa hata kwa zaidi ya masaa mawili hadi matatu.
Heka heka za uchaguzi zipo kwa kiasi kidogo sana. Ni mara chache sana utawakuta watu wamekaa wakijadili hili na lile kuhusu uchaguzi mkuu. Uelewa wa wanakijiji kwenye swala zima la uchaguzi si wa kuridhisha sana. Nilishangaa pale nilipomdadisi mama mmoja kuhusu wagombea wa kiti cha uraisi, aliponiuliza maswali kadhaa kuhusu dokta Slaa ambaye kwa mujibu wa huyu mama alisema kuwa amekuwa akimsikia sikia kwenye redio. Maswali aliyonitupia mama huyu ni kama, dokta Slaa anatokea wapi, ana elimu gani na anagombea nafasi gani ya uongozi. Niliwaza kama kosa ni la mwanakijiji huyu au ni la mgombea ameshindwa kumfikia mwananchi huyu. Hili bila shaka ni changamoto kwa wapinzani.
Karibu na ninapoishi, kuna eneo lenye maduka na sehemu ya vinywaji. Mida ya jioni vijana kwa wazee huonekana kwa wingi.
Vikundi vya wazee huonekana mida ya kuanzia saa kumi jioni wakicheza bao. Nilishangaa sana kuwaona vijana muda wa mchana wakicheza pool table na vijana wengine vijiweni wakicheza karata. Ni hatari kwa maendeleo yao na ya taifa.
Wengi wa wakazi wa hapa wanaonekana kutokuwa na kazi maalumu za kufanya. Mengi ya makazi ya wakazi bado ni duni kwa hakika. Maliwato kwa mfano, nyingi zikiwa ni zile zilizozungushiwa matawi ya miti kama namna ya kuwasitiri watumiaji.
Nilifanikiwa kupita kwenye baadhi ya vijiji kama Ngaghe, Unyaghumpi na Makyungu. Vijiji viwili nilivyotangulia kuvitaja hali yake si ya kuridhisha hata kidogo. Makazi ni duni hasa. Hali ngumu ya upatikanaji wa maji na huduma nyingine za kijamii. Katika vijiji hivi, kwa sehemu nilikopita, sikubahatika kuona nyumba yenye kutumia nishati ya umeme. Ajabu kabisa, niliona juu ya baadhi ya nyumba za tembe, bendera za CCM zikipepea. Niliwaza sana nini maana ya bendera hizo. Kwamba tumaini lao limelala hapo, au ni ushabiki tu, au wameridhika kwa mema waliyofanyiwa, au hasa ni nini? Tatizo la makazi, usafiri na shida ya maji, vyote vyawakabili wanakijiji hawa wapeperushao bendera za CCM juu ya nyumba zao za tembe. Nyaya za umeme niliziona zikiambaa ambaa kuelekea kijiji cha Makyungu chenye mwamko mkubwa wa maendeleo. Kaya karibu zote za vijiji vya Ngaghe na Unyaghumpi hazitumii nishati hii ya umeme.
Katika kijiji cha Makyungu, nilifurahi kuona nyumba nyingi zenye hadhi nzuri na ubora tofauti na vijiji vingine ambapo makazi bora yanahesabika. Kulikuwa na shughuli mbalimbali za kibiashara.
Jamii kubwa kabisa ya wakazi wanyeji hawa ni wanyaturu. Asilimia kubwa ya mawasiliano hufanywa kwa kinyaturu, kuanzia wazee, vijana na watoto. Hakika walimu wa shule za msingi wana kazi kubwa ya kuhamasisha watoto kuongea kiswahili na ndipo ifuate tena kazi nyingine ya kufundisha kiingereza. Hili ni tatizo sana hususani kwa waalimu ambao sio wazawa. Bila shaka tatizo hili lipo hata kwa shule za sekodari za kata.
Nimalizie kwa kuwajuza wachaga, hususani wanaume. Eti wanasema mchaga mwanaume akishaingia Singida harudi, hususani kwa wanyaturu. Wanawake wa kinyaturu kwa mujibu wa wenyeji ,huona fahari sana kuolewa na wachaga, sijajua ufahafari hasa watokana na nini. Ati siku moja nilishangaa kuambiwa kuwa ile "laki saba" ya mahari imekwisha, wanategemea kupokea nyingine kutoka kwangu.
Inamaana nami sitatoka tena huku?
Hadi wakati mwingine, ni "Chasaka" mimi, jina nijipalo kwa kuwa tu nipo ugenini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

0 comments:
Post a Comment