Ni wakati wa kutoa ahadi za kukamilisha ukarabati wa vipande vya barabara, ni wakati wa kusikia ahadi za kukamilisha vyumba vya madarasa, ni wakati wa kutoa ahadi za kusaidia vituo vya watoto yatima, ni wakati wa kuelezea namna rasilimali za nchi zinavyotafunwa, ni wakati wa kuahidi kuchimba visima vya maji. Huu ndio wakati wenyewe.
Kwa kweli ni wakati mwingine tena wa ahadi kemkem ambazo kwa kuzisikiliza tu, zina kila aina ya ushawishi. Ajabu kabisa, watu wanakuja na matatizo yanayolikabili eneo fulani na kugongea msumari hapo hapo. Wananchi kwa kutambua kuwa matatizo yao yatakwisha, wanafurahia kwa chereko na vifijo.
Ndio utaratibu wetu wa kampeni. Ni kampeni za mfumo wa ahadi. Wananchi nasi twabweteka, baada ya uchaguzi, twasubiria yaliyoahidiwa kuja kutimizwa. Mwishowe tunarudi kule kule kwa mjomba aliyechukua vipimo vya miguu kwa kamba kwa lengo la kutuletea viatu, baada ya miaka minne anakuja kutuambia tuliopimwa tusihofu, viatu vitaletwa, tuwe na subira.
Binafsi natamani kuona wale wanaofundisha mbinu za kutuwezesha kujichimbia visima, wale wanaotupa mbinu za kutuwezesha sisi wenyewe kujijengea madarasa kwa ajili ya wanetu, wale wanaotupa uhuru wa kuzisimamia rasilimali zetu wenyewe. Nawapenda wale wasionipa fedha, bali wanaoniwezesha ili nami niweze kujitafutia mwenyewe.
Natamani sera namba moja ya kila mgombea ingekuwa ni ya kuhimiza uzalendo kwa taifa, uzalendo kwa watanzania, uzalendo kwa rasilimali zetu. Sera inayohimiza umoja wa kitaifa. Mbali na watanzania wenyewe kutambua kuwa wanatakiwa kujijengea moyo wa uzalendo na mshikamano, lakini pia wagombea nao wanatakiwa waitumie fursa hii ya kukutana na jamii kubwa ya Watanzania kuhimiza uzalendo na umoja/mshikamano. Hakuna chuo wala shule ifundishayo uzalendo wala umoja wa kitaifa, hakuna. Basi kwa wagombea, hii iwe ni fursa ya pekee. Watanzania mbali ya wao wenyewe kujijengea moyo wa kujituma kulitumikia taifa kiuzalendo, wagombea nao waitumie fursa hii ya pekee kuiamsha ari ya uzalendo na umoja kwa taifa na kwa watanzania.
Uzalendo binafsi nauona kuwa ni silaha muhimu sana kwa maendeleo yetu. Mwanajamii mwenye uzalendo atalitumikia taifa na watanzania kizalendo. Mzalendo wa kweli, hatafuja rasilimali za taifa, hataomba rushwa au kupokea rushwa, atakuwa mwadilifu na mchapa kazi kwa moyo wake wote.
Wakati wa kampeni usiwe ni wakati wa kutoa ahadi, uwe ni wakati wa kupanda mbegu za uzalendo, wakati wa kujenga umoja wa kitaifa. Uwe ni wakati wa kusema mambo ambayo utimizaji wake utawahusisha wananchi moja kwa moja na si ahadi ambazo huwabwetesha wananchi na kubaki wakisubiria ahadi zitimizwe.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Dunia nzima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

2 comments:
Kumbuka malaria ni mradi unaolipa vizuri unataka malaria iishe ? watakula wapi
Eheeeee! Viongozi wa aina hii hata na wananchi wanaojifaidisha kupitia mafungu ya kupiga vita magonjwa sugu kama malaria na Ukimwi ndio hatuwataki. Hatuwataki hao wachache wanaojineemesha na kufurahi kwa kuiona rasilimali watu ikiteketea. Hatuwataki hao maana hawana uzalendo na nchi yao, hawana uzalendo na watu wao.
Post a Comment